Search This Blog

Wednesday, October 23, 2013

ASHANTI YAFIWA, YAENDELEA NA MAZOEZI

KLABU ya Ashanti United ya Dar es Salaam, imepata msiba wa mmoja wa viongozi wake aitwaye Jimmy Mhango ambaye ni mjumbe wa bodi, lakini kikosi cha timu hiyo kinaendelea na mazoezi tayari kwa mchezo dhidi ya JKT Oljoro wiki ijayo.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Ashanti, Marijani Rajabu, Jimmy amefariki jana na taratibu za mazishi zinaendelea na msiba huo ni pigo kwao kwani marehemu alishiriki kwa asilimia kubwa katika mchezo uliopita wa timu hiyo.
“Marehemu alikuwa kiongozi shupavu na alishiriki kwa asilimia 100 katika michezo yetu mingi ambayo tulifanya vizuri na hata ile ambayo hatukufanya vizuri. Ifahamike tu kwamba huu si msiba mdogo kwa Ashanti na wadau wote wa soka wilayani Ilala,” anasema Marijani.
Alisema uongozi mzima wa Ashanti unashirikiana bega kwa bega na familia ya marehemu kufanikisha safari ya mwisho ya marehemu ambaye alikuwa mtu muhimu katika uongozi wa Ashanti.
Marehemu amewahi kuzichezea klabu za Ushirika ya Moshi na Pan African ya Dar es Salaam.
WAKATI HUOHUO, pamoja na msiba huo, timu ya Ashanti imeendelea na mazoezi yake kujiandaa na mchezo dhidi ya JKT Oljoro jumatatu ijayo kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.
“Timu bado ianendelea na mazoezi licha ya kuwepo kwa msiba huu na tunategemea tutapata muda mwingi wa mazoezi baada ya ratiba kusogezwa mbele kwa siku moja kupisha mechi ya timu ya taifa ya wanawake,” anasema Marijani.
Ashanti hadi sasa ipo nafasi ya 10 katika msimamo wa Ligi Kuu ya Bara ikiwa na pointi 9, Oljoro ni ya 13 ikiwa na pointi 6. Timu zote zimecheza mechi 10.

No comments:

Post a Comment