Search This Blog

Saturday, August 24, 2013

KOCHA PATRICK LEIWIG: SHOMARY KAPOMBE ANAPOTEZA MUDA AS CANNES - HASTAHILI KUICHEZEA TIMU YA DARAJA LA NNE

KIRAKA wa Tanzania, Shomari Kapombe ametambulishwa juzi Ahamisi kwenye mazoezi ya klabu ya AS Cannes ya Ufaransa, lakini Kocha Mfaransa aliyetimuliwa Simba, Patrick Liewig amesema timu hiyo haina hadhi ya Kapombe.
Hata hivyo, Simba imemjibu Liewig kuwa asiwe na wasiwasi kwani tayari Kapombe anatakiwa na timu ya daraja la pili ya Ufaransa.
Liewig aliiambia Mwanaspoti kwa simu kutoka jijini Paris, Ufaransa jana Ijumaa kwamba klabu hiyo ya daraja la nne ni ya hadhi ya chini sana kulinganisha na ubora wa Kapombe ambaye alipaswa kuchezea madaraja ya juu hivyo Simba imempeleka sehemu anakokwenda kupoteza muda wake.
Liewig alisema; “Naijua Cannes ni timu ndogo sana, inashiriki daraja la nne ni ya chini sana kulinganisha na ubora wa Kapombe niliyemfundisha hapo Simba. Yeye hadhi yake ni daraja la kwanza au la pili, na zipo klabu nyingi tu ambazo angeweza kupata nafasi.”
“Simba na huyo wakala wanampotezea Kapombe muda wake, wachezaji wakubwa wa Tanzania wanapaswa kukaa chini na kujipanga. Klabu zikae na watu wa maana zifanye mambo kwa kufuata weledi, mimi najuana na watu wengi sana kuanzia makocha na viongozi ambao naweza kuwaunganishia wachezaji wa Tanzania na wakacheza soka daraja la kwanza.
“Mchezaji mwenyewe ajipange anifuate aonyeshe nia ya kweli mimi nitashirikiana na viongozi nitamsaidia, lakini huko alikokwenda Kapombe sijapaafiki,” alisisitiza kocha huyo ambaye bado hajapata dili mpya.
Katika klabu hiyo, Kapombe atajumuika na ‘Waswahili’ wanne kutoka Burundi, Uganda, Senegal na Togo.
Kapombe atakuwa katika klabu hiyo na iwapo atauzwa ndio Simba itapata mgawo wake.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Usajili wa Simba, Zacharia Hanspoppe aliliambia Mwanaspoti jana Ijumaa kuwa hawana wasiwasi na suala hilo kwani tayari Kapombe ameivutia timu ya daraja la pili.
“Sisi tunajiamini na mambo tunayoyafanya, hapo nazungumza na wewe nilikuwa napata mawasiliano kutoka Ufaransa kuwa kuna timu ya daraja la pili inamhitaji Kapombe. Hao AS Cannes wakimuuza Kapombe sisi tunapata asilimia 40,” alisema Hanspoppe.

SOURCE: MWANASPOTI

No comments:

Post a Comment