Search This Blog

Friday, July 19, 2013

Kilimanjaro: Taifa Stars itafanya maajabu Kampala

Na Mwandishi wetu,

Mwanza
Wadhamini wa timu ya Taifa (Taifa Stars) Kilimanjaro Premium Lager, wamesema wana imani Stars itafanya vizuri katika mechi ya marudiano na Uganda Cranes kuwania kucheza katika mashindano ya CHAN kwani maandalizi ni mazuri.
Hayo yalisemwa na Meneja wa Kampuni ya Bia Tanzania Kanda ya Ziwa, Malaki Sitaki wakati  TBL Mwanza  iliwaandalia chakula cha jioni wachezaji wa Stars.
Aliishukuru TFF kwa kuichagua Mwanza tena iwe Kambi ya timu ya Taifa kwani wakaazi wa Mwanza wanaipenda timu yao na wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kuangalia wachezaji wakiendelea na mazoezi chini ya Kocha Kim Poulsen.
“Tuna imani mutafanya vizuri ili twende CHAN….kama Waganda walitufunga bao moja kwetu sisi tuna uwezo wa kuwafunga mawili kwao,” alisema Bw Malaki.
Alisema kocha amefanya kazi nzuri tangu aanze kuifundisha Timu ya Taifa na anastahili pongezi kwa mafanikio aliyopata mpaka sasa.
“Matunda mojawapo tuliyoona ni kuwafunga vigogo kama Zambia, Cameroon na Morocco,” alisema na kuongeza kuwa Kilimanjaro Premium Lager iko pamoja na Stars kwani ushirikiano uliopo ni wa manufaa kwa pande zote.
Naye Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Saad Kawemba, aliipongeza Kilimanjaro Premium Lager kwa kuwa karibu na Taifa Stars wakati wote.
Alisema matokeo ya awali ya Stars kufungwa bao moja yasiwakatishe wachezaji na wananchi tama kwani kilichotokea ni matokeo ya mpira na Stars wanaweza kugeuza meza wakiwa Kampala.
Alisema Stars ilivyopiga kambi Mwanza mwaka jana kabla ya kwenda kwenye mashindano ya CECAFA ilishinda mechi tatu mfululizo kwa hivyo wanaamini safari hii pia kutakuwa na matokeo mazuri Kampala Jumamosi Julai 27, Stars itakapocheza na Cranes katika mechi ya marudiano.
Alisema wachezaji wanahitaji sapoti kubwa wakiwa Kampala na ni muhimu watanzania wanaoishi Mwanza na mikoa mingine ya jirani na Uganda wajitokeze kwa wingi katika mechi hiyo.
Naye kocha Kim Poulsen alisema wachezaji wako katika hali nzuri na ana imani watafanya kazi nzuri Kampala.

“Hali ya hewa ya Mwanza ni sawa kabisa na Kampala na wachzaji wameshazoea na wako katika hali nzuri ya mchezo,” alisema.

No comments:

Post a Comment