Search This Blog

Monday, June 17, 2013

UCHAMBUZI MCHEZO WA TANZANIA VS IVORY COAST - ILIKUWA LAZIMA IVORY COAST ISHINDE NDANI NA NJE YA UWANJA



TIMU ya soka ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars imefungwa mabao 4-2 dhidi ya Ivory Coast na kuzima harakati zake za kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia 2014 huko Brazil.
Watanzania wengi na wadau wa michezo walidhani Taifa Stars ingeweza kusonga mbele katika harakati hizo za kufuzu kucheza Kombe la Dunia 2014, lakini sasa ukweli umejidhihirisha.
Sasa wengi wamekubaliana na uhalisia wa mambo kwamba, inahitaji muda kidogo kuona Taifa Stars ikisonga mbele katika kuelekea kufuzu Kombe la Dunia na siyo rahisi kama ilivyodhaniwa hapo kabla.
Ni mambo mengi yaliyotokea katika mchezo dhidi ya Ivory Coast ambayo yaliigharimu Taifa Stars licha ya uwanja kujaa idadi kubwa ya mashabiki waliokuwa wakiishangilia timu yao bila kuchoka.
Jambo la msingi ni kwamba, Taifa Stars ikiwa katika harakati za kuhakikisha inafuzu Kombe la Dunia wengi tulisahau kwamba, kwa ‘reality’ ilikuwa ngumu kwa Taifa Stars kufuzu fainali hizo japokuwa kwa mapenzi tulidhani timu hii ingeweza kufuzu kwa kuanza na vipigo kwa timu za Morocco na Ivory Coast.
Tukitazama mchezo kati ya Taifa Stars na Ivory Coast kuna baadhi ya mambo yalionekana kwamba bado tuna safari ndefu ya kufuzu Kombe la Dunia kama kweli tuna nia ya kufanya hivyo.
Mambo mengi mno yalijitokeza katika mchezo kati ya Taifa Stars dhidi ya Ivory Coast na haya ni machache kati ya mengi yake;

TAIFA STARS ILICHEZA KUFURAHISHA MASHABIKI SIYO KUIFUNGA IVORY COAST
Kiungo wa Manchester City, Yaya Toure alicheza kama mshambuliaji na alitimiza majukumu yake kama straika hasa kwa kutokubali kukaa na mpira kwa muda mrefu licha ya kuwa na uwezo wa kufanya hivyo.
Wakati Toure mwenye uwezo wa kumiliki mpira atakavyo na kufanya jambo lolote hakutoa nafasi hiyo zaidi ya kutafuta ushindi kwa timu yake, viungo na wachezaji wengi wa Taifa Stars walikuwa wakitumia muda mwingi kukaa na mpira bila ya sababu ya msingi.
Kiungo Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ mara nyingi alikuwa kitumia muda mwingi kukaa na mpira na kutaka kupambana na wachezaji wa Ivory Coast licha ya kuonekana wazi kwamba mara zote alizidiwa nguvu.
Tazama hata Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto na Frank Domayo walikuwa wakitumia muda mwingi ‘ku-hold’ mipira huku wakitoa pasi zisizo na macho na kujikuta wakipoteza mipira mingi kutokana tu na vitendo vyao vya kuchelewesha mipira.
Pamoja na vitendo hivyo kuwa hatari kwa timu, lakini mashabiki walikuwa wakiwashangilia kwa nguvu viungo wa Taifa Stars bila ya kujua madhara ya kufanya hivyo. Hao walijali zaidi kushangiliwa kuliko umuhimu wa mchezo husika.
Taifa Stars ilihitaji zaidi kucheza kwa kutokubali kukaa na mpira kwa muda mrefu kwa wachezaji wake ili kuitengeneza nafasi za haraka za kupata bao ili iweze kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele.
Kuanzia Sure Boy, Kiemba, Kazimoto na Domayo, wote walionekana kufurahishwa na kelele za mashabiki waliokuwa wakiwashangilia kutokana na chenga na madoido mengine waliyokuwa wakiyafanya uwanjani.

SAFU YA ULINZI ILIPAPARIKA
Ilikuwa kama kila mchezaji ameahidiwa kiasi kikubwa cha fedha, kwani mara nyingi wachezaji wa Taifa Stars hawakucheza katika nafasi zao na hilo liligharimu timu na kujikuta wakilala mabao 4-2.
Erasto Nyoni ndiye beki anayeweza kuondoka na lawama nyingi lakini halikuwa kosa lake wakati mwingine kwani alilazimika kwenda katikati kusahihisha makosa ya mabeki wa kati na kuisahau nafasi yake.
Ilionekana wazi kwamba yalikuwepo mawasiliano hafifu juu ya kutengeneza mtego wa kuotea yaani ‘offside trick’ na matokeo yake Ivory Coast walitumia vyema mwanya huo na kujipatia mabao manne.
Baada ya kuonekana ‘njia’ tangu dakika za mwanzo, beki Erasto Nyoni inaonekana hakupata ushauri wa kutosha kuhusu kutulia na kucheza soka kwani hata makelele ya mashabiki yalimfanya aonekane mtu asiyefaa kikosini. Lakini alikuwepo benchi anayeweza kumudu nafasi yake moja kwa moja?

NGUVU HAFIFU
Wachezaji wengi wa Taifa Stars walionekana kutokuwa na nguvu ya kupambana na wenzao wa Ivory Coast kutokana na hali halisi ya miili yao.
Sure Boy mfupi na mwenye mwili mdogo alionekana kama mchezaji wa kawaida mbele ya Yaya Toure mwenye mwili mkubwa na nguvu, na mara nyingi Toure aliiwahi mipira ambayo ingeweza kuwahiwa na Sure Boy.
Domayo naye hakuweza kufua dafu mbele ya Traore Lucina na Jean Jacques ambao wote ni watu wa miraba minne. 
   
WAO WALIMKATAA KALOU, SISI TUKAFUATA SAMBUSA
Kabla hata ya mapumziko, waandishi kadhaa wa Ivory Coast walionekana kutopendezwa na uchezaji wa Salomon Kalou ambaye muda mwingi kila alipopewa mpira alikuwa akitaka kukaa nao kwa muda mrefu kama ilivyokuwa kwa kina Sure Boy na wengine wa Taifa Stars.
Waandishi hao walionekana wazi kuchukizwa na hali hiyo na mara kwa mara walionyesha wazi kutoridhika na uchezaji wa Kalou.
Ulipofika wakati wa mapumziko, waandishi hao walishuka chini katika vyumba vya kubadilishia na kuzungumza na baadhi ya maafisa wa timu yao ili kutazama uwezekano wa kumpumzisha Kalou kwa maslahi ya nchi.
Wakati hayo yakitokea kwa Ivory Coast, waandishi wa Tanzania walikuwa wamekaribishwa ukumbi wa VIP kupata vitafunwa kama sambusa, mishikaki na vinywaji baridi, hao hawakuwaza kupeleka mawazo yao kwa benchi la ufundi na hata wangefanya hivyo wasingesikilizwa kutokana na utaratibu ulivyo.
Mbaya zaidi siyo waandishi tu, hata viongozi kadhaa wa Kamati ya Ushindi ya Taifa Stars nao walionekana wakiwa VIP wakijichana kana kwamba Taifa Stars ipo katika nafai nzuri. Kumbuka hadi muda huo timu ilikuwa ipo nyuma kwa mabao 3-2.
HONGERA ULIMWENGU
 
Kama kuna mchezaji wa Ivory Coast aliyeomba mpira uishe haraka kuliko wengine basi ni Bamba Souleman ambaye alikuwa akicheza kama beki wa kati anayemkaba mshambuliaji wa Taifa Stars, Thomas Ulimwengu.
Ulimwengu alimmudu vizuri Bamba kiasi cha kumkimbiza na kuufanya mpira atakavyo hadi kufunga bao moja. Mara nyingi Bamba alizidiwa nguvu na kasi na Ulimwengu kiasi cha kulalamikiwa na wenzake.
Kama wachezaji wanne tu wa Taifa Stars wangeweza kucheza kama Ulimwengu, ni wazi timu hiyo ingepata matokeo mazuri na ya kuridhisha.  

BY ELIUS KAMBILI

8 comments:

  1. Nimesoma makala yako na nimekubali. Kwa kuongezea tu. Code voire walichofuata ni matokeo ss hatujitambui na hatutajitambua kwa kuwa tunategemea mpira uamuliwe na dua za watanzania na nasaha za viongozi kwa wachezaji. Tizama benchi letu la stars na kila mmoja aulizwe nn kilichomuweka pale ni kichekesho kitupu utakaposikiliza maelezo yake.mwisho hata ukisoma magazeti yetu jinsi yalivyoripoti mechi hiyo hadithi nihiyohiyo ya sambusa bagia na soda za mechi ijayo .niandike vzr ili nisikosane na fulani mwenye dhamana pale au nisimkosoe mchezaji fulani kwa kuwa anatoka timu yangu Mungu akupe nn umepata bao dk 1 . Unataka dua gani? Ya watanzania.

    ReplyDelete
  2. nakubaliana na wewe,ila tukubali tukatae,Erasto Nyoni ndiye aliyetuchomesha jana,na si jana tu,bali mechi 2 za nyuma nazo alituchomesha pia.Wasaidizi wa Kim hawajui wajibu wao bali kuendelea kubeba wachezaji wanaotuliza washabiki kila siku.

    ReplyDelete
  3. Naheshimu sana baadhi ya chambuzi zako mwenye blog ila hapa ngoja nikuweke sawa. Punguza jazba maana umekaa mkao wa lawama zaidi wakati unafaham kwenye soccer pale unapokosea ndipo unaumizwa. Unatumia maneno ya wao taifa stars wakati ni timu yetu wote wadau wa mpira Tanzania.

    Suala la kukaa na mipra.
    Shafi huwez kuwa na pass za haraka kamaunavyodhan pasipo kuwa na uwezo wa mpira wa kasi. Sure boy aliyecheza ndiye yule yule wa azam tatizo tumefungwa. Kiemba alijituma sana na ilimpasa akae na mpira na alimudu kufanya hivyo maana nae si mtu wa kasi. Nadhan ulihitaji wacheze kama kina iniests jambo ambalo hata ww ungepewa timu isingewezekana. Flopy kwenye mido ni domayo sawa maana alionekana kuwa na hofu baada ya kuzidiwa kati.

    Kuhusu defence nakubaliana na udhahifu ila sio wa kudhihaki kama unavyosema waliahidiwa pesa. Kumbuka walitumia nguvu zao kulibeba taifa na wewe kama mfau sio unapopata matokeo mabaya unajitoa kifua mbele kukashifu.

    WAtanzania wenzangu hafa ninyi wenye access za media nitaendelea kuwanyooshea vidole kwa kuwa mnatoa mchango wa kudhihofisha zaid kuliko kusaidia.

    Sasa umekuwa mdaku kuangalia watu wanaenda kula sambusa. Je ni kwel waandishi wote wa ivory walishuka kutoa mapendekezo? Na je ulipoona wanakula sambusa ulichukua hatua gani?

    MAJUNGU SI MTAJI ndugu zanguni. Jambo la kitaifa linaanza kuleta kelele. Haya kazi ya sisi mashabiki ni kushangilia mwanzo mpaka mwisho wa game sijui ulitaka tuboo!

    Kweli ulimwengu alikuwa shujaa ila je angecheza mwenyewe uwanjani angeweza? Kila mmoja ametoa mchango wake pale.

    NI HAYO TU.

    ReplyDelete
  4. Hii ni tathmini ya kukurupuka kama ilivyo kawaida yetu wabongo.Tathmini hii imejikita katika hisia badala ya uhalisia na kwa haraka haraka unaweza kukisia iliandikwa kwa hisia za kabla ya mechi na siyo matukio halisi ya wakati wa mechi.Wachezaji wetu walicheza kwa maelekezo ya kocha na walichokifanya ndiyo uwezo wao ulipoishia.Tulichozidiwa ni mbinu za mchezaji mmoja mmoja ambazo wenzetu wako juu kutokana na uzoefu wao wa mechi za aina hii.Tunapenda kupata tathmini kutoka kwa kwa makocha, wataalamu halisi wa soka na wachambuzi huru badala ya uchambuzi wa hapo juu ambao ni dhahiri umefanywawa na mtu ambaye hata kabla ya mechi tayari alikuwa anaiombea mabaya stars na pia ana maslahi kwenye uchaguzi mkuu wa TFF

    ReplyDelete
  5. Bado tunaweza cha msingi tusikate tamaa bali tuendelee kujituma zaidi.!

    ReplyDelete
  6. mimi nimeona mambo kama matatu,kwanza ni kutoelewanba kwa wachezaji kwani hata magoli tuliyofunwa ni marahisi sana,
    pili psychologically wachezaji wa TZ kama dumayo,na nyoni walipaniki,
    labda la tau na la kuongezea ni kuwa tukubali tukatae uwezo wetu mdogo,,kama ligi ni mbovu unategemeaje kupata wachezaji wazuri timu ya taifa??
    mapendekezo::lets invest in football,,haya mashindano makubwa sio ndo mwisho wake kwani sio mda yatakuja ya chan na baadae mataifa AFRICA,nguvu tulizotumia kutka kwenda brazil ndio tutumie hizo hizo kutengeneza timu bora ya TAIFA ya miaka ijayo,,
    ni hayo tu

    ReplyDelete
  7. nakubaliana kabsa na bwana Geogre Paskal

    ReplyDelete
  8. shaffih hukutuchambulia mechi ya tanzania 3 morocco 1 kwa nini umechambua kwa haraka sana mechi hii tanzania 2 ivory coast 4

    ReplyDelete