Search This Blog

Sunday, June 23, 2013

MAKALA: VIONGOZI SIMBA WANAJISAFISHA KWA MAJI MACHAFU, WAMLIPE LIEWIG



ALIYEKUWA Kocha wa Simba, Patrick Liewig yupo nchini akisota kuhusu malipo yake ya kusitishiwa kwa mkataba wake baada ya kutumikia timu hiyo kuanzia Januari mwaka huu.

Kutokana na kusitishiwa mkataba wake, Liewig anaidai Simba kiasi cha dola 26000 ambacho ni zaidi ya Sh. 41.6 milioni. Lakini uongozi wa Simba unadai unadaiwa dola 20,000 pekee ambazo ni zaidi ya Sh. 30 milioni.

Iwe Liewig ameongeza au kupunguziwa kiasi anachoidai Simba, ukweli ni kwamba klabu hiyo inadaiwa na kocha aliyekuwa akiifundisha. Ni lazima Simba ilipe hakuna ubabaishaji katika jambo hili.

Kuna jambo la kushangaza linaloendelea kila kukicha katika klabu kongwe za Simba na Yanga hasa katika hali ya kufukuza makocha. Mara huwa hazina sababu ya msingi.

Suala la kujiuliza ni kwamba, usajili wa wachezaji na makocha huwa unafanywa na watu makini au hufanywa kwa lengo la kunufaisha watu fulani hasa wapiga kura?



MADUDU YA BASENA HUKU UONGOZI UKIJISAFISHA KWA MAJI MACHAFU
Ndani ya miezi 11, Simba imefundishwa na makocha watatu ambao wote walitimuliwa kwa mtindo unaofanana tena kwa kashfa juu. Alianza Moses Basena raia wa Uganda.

Huyu aliifundisha timu hii kwa mafanikio lakini katikati ya msimu wa 2011/12, alitimuliwa na nafasi yake ikachukuliwa na Milovan Cirkovic. Wakati anatimuliwa Basena tuliambiwa eti hakuwa na vyeti.

Sababu hiyo haikuwa na mashiko na ilionekana kukaa kishabiki zaidi huku uongozi ukitaka kujiosha kwa wananchi kwa kutumia maji machafu kwani ni wao kwa kutokuwa makini kwao ndiyo waliompa kazi Basena akiwa hana vyeti.

Kwa kuonyesha kwamba sababu ya kumtimua Basena haikuwa na mashiko, timu hiyo ilimrejesha kikosini kama meneja wa timu aliye chini ya Liewig na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.

MILOVAN NA GHARAMA ZA UONGO
Baada ya Basena kuondoka, Simba iliamua kumpa kazi Milovan ambaye aliipa Simba ubingwa Ligi Kuu ya Bara msimu wa 2011/12 na hata kuifunga Yanga mabao 5-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika hali ya kawaida mwajiri yeyote huwa hayupo tayari kumpa kazi mtu ambaye atashindwa kumlipa, Simba haikudumu na Milovan kwa maelezo kwamba haiwezi kumudu gharama zake.

Viongozi wakamngoja Milovan ameenda kwao Serbia kupumzika huku wakimhaidi kumtumia tiketi ya ndege ya kurudi nchini, wakamchunia na moja kwa moja wakamtumia barua pepe kwamba kazi basi.

Milovan hakuwakawiza Simba, akawafuata na kudai haki zake ambazo alilipwa na mmoja wa wafadhili wa timu hiyo, Rahma Al Kharoos.

Sasa wakati Milovan anaondoka uongozi ulidai gharama za kuwa naye ni kubwa, ikaamua kumpa kazi Liewig raia wa Ufaransa kwa mshahara wa dola 6000 ambazo ni zaidi ya Sh. 9.7 milioni.

WASHINDWA KUMLIPA KOCHA WA BEI RAHISI
Watu walewale waliompa kazi Basena kisha kumtimua na kumrejesha Milovan pia wakamtimua, wakaamua kumpa kazi Liewig kwa kisingizio kuwa ni kocha wa bei rahisi.

Kweli Liewig alikuwa wa bei rahisi lakini alisimamia kwa kiasi kikubwa nidhamu ndani ya timu na hakuwa tayari kupangiwa timu na viongozi wababaishaji wasio hata kufundisha soka.

Baada ya kuona ubabaishaji unakuwa mwingi, Liewig aliamua kujenga timu wakati wenzake hawana mpango huo, akawajaza chipukizi kikosini mwake na moja kwa moja akaugawa uongozi.

Sasa kwa kuwa uongozi uligawanyika katika makundi mawili, moja lililokuwa likiunga mkono maamuzi ya Liewig ya kufukuza wachezaji watovu wa nidhamu na kuwatumia chipukizi.

Kundi hili linaundwa na viongozi vijana wengi ambao wanafikiria mbali kuhusu Simba, NA KUNDI LILILOBAKI ni lile la viongozi wanaopoteza muda ndani ya timu huku wakitaka sifa za kuwawezesha kwenda kupata nafasi nyingine za uongozi katika jamii.

Kweli wanaoweza wanaweza, lile kundi la viongozi wasio na malengo na Simba wakakwamisha malipo ya Liewig na kumwagia sumu afukuzwe kikosini na kweli wamefanikiwa.

VIONGOZI WAZURI HAWANA KITU, WENYE NAZO HAWANA MALENGO NA SIMBA
Simba sasa imegawanyika katika safu yake ya uongozi, kwani wale viongozi vijana au wasomi wenye nia ya dhati ya maendeleo ni wachache na wengi wao hawana uwezo hata wa kulipa mshahara wa mchezaji mmoja.

Hawa walijaribu kumkingia kifua Liewig lakini hawakufanikiwa kwani hawakuwa na nguvu ya kumbakisha klabuni. Nguvu hiyo ni kumlipa stahiki zake.

Lile kundi la pili la wasiotaka maendeleo ndilo lenye nguvu na ndilo lenye fedha za kuendesha klabu hata kulipa mishahara ya kocha. Hao ndiyo waliomtimua Liewig.

Itaendelea……

3 comments:

  1. viongozi wa soka hapa kwetu ni wababaishaji wakuu sio simba pekee.ila kwa simba yamezidi nq hayana kiwango wala mwelekeo nasikiyika kuwa wana simba walikuwa na tamaa ya kufanya vema sana kwa uongozi wa rage kwa mujibu ahadi zake inahuzunisha na kusikitisha yote yameota mbawa na rage na gange lake hawataki kuachia madaraka hali wanajua fika kuwa wameshindwa.

    ReplyDelete
  2. haya matimu ya kijinga yametuchosha sijui tufanye nini yashuke daraja au yafe kabisa



    ReplyDelete
  3. Kocha alijua fili tu ila tatizo lililopo soka letu viongozi wapo kwa maslai yao binafsi sio club.
    Maana kila mtu anatakiwa afanye kazi katika idara yake.
    Na ubadilishaji wa makocha ni matatizo sana.
    Na mbaya zaidi mizengwe ni mingi sana, kocha msaidizi anamadaraka kama mkuu na mbaya zaidi msaidizi ndio anaesababisha haya yote na mbaya zaidi kikitokea chochote anamgeuka hiyo fitina mbaya sana ata mungu apendi.

    ReplyDelete