Search This Blog

Friday, May 3, 2013

KAMATI YA UTENDAJI YA TFF SASA KUKUTANA KUPANGA NAMNA YA KUTEKELEZA MAAGIZO YA FIFA KUHUSU UCHAGUZI MKUU

Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inakutana Mei 9 mwaka huu jijini Dar es Salaam kupokea na kupanga utekelezaji wa maagizo ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kuhusu uchaguzi wa shirikisho.

Kikao hicho cha dharura chini ya Uenyekiti wa Rais wa TFF, Leodegar Tenga kitakuwa na ajenda hiyo moja tu katika kuhakikisha utekelezaji wa maelekezo ya FIFA unafanyika haraka ili uchaguzi ufanyike ndani ya muda uliopangwa.

FIFA katika maelekezo yake imetaka kwanza ziundwe Kamati ya Maadili na Kamati ya Rufani ya Maadili kabla ya kuingia kwenye mchakato wa uchaguzi wa Kamati mpya ya Utendaji ya TFF. FIFA imeagiza uchaguzi uwe umefanyika kabla ya Oktoba 30 mwaka huu.

KILA LA KHERI AZAM KOMBE LA SHIRIKISHO
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaitakia kila la kheri timu ya Azam katika mechi yake ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika itakayochezwa Morocco kesho (Mei 4 mwaka huu).

Mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya pili ya michuano hiyo itachezwa jijini Rabat kuanzia saa 11 jioni kwa saa za Morocco. Timu hizo zilitoka suluhu katika mechi ya kwanza iliyochezwa jijini Dar es Salaam wiki mbili zilizopita.

Azam iko nchini Morocco kwa karibu wiki nzima sasa ikijiandaa kwa mechi hiyo chini ya Kocha wake Stewart John Hall. Msafara wa Azam nchini humo unaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Eliud Mvella.

25 WARIPOTI KAMBINI YOUNG TAIFA STARS
Wachezaji 25 kati ya 30 walioitwa na Kocha Kim Poulsen kwenye kikosi cha pili cha Taifa Stars (Young Taifa Stars) wameripoti kambini ambapo mazoezi yalianza tangu jana jioni (Mei 2 mwaka huu).
Kocha Kim amewaitaka wachezaji katika kambi hiyo ya siku tano ili kuangalia uwezo wao katika maeneo kadhaa kwa lengo la kupata baadhi ambao anaweza kuwajumuisha kwenye kikosi cha Taifa Stars siku za usoni.

Wachezaji watano walioshindwa kujiunga katika kambi ya timu hiyo iliyoko hoteli ya Sapphire jijini Dar es Salaam ni Aishi Manula, David Mwantika, Himid Mao, Samih Nuhu na Seif Abdallah ambao wako Morocco na timu yao ya Azam.

KAMATI YA MASHINDANO KUPITIA MAANDALIZI RCL
Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inakutana Jumapili (Mei 5 mwaka huu) kupitia maandalizi ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) iliyopangwa kuanza Mei 12 mwaka huu.

Tayari mikoa 18 kati ya 27 kimpira imeshapata mabingwa wao kwa ajili ya RCL itakayotoa timu tatu zitakazopanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao (2013/2014).

Kamati hiyo chini ya Uenyekiti wa Blassy Kiondo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF itapokea taarifa ya maandalizi ya ligi hiyo kutoka Idara ya Mashindano ya TFF na kufanya uamuzi juu ya mikoa ambayo haijawasilisha mabingwa wao.

Ligi hiyo itachezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini, na ratiba (draw) itapangwa wakati wowote. Ada ya kushiriki ligi hiyo kwa kila klabu ni sh. 100,000 na usajili utakaotumika na ule ule wa ligi ngazi ya mkoa. Hakutakuwa na usajili mpya wa wachezaji.

No comments:

Post a Comment