Search This Blog

Thursday, April 4, 2013

WANANDINGA JKT RUVU SASA HAKUNA KULALA, WAHITAJI KUBAKIA LIGI KUU!


Na Baraka Mpenja  Dar es Salaam
Mlinzi wa kushoto wa klabu ya maafande wa jeshi la kujenga taifa wa JKT Ruvu kutoka mkoani Pwani, Stanley Nkomola, amesema ligi kuu soka Tanzania bara msimu huu ni ngumu sana kwao na wanahitaji kupigana kufa na kupona ili kukwepa panga la kushuka daraja.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na mtandao huu, Nkomola amesema timu ikiwa na pointi 31 kwenda juu inaweza kujinusuru na mkasi wa kushuka daraja, lakini chini ya pointi hizo inaweza kuporomoka daraja.
“kwa sasa tuna pointi 22 na aprili 10 tunakutana na wagosi wa kaya Coastal union uwanja wa mkwakwani Tanga, tunahitaji ushindi ili angalau tufikishe pointi 25 na kuendeleza harakati za kubakia ligi kuu msimu ujao”. Alisema Nkomola.
Mchezaji huyo aliongeza kuwa kila mchezaji sasa ametambua kuwa anatakiwa kuwajibika kwa nafasi yake, kwani klabu hiyo ikishuka daraja itakuwa balaa mkoani Pwani na jeshi kwa ujumla.
Pia Nkomola alisisitiza kuwa kubwaga manyanja kwa kocha wao mkuu Charles Kilinda kumewaathiri sana kiuchezaji kwani wamekosa mambo mengi ya kiufundi kutoka kwa kocha huyo.
“Unajua kuondoka kwa Kilinda ni sawa na kuondoka kwa mzazi, lakini tumejipanga ipasavyo kuibakisha timu ligi kuu na yeye atakaposikia atafurahi sana”. Aliongeza Nkomola.
Akiongelea suala la mashabiki wa klabu hiyo kukosa imani na timu hiyo, mchezaji huyo alisema klabu hiyo haiwezi kushuka daraja kutokana na mipango yao ya sasa.
Maafande wa JKT Ruvu wapo nafasi ya 10 katika msimamo wa ligi kuu, nyuma yao kuna timu za  Tanzania Prisons wenye pointi 20 nafasi ya kumi na moja, nafasi ya 12 wapo Africa Lyon wenye pointi 19, nafasi ya 12 wapo maafande wa Polisi morogoro wakiwa na poniti 18 na mkia unashikiliwa na Toto Africans wenye pointi 18.

No comments:

Post a Comment