Ni miaka takribani mitatu sasa tangu Inter Milan watwae makombe matatu(treble) kwa msimu mmoja ambao ulikuwa ni msimu wa mwaka 2009-10.Inter walitwaa makombe ya Escudetto(Serie A),Coppa Di Italia na Klabu Bingwa Ulaya.
Hakika ulikuwa ni msimu ambao utakumbukwa mno na Uongozi wa timu hiyo chini ya Rais Massimmo Moratti na pia wachezaji wa timu hiyo waliojitoa kwa jasho na damu kwa ajili ya kuipigania timu hiyo.
Tangu Inter watwae vikombe hivyo miaka mitatu nyuma,timu hiyo imeonekana kupoteza makali yake hivi karibuni na hata kushindwa kushika nafasi za juu za Ligi ya Italia maarufu kama Serie A.
Hali imekuwa ngumu kwao na hasa katika kipindi hiki ambacho Ligi ya Italia imepokonywa nafasi moja kati ya timu nne zinazotakiwa kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya huku nafasi hiyo ikienda katika Ligi kuu ya soka nchini Ujerumani’Bundesliga’.
Wengi wanafahamu kuwa soka la nchini Italia limepoteza mvuto hivi karibuni kutokana na mambo kadha wa kadha yakiwepo masuala ya viwanja kukosa mvuto,kashfa za upangaji matokeo mfano wa Calciopoli (2006) na Scommensiopoli (2011) na bila kusahau bei ghali za tiketi ambazo zinasababisha viwanja vingi nchini humo kukosa watu wengi wa kutazama mechi za Serie A.
Leo nataka kuizungumzia klabu ya Inter Milan ikiwa ni pamoja na kujibu maswali ya wadau wengi ya kwa nini Inter Milan hawafanyi vizuri hivi karibuni.
Tangu kuondoka kwa kocha Jose Mourinho mwaka 2010,Inter imekuwa katika wakati mgumu wa kupata kocha atakayerithi mikoba yake.Wamepita makocha takribani watano katika klabu hiyo kila mmoja akijaribu kufanya kile ambacho Jose Mourinho alikifanya kwa kutwaa vikombe vitatu ndani ya msimu mmoja wa 2009-10.
Makocha kama Rafa Benitez,Leonardo,Claudio Ranieri na Gian Piero Gasperin wamepitia klabu hiyo na wote wameambulia kufukuzwa na Rais Moratti.Kocha wa sasa Andrea Stramacchioni alionekana kuanza vyema msimu huu lakini kadiri muda unavyokwenda naye anaanza kupoteza matumaini ya klabu ya kuhakikisha inapata nafsi angalau ya tatu ya ili iweze kucheza mtoano katika Ligi ya mabingwa Ulaya.
Rekodi za Inter za msimu uliopita na msimu huu ni mbaya kwa ujumla na hazitofautiani sana ingawa kwa msimu huu Inter wameonekana dhairi kuendelea kushindwakuyafanyia kazi baadhi ya maeneo ambayo yaliwagharimu msimu uliopita.Maeneo hayo ni pamoja na sehemu ya ulinzi ambayo bado imeonekana pia kuwa na matatizo makubwa sana mpaka msimu huu.
Msimu uliopita Inter Milan waliruhusu jumla ya magoli 55 katika michezo 38 ya Serie A idadi ambayo ni kubwa sana kwa timu ya kariba yake ambayo kila msimu inataka kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.Na haikushangaza kuona ikishika nafasi ya sita katika msimu uliopita wa 2011-12.
Wachezaji wa msimu uliopita katika idara ya ulinzi karibu wote hawakufanua vizuri na wengi wao walikuwa ni maveterani kwani walikuwa na umri wa zaidi ya miaka 30 na wengi walikuwa wakianza katika kikosi cha kwanza.Mfano Lucio alikuwa na miaka 33,golikipa Julio Cesar alikuwa na miaka 32,Maicon 30,Walter Samuel 33,Ivan Cordoba 35,Cristian Chivu 31,Andrea Rannochia 23,Javier Zanetti 38,Yuto Nagatomo 25 na David Santon 20 na hivyo kufanya wastani wao wa umri kuwa miaka 29.
Msimu huu ikiwa ni raundi ya 32 katika Serie A tayari Inter wamesharuhusu wavu waokutikiswa mara 45 na hivyo kuendelea kuonesha kuwa bado kuna tatizo katika safu ya ulinzi ya timu hiyo.Uimara wa safu ya ulinzi wa klabu ndiyo msingi wa mafanikio ya timu yoyote ile.Wakati Inter wakiruhusu wavu wao kutikiswa mara 45wapinzani wao AC Milan wavu wao ulitikiswa mara 35,Juventus 20 na Napoli 30.
Tofauti ya msimu uliopita na msimu huu ni kuwa safu ya ulinzi ya klabu hiyo inaundwa na chipukizi wanaofanya vizuri na suala la muda tu watakuja kuwa mabeki wazuri sana.Nawazungumzia Juan Jesus (21),Andrea Rannochia(24),Yuto Ngatomo(26),Jonathan (27),Mattia Silvestre(27),Alvaro Pereyra(28),Walter Samuel (35),Ibrahim Mbaye(19),Javier Zanneti(39) nk ambao kwa ujumla wanatengeneza wastani wa miaka 27.Kwa kikosi kilichopo kinatoa ahueni kidogo kuhusu mustakabali wa timu hiyo kwa miaka 5 ijayo kwa wachezaji kama Rannochia,Juan Jesus,Yuto Nagatomo na Alvaro Pereira ambao wamekuwa wakipata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza mara kwa mara.
NINI KINAIGHARIMU INTER MILAN.
Kukosekana kwa uimara katika safu ya ulinzi kumekuwa ni tatizo kubwa sana kwa Inter msimu huu.Pamoja na kufanya vizuri kwa mabeki vijana nawazungumzia Rannochia na Juan Jesus lakini bado pengo la aliyekuwa beki na kiongozi wa ulinzi katika timu hiyo Lucio linaendelea kuonekana.Ni ukweli usiopingika kuwa Inter bado hawajampata mbadala wa beki Lucio ambaye alikuwa kiongozi uwanjani,alikuwa na uwezo wa kushambulia na kutengeneza nafasi za kufunga kwa washambuliaji.Mabeki waliokuwepo hawana uwezo wa kufanya hivyo kwa maana ya kusaidia safu ya kiungo katika kutengeneza mashambulizi.Safu ya ulinzi kwa msimu huu imeruhusu magoli 45 mpaka sasa katika mechi 32 kukiwa kumebaki mechi 6 kumalizikia kwa serie A.
Majeruhi ya wachezaji nyota.
Hili nalo limekuwa likiifanya klabu ya Inter kushindwa kuwa na muendelezo mzuri wa matokeo katika mechi za Serie A(consistency).Wachezaji kama Diego Milito,Walter Samuel,Gabby Mudingayi,Walter Gargano,Yuto Nagatomo,Christian Chivu,Rodrigo Palacios,Antonio Cassano,Estaeban Cambiasso wamekuwa na majeraha ya mara kwa mara na ni sehemu ya wachezaji wa kikosi cha kwanza hivyo kuipa wakati mgumu sana kikosi cha Inter kuweza kupata watu wa kushika nafasi zao .Inter wana kikosi kikubwa ila wengi wa nyota wake ni wapya katika timu hiyo hivyo wanahitaji muda wa kuzoeana na kuzoea pia mfumo wa mwalimu Andrea Stramacchioni.
Uongozi kutokuwa na maamuzi sahihi juu ya wachezaji chipukizi.
Nyota chipukizi kama Samuel Longo,Marco Livaja,Alfred Duncan na Phelipe Coutinho ambaye ameuzwa kwenda Liverpool walipaswa kubaki katika timu hiyo kwani walionekana kuwa ndiyo matunda ya klabu hapo badae.Lakini kutokupewa nafasi ya kucheza mara kwa mara kumewafanya nyota hao kuchukuliwa na vilabu vingine na kuonekana kuwa lulu katika vilabu vyao hivyo vipya.Mfano Phelipe Coutinho ambaye tangu amesajiliwa na klabu ya Liverpool mwezi januari mwaka huu ameonekana kufanya vyema sana.Katika mechi saba alizocheza mpaka sasa katika klabu hiyo ametoa pasi za magoli 3(Assist) na amefunga magoli mawili(2).
Lawama ziende pia kwa uongozi hasa mkurugenzi wa ufundi Marco Branca.
Kama kuna mtu/watu wa kulaumiwa katika kufanya vibaya kwa klabu ya Inter msimu huu basini uongozi mzima wa klabu ya Inter lakini hasa mkurugenzi wake wa ufundi Marco Branca.Marco ndiyo chanzo cha kuondoka kwa Wesley Sneidjer ambaye kwa kiasi kikubwa alihitajika katika kikosi cha Interkwa msimu huu ili kuiongezea nguvu safu ya ushambuliaji ya klabu ya hiyo.Uongozi umeshindwa kuonesha uelekeo wa klabu hiyo ya Inter kwa miaka inayokuja.Tatizo lingine kwa uongozi wa Inter Milan ni kushindwa kuwa na sera nzuri ya kuwalinda wachezaji wake chipukizi ili waje kuichezea timu hiyo kwa mafanikio makubwa hapo badae.
Wachezaji kama Leonardo Bonucci amekulia katika klabu ya Inter lakini uongozi wa Inter ukamwacha aende zake klabu nyingine na leo ni mmoja kati ya mabeki bora duniani akiwa na klabu ya Juventus.
Takwimu zinaonesha kuwa katika mwaka huu mpya wa 2013,Inter Milan imejikusanyia pointi 15 katika michezo minne.Wakishinda michezo minne,wakitoka sare michezo mitatu na kufungwa michezo saba.Siyo takwimu nzuri kwa klabu ya kariba ya Inter Milan ambayo ingependa kuwepo katika michuano yenye utajili mkubwa sana kwa upande wa vilabu michuano ya Klabu Bingwa Ulaya.
NINI KIFANYIKE.
Nashauri nafasi ya kurugenzi ya ufundi aje mtu mwingine kuchukua nafasi ya Marco Branca.Branca kaifanyia makubwa klabu ya Inter Milan lakini umefika wakati sasa wa kuangalia watu wengine wenye uwezo wa kuiongoza idara ya ufundi.Nampendekeza bosi wa zamani wa vilabu vya Lecce na Fiorentina Pantaleo Corvino kuchukua nafasi hiyo.
Kutafuta washambuliaji wenye uwezo ili kuipa nguvu safu ya ushambuliaji.Diego Milito alikuwa na msimu mzuri sana lakini majeraha yamekuwa yakishusha kiwango chake hivyo Inter haina budi kuanza kuangalia nyota wengine wenye uwezo wa kuziba pengo lake.Pia katika idara hiyo huwezi kumsahahu mshambuliaji Rodrigo Palacios kwani amekuwa na msaada mkubwa sana kwa klabu ya Inter tangu aliposajiliwa akitokea klabu ya Genoa.
Tatizo ni kuwa Milito ana 34,Palacios ana 30,Cassano ana 30 na Thomasi Rocchi ana 35 hivyo Inter inabidi waiangalie pia safu ya ushambuliaji kwa jicho la tatu.Nawapendekeza Carlos Tevez(Man City),Kevin Gameiro(PSG),Cavani(Napoli) na Radamel Falcao(Atletico Madrid) na Mario Gomez(Bayern Munich).
Hao ni nyota naoamini kuwa wana uwezo wa kuleta ufanisi mkubwa katika sehemu ya ushambuliaji.
Kuongeza nguvu katika sehemu ya ulinzi.Kumekuwa na tatizo katika safu ya ulinzi tangu waondoke akina Maicon,Luico na pia majeraha ya mara kwa mara ya mabeki Walter Samuel pamoja na umri wao vinachangia klabu ya Inter kufanya vibaya katika safu ya ulinzi.
Mabeki chipukizi Ranocchia na Juan Jesus wanafanya vizuri lakini wanakosa uzoefu na kiongozi katika eneo hilo.Ni ukweli ulio wazi kuwa pamoja na umri kuonekana kumtupa mkono,bado Inter hawajampata mbadala wa beki Lucio.Hivyo ni jukumu la uongozi kuingia katika soko la usajili kutafuta wachezaji wa safu ya ulinzi.Nawapendekeza Matts Humels/Neven Subotic(Dortmund),Nemanja Vidic(Man United),Facundo Roncaglia(Fiorentina) na Ezequel Garay(Benfica).
Edgar Kibwana
Email.edgarkibwana@gmail.com
Email.edgarkibwana@gmail.com
No comments:
Post a Comment