Search This Blog

Saturday, April 27, 2013

GEORGE BANDA: KINDA LA YANGA LINATOSHIA UWEPO WA JERRY TEGETE KIKOSI CHA KWANZA



KOCHA wa Simba, Patrick Liewig amethubutu kuwatumia vijana kwenye kikosi chake bila kujali matokeo ya timu hiyo kwenye ligi.
  
Mfaransa huyo mwenye msimamo na kazi yake alisema; "Nitawatumia wachezaji vijana kwenye kikosi changu hadi ligi itakapomalizika bila kujali matokeo ya timu.

"Ni vijana ambao wameonyesha nidhamu ya hali ya juu na moyo wa kujituma uwanjani kwa ajili ya timu yao.Binafsi ninavyojua, hakuna mchezaji anayeweza kuwa juu ya timu. Nafikiri bila nidhamu, hatuwezi kufikia kwenye malengo ambayo tumejiwekea." alisema kocha huyo.

George Banda ni mshambuliaji wa Yanga aliyepandishwa kikosi cha timu ya wakubwa pamoja na winga Rehan Kibingu. Makinda hayo yamepandishwa kutoka timu ya vijana iliyokuwa ikinolewa na beki wa kushoto wa zamani wa Yanga, Kenneth Pius Mkapa, lakini kwa sasa benchi hilo linaongozwa na kiungo Salvatory Edward 'Mtaalam'. Hiyo ni baada ya Mkapa kurudi darasani kwenda kuongeza taalum yake ya kufundisha mchezo wa soka.

Banda kwa sasa yupo nyuma ya mastraika wanne, Hamis Kiiza wa Uganda, Mrundi Didier Kavumbagu, Said Bahanuzi na Jerry Tegete. Ni nani huyo Banda?

Familia ya Michezo

Banda anasema kuwa Baba yake mzazi, Joseph Banda alikuwa akicheza soka, lakini alipoumia aliamua kujikitiza kwenye biashara.

"Alikuwa akicheza soka, lakini baada ya kung'oa kucha kwenye kidole gumba cha mguu wake aliamua kuachana na soka."

Anaeleza kuwa hakubahatika kucheza na timu yoyote ya Ligi Kuu isipokuwa alikuwa akikipiga na timu mbalimbali za mtaani. Mwanzo wa soka Banda anasema aliupenda mchezo wa soka tangu akiwa mdogo na kuanza kucheza timu tofauti za mtaani.

"Mwaka 2004 nilishiriki Ligi ya TFF Ngazi ya Taifa iliyokuwa ikishirikisha timu za vijana wenye umri chini ya miaka 14."

"Nilishiriki na timu yangu ya mtaani, River Heroes ya Banana
Ukongo, jijini Dar es Salaam. Baada ya ligi hiyo kumalizika. Nilifanikiwa kuchaguliwa kwenye kikosi bora cha mashindano hayo.

"Tuliahidiwa kupelekwa Ulaya kwenda kujifunza zaidi soka. Lakini, ghafla nilienguliwa kwenye safari hiyo. Sijui hadi leo sababu za msingi ambazo zilinifanya kuondolewa kwenye msafara huo." anasema Banda.

Soka na Shule

Banda aliyecheza kwa mara ya kwanza kikosi cha Yanga dhidi ya Tusker ya Kenya katika mchezo wa kirafiki wa Kimataifa uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Januari, mwaka huu kwa dakika 45 za kwanza ambapo Yanga ililala kwa bao 1-0.

Anaeleza kuwa elimu yake ni ya darasa la saba aliyohitimu katika shule ya msingi Karakata iliopo Kipawa jijini Dar es Salaam.

"Nimehitimu darasa la saba katika shule ya msingi Karakata, Kipawa (Dar es Salaam). Sikutaka kuendelea. Niliamua kuelekeza nguvu zangu kwenye soka. Binafsi niliamini ndiyo njia yangu sahihi kutoka kimaisha."

"Familia ilinitaka kuendelea na shule. Lakini niliwaambia niacheni kama nilivyo, nitajua mwenyewe. Mambo yalikuwa magumu. Lakini nilipata nafasi yakujiunga na timu ya Mogo FC ya Ukonga (Dar es Salaam." anaeleza kinda huyo ambaye amekiri kuwa iwapo atapata mfadhili wa kumlipia ada yupo tayari kuendelea na elimu ya sekondari.

Atua Mtibwa, aula Yanga

Kinda huyo mwenye umbo kubwa na nguvu za kusukuma na mabeki wa timu pinzani anaeleza kuwa timu ya Mtibwa ilimwona na kuvutiwa na kiwango chake.

"Baada ya kuvutiwa na kiwango changu, walinichukua kwenye timu yao ya vijana. Nilidumu nao kwa misimu miwili tu na kurejea tena kwenye timu yangu ya zamani Mogo FC. Maslahi yalikuwa madogo.

"Mwaka 2011, Mlezi wa Mogo FC Ally Ruvu aliamini kiwango changu na kunipeleka Yanga kufanya majaribio na kufaulu siku hiyo hiyo."

Anaeleza kuwa majaribio hayo alifanya na kikosi cha timu ya vijana kilichokuwa kikinolewa na kocha Kenneth Mkapa na Abubakari Salum 'Sure Boy'.

Banda anasema kocha Ernie Brandts alipomwona kwa mara ya kwanza na kikosi cha timu ya vijana katika mashindano ya Kombe la Itihad yalifanyika Mwananyamala Dar es Salaam na kumpandisha timu ya wakubwa siku hiyo hiyo.

"Kocha Brandts aliponiona kwa mara ya kwanza alikoshwa na kiwango changu na kunipandisha timu ya wakubwa pamoja na Kibingu (Rehan).

"Sikuamini ukizingatia bado umri wangu bado mdogo. Vile vile, sina uzoefu. Niliona ni kazi kubwa kwangu kupata namba mbele ya Tegete, Bahanuzi, Kiiza na Kavumbagu ambao wana uzoefu mkubwa na ligi." anaeleza yosso huyo anayevutiwa na staa wa Anzhi Makhachkala na Cameroon, Samuel Eto'o 'Fils'.

Matarajio yake

Banda anaeleza kuwa ndoto zake haziwezi kutimia bila kujituma
kwa bidii na nidhamu kwa wote.

"Naamini kuwa ili kutimiza ndoto zangu nilizojiwekea. Lazima kujituma na nidhamu kwa kila mtu. Kwanza nafikiri ni kupambana kupata namba kikosi cha kwanza cha Yanga. Pia, kucheza timu ya
Taifa Stars na kujitangaza zaidi kimataifa.

"Itakuwa njia rahisi kwangu kuonekana na kujitangaza kucheza soka la kulipwa nje ya nje kama walivyo Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu." anaeleza Banda.

Historia

Banda ni mtoto wa tatu katika familia ya Mzee Joseph Joseph Banda yenye watoto saba, watano wakiwa wakiume na wawili wa kike.
Anaeleza kuwa kaka yake wa kwanza aitwae Gabriel ndiye anayecheza soka, lakini wengine hawataki kabisa kusikia mchezo huo.


GEORGE BANDA

Kuzaliwa; Julai 19, 1993
Mahali; Ilala, Dar es Salaam
Klabu alizocheza;
River Heroes; 2002/04
Mogo FC; 2005/O7
Mtibwa Sugar; 2008/10
Yanga; 2013
Taifa; Tanzania

No comments:

Post a Comment