Search This Blog

Thursday, March 21, 2013

SERIKALI IMERIDHIA MCHAKATO WA UCHAGUZI WA TFF UENDELEE KWA KATIBA IPI ?

 WAKATI Serikali na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakikubaliana mchakato wa uchaguzi wa TFF uendelee kwa sharti la kuhakikisha haki inatendeka kwa wagombea waliokatwa kufanyiwa mapitio ya mchakato wa kuwaondoa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), kuna jambo halipo sawa.

Ikumbukwe kwamba, serikali ilisitisha uchaguzi huo baada ya kupokea malalamiko yaliyohusu utumikaji wa katiba mpya ya TFF ya mwaka 2012 ambayo ilipitishwa isivyo halali bila mkutano mkuu kukaa.

Serikali ilielekeza kutumika kwa katiba ya mwaka 2006 ambayo ilipitishwa na mkutano mkuu wa TFF, au mkutano mkuu ukutane kupitisha katiba ya 2012 ndipo mchakato wa uchaguzi uendelee.

Jana, wakati Rais wa TFF, Leodegar Tenga akitangaza kufikia makubaliano hayo yaliyofikiwa baada ya kikao cha pamoja kati ya TFF, uongozi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo chini ya Waziri Dk. Fenella Mukangara na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), HAKUWEKA wazi kwamba mchakato huu wa uchaguzi unaoendelea unafanyika kwa kutumia katiba ipi.

Tenga alienda mbele kwa kusema baada ya makubaliano hayo, TFF itaiandikia barua Fifa ambayo itasimamisha mchakato wa review ili iweze kutuma ujumbe wake kwa ajili ya kusikiliza malalamiko ya wagombea walioenguliwa.

KUNA NINI KATIKA KATIBA?
Kama serikali awali ilitoa maelekezo ya katiba ya mwaka 2012 kutotumika kwa kuwa ni batili, sasa kwa nini Tenga ameshindwa kuweka wazi kwamba uchaguzi huu unafanyika kwa katiba ipi?

Kama Fifa wanakuja kufanyia kazi malalamiko ya wagombea ambao hadi wanachinjwa katika uchaguzi huu, mchakato wake ulikuwa unafanyika chini ya katiba ya mwaka 2012, ina maana Fifa watafanya kazi kwa kutumia katiba ya mwaka 2012 ambayo serikali imeipinga.

Je, uhalali wa katiba ya mwaka 2012 umetoka wapi? Maana serikali ilipofanya mapitio ya kupitisha hadi kusajiliwa kwa katiba hiyo ya mwaka 2012, iligundua upungufu kiasi cha kumsimamisha kazi mtu aliyeipitisha.

Usafi wa katiba ya mwaka 2012 umetoka wapi? Ni nini kilizungumzwa zaidi katika kikao hicho na kuamua suala la katiba kuachwa hewani wakati serikali ilishatoa msisitizo wa kutoitambua katiba ya mwaka 2012?

MSISITIZO WA UCHAGUZI KABLA YA MEI 25

Tenga amesisitiza huku akiahidi kuwa uchaguzi wa TFF utafanyika kabla ya Mei 25 mwaka huu kama walivyokubaliana na Serikali, na kuwa haki si tu itatendeka bali ionekane imetendeka.

“Serikali imetuelekeza uchaguzi ufanyike kabla ya Mei 25. Tumewaambia kwetu huko ni mbali. Fifa wakija hata kesho wakituambia endeleeni sisi tuko tayari.

Hesabu zetu ziko tayari, makabrasha yote yako tayari yanasubiri mkutano tu. Labda itakuwa kutoa muda tu kwa wajumbe walioko mbali waweze kujiandaa, maana wajumbe huwezi kuwaita ghafla,” amesema.

Hapa inawezekana kweli Tenga ana nia thabiti ya kuhakikisha mkutano unafanyika kabla ya Mei 25, tatizo linakuja uchaguzi utafanyikaje bila ya maswali muhimu kujibiwa hasa kuhusu katiba?

MSIMAMO WA MTANDAO HUU
Tunaamini Tenga na TFF ni watu wanaojua kile wanachofanya katika uongozi wao, sasa ni muhimu kwao kuweka wazi kuhusu katiba itakayotumika katika uchaguzi huu japokuwa hadi kauli ya jana ya TFF ni wazi katiba ya mwaka 2012 ndiyo itakayotumika.

Kama katiba itakayotumika ni ya 2012, tuelezwe sababu za kufanyika hivyo, nayo serikali itueleze imekubali vipi kuendelea na uchaguzi kwa kutumia katiba ambayo awali iliikataa.

Tunaamini uchaguzi wa TFF utafanyika kwa haki na anayestahili ndiye atakayeshinda lakini ni muhimu kwenda huko huku mambo yaliyotatiza hapo awali yakashughulikiwa mapema ili kutoweka mkanganyiko hapo baadaye.

3 comments:

  1. suala la katiba gani itatumika ni suala la kujibiwa na serikali kwani ndiyo iliyofuta katiba ya 2012,siyo Tenga.mAADAM SERIKALI IMERUHUSU MCHAKATO WA UCHAGUZI UENDELEE NI DHAHIRI KATIBA ITAKAYOTUMIKA NI YA MWAKA 2012 PAMOJA NA KANUNI ZA UCHAGUZI ZA 2012ZILIZOANDALIWA CHINI YA KATIBA HIYO,KWA SABABU NDIZO ZILIZOTUMIKA KUANZIA MWANZO WA MCHAKATO WA UCHAGUZI.KUFANYA TOFAUTI NA HIVYO ITABIDI MCHAKATO UANZE UPYAA KABISA NA NAFASI YA MAKAMU WA PILI WA RAIS ITABIDI NAYO IGOMBANIWE.HAPA TUTARAJIE VITUKO ZAIDI.KIMSINGI KATIBA YA MWAKA 2012 NI SAHIHI KWA SABABU WAJUMBE WA MKUTANO MKUU WA TFF WALIRIDHIA IREKEBISHWE KWA WARAKA BADALA YA MKUTANO NKUU BAADA YA KURIDHIKA NA SABABU WALIZOELEZWA NA KAMATI YA UTENDAJI NA KUPUUZA HOJA ZA MALINZI NA KRFA.JUKUMU LA KUPINGA KATIBA ILIYOREKEBISHWA KWA WARAKA LILIKUWA LA WAJUMBE WA MKUTANO MKUU WA TFF,SIYO SERIKALI WALA WAMBURA,DIONIZI MALINZI AU MAULIDI KITENGE.MAADAM WENYE TFF WAMERIDHIA UTARATIBU HUO AKIWEMO MALINZI MWENYEWE AMBAYE ALICHUKUA FOMU KUGOMBEA UONGOZI CHINI YA KATIBA HIYO,NA UTARATIBU WA WARAKA ULITANGAZWA WAZI BILA KIFICHO,KAZI YA SERIKALI NI KUISAJILI TU NA NDICHO ILICHOFANYA.KITENDO CHOCHOTE CHA KUINGILIA UTARATIBU ULIOKUBALIWA NA WENYE TFF NI KUINGILIA UENDESHAJI WA TFF

    ReplyDelete
  2. Kaka hiyo ndio Tanzania tumezoea kuruka mkojo na kukanyaga mavi, serekali na tff mbmuzi yao wote ni batili.

    ReplyDelete
  3. Ndiyo tabia zetu watanzania kuficha maovu na kutetea ujinga

    ReplyDelete