Search This Blog

Tuesday, February 12, 2013

MNYAMA VS LIBOLO: SIMBA WASEMA KAMBI INAENDELEA VIZURI ARUSHA - WAOMBA SAPOTI


HALI ya kambi jijini Arusha inaendelea vizuri. Kikosi hakina majeruhi mpya na wachezaji wote wanaendelea na mazoezi vizuri. Uongozi wa Simba SC unavishukuru sana vyombo vya habari hapa nchini ambavyo vinazidi kuarifu jamii kuhusiana na mechi yetu ya kimataifa dhidi ya Libolo ya Angola itakayochezwa Jumapili ijayo katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Hata hivyo, uongozi wa Simba ungeomba sapoti zaidi katika namna ya kuripoti mechi hizi za kimataifa.

Kwa mfano, leo hii kuna gazeti limeandika kuhusu umafia (unyama) ambao Libolo wamefanyiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) la kutopewa uwanja wa kufanyia mazoezi.

Pamoja na maelezo mazuri ya Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, kwamba kilichofanyika kipo ndani ya kanuni za CAF, bado gazeti hilo limeandika kwamba huo ni unyama.

Tunaomba kueleza machache kwa vyombo vyetu vya habari hapa nchini. Mwishoni mwa mwaka jana, wachezaji na baadhi ya  wanaounda jopo la ufundi la Timu ya Taifa la Vijana (Ngorongoro Heroes) walipigwa na askari nchini Kongo kwenye mechi za kuwania kufuzu michuano ya CAF kwa Vijana.

Hakuna gazeti hata moja la Kongo lililoripoti kuhusu vipigo na mateso waliyopata Watanzania nchini humo na timu yao ikashinda. Msimu uliopita, Simba ilinyimwa kufanya mazoezi kwa siku tatu katika mji wa Shandi nchini Sudan kwa sababu zisizo na kichwa wala miguu. Hakuna chombo chochote cha Sudan kilichoripoti kuhusu tukio hilo ingawa hiyo ilikuwa ni miongoni mwa sababu zilizosababisha Simba itolewe kwenye michuano hiyo.

Msimu huo huo uliopita, wachezaji wa Simba waliachwa wakipigwa na baridi ya nyuzi joto 4C nje ya uwanja wa mazoezi kwa zaidi ya saa nzima mjini Setif, Algeria kwenye mechi ya CAF Orange Cup... Hakuna chombo chochote cha habari cha Algeria kilichoripoti kuhusu hili.

Hivyo ndivyo vilikuwa vitendo vya kinyama. Lakini Simba SC inaamini TFF ilifanya ilichofanya kwa mujibu wa kanuni.

Ujumbe ambao Simba SC inataka kuufikisha kwa wadau wetu wa vyombo vya habari ni kufahamu kwamba vyombo vyetu haviko kwa ajili ya kutetea wageni. Vyombo hivi vinatakiwa kusaidia vilabu vya Tanzania viliwakilishe taifa vizuri katika mashindano.

Si nia ya Simba SC kutaka vyombo vya habari vya Tanzania vitetea unyama, la hasha. Hata hivyo, nia ya Simba ni kuona vyombo vya habari vinakua chachu ya kusaidia timu zetu zifanye vizuri na si kusaidia timu za kigeni kwa vile timu zetu zikienda ugenini huwa hazisaidiwi na yeyote.

Ombi letu kubwa kwenu ni kwamba uzalendo utangulie kwenye kuripoti matukio makubwa ya kimichezo hapa kwetu.

5 comments:

  1. simba hii ndo nafasi yenu ya kurudisha imani kwa mashabiki waliopoteza imani nanyi,

    ReplyDelete
  2. kweli kabisa wandishi muangalie vya kuandika wakati mwengine

    ReplyDelete
  3. Tatizo Waandishi wa bongo hawana maadili ya kazi zao wanajua kaz ni kuandika kila ki2 that's y i hate waandishi wa habari.

    ReplyDelete
  4. Waandishi wengi wa bongo ni vilaza na hawajui vyuoni walisomea nini. Kwa jinsi mnavyo ripoti taarifa mbalimbali zinaegemea sana upenzi wa timu fulani si weledi wa kazi yao. Mimi binafsi ni mdau sana wa MAGIC RADIO hasa kipindi chao cha michezo lakini waandishi wa michezo hawana weledi hata kidogo juu ya kazi yao ya Uandishi. Mathalani matukio yoyote mazuri yanayoihusu Simba SC hawatangazi kwa msisitizo kama wanavyotangaza mabaya hata kama tukio lenyewe si kubwa kwa namna ambavyo wanalizungumzia. Huko ni kuonesha ukilaza walionao. Waandishi tunawaomba mbadilike kwani ninyi ni kioo cha michezo nchini kwa watu kutegemea kupata taarifa kupitia kwenu. Naomba kuwasilisha.
    BY MKINGA C.J wa KIMARA DSM

    ReplyDelete
  5. Waandishi wengi wa bongo ni vilaza na hawajui vyuoni walisomea nini. Kwa jinsi mnavyo ripoti taarifa mbalimbali zinaegemea sana upenzi wa timu fulani si weledi wa kazi yao. Mimi binafsi ni mdau sana wa MAGIC RADIO hasa kipindi chao cha michezo lakini waandishi wa michezo hawana weledi hata kidogo juu ya kazi yao ya Uandishi. Mathalani matukio yoyote mazuri yanayoihusu Simba SC hawatangazi kwa msisitizo kama wanavyotangaza mabaya hata kama tukio lenyewe si kubwa kwa namna ambavyo wanalizungumzia. Huko ni kuonesha ukilaza walionao. Waandishi tunawaomba mbadilike kwani ninyi ni kioo cha michezo nchini kwa watu kutegemea kupata taarifa kupitia kwenu. Naomba kuwasilisha.
    BY MKINGA C.J wa KIMARA DSM

    ReplyDelete