Search This Blog

Tuesday, February 19, 2013

LIBOLO YATUMIA ZAIDI YA TSH. MILIONI 180 KUIFUNGA SIMBA KWENYE MCHEZO MMOJA TU.

KLABU ya soka ya CRD Libolo ya Angola imetumia zaidi ya Sh. 180 milioni katika maandalizi yake ya mechi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi Simba na kuweza kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Katika kiasi hicho cha fedha za maandalizi, Libolo ikiwa chini ya afisa mipango wake, Edson Naval iliweza kujilipia yenyewe kila kitu ilipokuwa nchini.


Mtandao wa shaffihdauda.com ulizungumza na Kasim Malinda aliyekuwa sambamba na maafisa wa Libolo waliotangulia nchini mwezi mmoja kabla ya kuivaa Simba, ambaye anasema timu hiyo ilikuwa imejiandaa ipasavyo kuhakikisha inashinda.
Katika mchezo wake wa Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Libolo ilishinda bao 1-0 lililofungwa na Joao Martins kwa kichwa dakika ya 24 akiunganisha krosi ya Carlos Almeida kutoka wingi ya kulia.
“Jamaa walikuwa wamejipanga katika vitu vingi. Walikuwa wakilipa wenyewe vitu vingi kuanzia uwanja hadi mabwawa ya kuogelea. Hawakuwa na mambo ya kulalamika kuonewa wala nini, kila kitu chao kilikuwa kimepangwa na watu waliotangulia kuja,” anasema Malinda ambaye alikaa na maafisa hao wa Libolo kwa muda wa zaidi ya siku 27. 
Katika mchanganuo wa matumizi ya Sh. 180 milioni, Malinda alisema, watu wasiopungua 40 walikuwepo katika msafara wa Libolo na walikaa katika hoteli ya Double Tree kwa siku 10 huku gharama ya chumba kwa siku moja ikiwa si chini ya dola 200, hivyo malazi tu walitumia Sh. 120 milioni.
Kwa chakula, watu 40 walitumia gharama ya dola 80 kwa siku 10 ambapo jumla yake ni Sh. 48 milioni. Usafiri, walikodi basi kubwa aina ya YUTON kwa gharama ya dola 350 kwa siku, hivyo kwa siku 10 walitumia Sh. 5,250,000.
Libolo ilikuwa ikifanyia mazoezi yake kwenye viwanja vya Gymkhana ambapo kwa siku walikuwa wakilipa Sh. 500,000 ambapo kwa siku 10 walitumia Sh. 5,000,000.
Ukijumlisha gharama za malazi, chakula, usafiri na uwanja, jumla Libolo ilikuwa imetumia kiasi cha Sh. 178 milioni. Fedha hizo ni nje ya matumizi mengine ambayo hayakuweza kuhainishwa mara moja kama ukodishaji wa mabwawa ya kuogelea baada ya kushindwa kulitumia lile la hoteli waliyofikia lililokuwa katika matengenezo.
Katika hayo matumizi mengine ndipo unapopata zaidi ya Sh. 2 milioni ambazo zinafikisha gharama za Sh. 180 milioni na zaidi.
“Libolo walikuwa wakikodi hadi mapipa maalum ambayo mchezaji alikuwa akiingia ndani yake yakiwa na maji baridi kila baada ya mazoezi,” anasema Malinda.


WALIIPIGA PICHA SIMBA WAKIHOFU USALAMA;
Malinda anakiri kufanya kazi na Libolo katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kurekodi mechi za Simba dhidi ya African Lyon na nyingine dhidi ya JKT Ruvu. Baadhi ya magazeti yaliwaona, lakini walipoulizwa walidai wao ni watalii.
“Wale jamaa ni waoga mno na kila kitu wanakifanya kwa tahadhari kubwa. Walikuwa wakiogopa usalama wao kwani waliwahi kuvunjiwa kamera zao Afrika Kusini na Nigeria walipokwenda kurekodi mechi za wapinzani wao, ndiyo maana walijibu wao ni watalii,” anasema Malinda.


UGUMU WA MECHI YA MARUDIANO;
Baada ya wiki mbili zijazo Simba inatarajiwa kwenda Angola kurudiana na Libolo lakini Malinda anaipa tahadhari klabu hiyo kwani inaweza kukumbana na soka tofauti kutoka kwa wapinzani wao.
Malinda anasema, kwa alivyoiona Libolo katika mazoezi na kwenye mechi ni vitu viwili tofauti. “Walikuwa wakicheza mazoezi aina nyingine ya soka na kwenye mechi wamecheza tofauti, labda zile dakika tano za mwisho ndiyo wamecheza soka lao la kasi na pasi nyingi,” alisema Malinda.


SIMBA HAIKUWA MAKINI
Malinda anasema kwa muda wote ambao Libolo ilikuwa ikifanya mazoezi kwenye viwanja vya Gymkhana, viongozi wa Simba hawakuweza kutuma mtu kwenda kuwatazama Libolo.
“Kwa muda wote tuliokuwa Gymkhana sikuwahi kuona watu wa Simba wanakuja labda kuiba mbinu za Libolo na jamaa walicheza mazoezi bila kificho na hata wao walishangaa hali hiyo, yaani hawajafuatiliwa kabisa,” anasema Malinda.

4 comments:

  1. Malinda na woote mnaofuatilia hili, kwanza asante kwa kuweka wazi hili. lakini hivi ulitegemea uongozi wa Simba uwe makini katika nini? Uongozi wa Simba upo katika mgando kwamba wanachama wa Simba ni wa kudangaya tu na siku zinakwenda. Lakini Simba imepoteza muelekeo na kila siku uwezo wa timu unapungua. Viongozi, Simba inahitaji watu wote wanaoipenda Simba wafanye kazi pamoja. Uongozi wa kizamani wa makundi unatuumiza..

    ReplyDelete
  2. Yakheee Simba amefungwa na LIBOLO MOJA TU.

    ReplyDelete
  3. simba kwa Sasa haipo vizuri kabisa,viongozi wanawaza siasa tu wanasahau majukumu yao ya kimpira.Nadhan inabd wanachama wenzangu tutenganishe siasa na mpira kwa kuamua kuwa kiongozi wa juu wa mpira hatakiwi kuwa mwana siasa nadhan kwa style hiyo labda tunaweza sogea mbele kisoka katika klabu zetu.RAGE TUNAOMBA UJIUZULU UBUNGE ULIOKUWA UNAUTAKA KUPITIA MPIRA UMESHAUPATA TUNAOMBA TIMU YETU ILI TUIONGOZE.

    ReplyDelete
  4. simba siyo ile ambayo ilikwa inaogopesha,hata yanga wakajitahidi kufuatilia na kusajili wachezaji wazuri msimu huu tofauti na simba ambayo inauza wachezaji wazuri sana halafu inalipa madeni ya usajili wa wachezaji bomu bila kufanya kitu cho chote cha kuinua timu.nadhani mwaka huu zile goli tano mlizompa Yanga atazirudisha na nyongeza juu.Rage pumzika ubaki na uheshimiwa.

    ReplyDelete