Search This Blog

Monday, February 11, 2013

KOCHA WA STARS AWAAMBIA AGGREY MORRIS NA NYONI WATAFUTE TIMU


KOCHA wa Taifa Stars, Kim Poulsen amewataka mabeki wa Taifa Stars Aggrey Morris na Erasto Nyoni kusaka timu kwa ajili ya kufanya mazoezi kujiweka fiti.

Mabeki hao kwa sasa wamesimamishwa na uongozi wa Azam FC kwa tuhuma za kuchukua rushwa kwenye mechi ya ligi dhidi ya Simba mwaka jana. Azam ililala mabao 3-1. 


Kim alisema jijini Dar es Salaam kuwa ni wachezaji muhimu kwenye kikosi chake hivyo hapendi kuwapoteza.

"Nafikiri walicheza vizuri dhidi ya Cameroon, licha ya kuwa nje ya uwanja. Mchango wao na timu ni mkubwa. Nafikiri wanatakiwa kusaka timu kufanya nayo mazoezi kila siku kijiweka fiti zaidi."

Alisema alikuwa akiwafuatilia kila mara na kuvutiwa na uchezaji wao, lakini kuna jambo ambalo aliligundua. 

"Morris (Aggrey) alicheza vizuri na Yondan (Kelvin) nafasi ya ulinzi. Lakini kuna wakati alionekana kukosa ufiti."

Alieleza kuwa hali hiyo ilimfanya beki huyo wa kati kumvamia mshambuliaji, Fabrice Olinga wa Cameroon na kuzaa faulo ambazo anaamini zingeweza kuigharimu timu kama wapinzani wangezitumia vizuri.

"Nafikiri ni wachezaji muhimu kwenye kikosi changu. Sitaki kuwakosa ukizingatia tuna mchezo mbele yetu dhidi ya Morocco." alisisitiza kocha huyo.

Stars itacheza na Morocco mwezi ujao kusaka tiketi yakushiriki fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2015.

1 comment:

  1. Ushauri mzuri wachezaji husika wazingatie kwani kikosi kwa sasa kinatia matumaini! NURU SPORTS MSM

    ReplyDelete