Search This Blog

Sunday, December 2, 2012

SERENGETI YATOLEWA NA CONGO AFRIKA: JAMHURI KIHWELO NA MKALIMANI WAPIGWA NA POLISI

Kocha wa timu ya taifa ya vijana, Jacob Michelsen amesema kuwa anajivunia vijana wake licha ya kuondolewa na Congo kwenye mashindano ya kuwania nafasi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika na kulaumu uamuzi kuwa ulichangia kwa kiasi kikubwa Serengeti Boys kulala kwa mabao 2-0 mjini Brazaville.
Kwa matokeo hayo, Serengeti Boys imeondolewa kwenye mashindano ya Afrika kwa vijana walio na umri chini ya miaka 17 kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya mechi ya kwanza iliyofanyika jijini Dar es salaam kuisha kwa Tanzania kuibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa. Timu hiyo itarejea nchini siku ya Jumanne saa 1:00 jioni kwa ndege ya Kenya Airways.
“Vijana walicheza vizuri sana na walicheza kwa juhudi wakati wote wa mchezo na safari hii wacheza dhidi ya vijana ambao ni wakubwa zaidi,” alisema kocha huyo kutoka Denmark. “Lakini waliangushwa na uamuzi kwa sababu walipata penati ambayo haikustahili.
“Kwa kweli hata tukio lenyewe lilitokea nje ya penati na beki wetu alilala kuchukua mpira na alifanikiwa kuufikia bila ya kumgusa mshambuliaji wa Congo. Lakini wakati beki wetu akiwa ameshauchukua mpira na yule aliyejiangusha akiwa ameshanyanyuka, mwamuzi alipiga filimbi kuamuru penati.”
Kocha huyo alisema pamoja na bao hilo Serengeti Boys iliendelea kucheza vizuri na nusura mchezo huo uamuliwe kwa penati tano, lakini wenyeji wakapata bao la pili lililoinyima Tanzania nafasi ya kufuzu kwa mara ya kwanza kucheza fainali hizo.
“Lilikuwa ni bao lilitokana na shambulizi la kushtukiza na walikimbia vizuri na mpira na baadaye kupiga krosi iliyounganishwa kwa kichwa,” alisema Michelsen.
“Najivunia vijana wangu kwa sababu walicheza kwa kujituma na kujiamini; walifanya juhudi kubwa, lakini uamuzi ulituangusha. Nina imani na timu hii na natumaini kama vijana watano walitoka kwenye timu ya U-20 na kuingia timu ya taifa, basi kuna vijana wengine wanaoweza kutoka kwenye timu hii na kuingia timu ya taifa. Ni vizuri tukaendelea na programu za vijana tuweze kujenga timu nzuri baadaye.”
Afisa wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Salum Madadi ambaye aliambatana na timu hiyo Congo, alisema mechi hiyo ilizingirwa na mizengwe kabla na baada ya mechi na kwamba wamesharipoti matukio yote kwa kamisaa wa mechi hiyo baada ya kocha msaidizi, Jamhuri Kihwelo, mtunza vifaa Juma Kizwezwe na mkalimani wa timu kushambuliwa na polisi na mashabiki kabla ya mechi hiyo.
“Hatukupewa gari la polisi wakati wa kwenda uwanjani na hivyo hatukujua tuingilie wapi. Tulipofika uwanjani, walituelekeza mlango ambao tuliona wanaumwagia maji ambayo Julio aliona yangeathiri wachezaji na kuwaagiza wasitumie mlango huo na ndipo polisi walipomvamia,” alisema Madadi.
“Kizwezwe alishambuliwa na mashabiki baada ya kamisaa kumuagiza arejee hotelini kufuata jezi zaidi kutokana na Congo kuwasilisha pingamizi kabla ya mechi kuwa jezi za Tanzania hazikuwa kwenye mlolongo uliokuwa kwenye orodha iliyowasilishwa.
“Alipotaka kutoka uwanjani, alizuiwa na askari na tukalazimika kumuita kamisaa ambaye aliagiza polisi wamruhusu atoke uwanjani. Alipotoka mashabiki walimzuia asiondoke na mzozo ulipokuwa mkubwa mashabiki walimvamia na ndipo tulipomwita tena kamisaa ambaye aliagiza Kizwezwe asiondoke na badala yake jezi zilizokuwa na matatizo zibandikwe plasta. Hata hivyo, polisi walimzuia Kizwezwe asiende kukaa kwenye benchi hadi mchezo ulipoisha.”
Madadi alisema kuwa kutokana na vurugu hizo, kamisaa huyo kutoka Afrika Kusini aliomba majina ya walioshambuliwa na akaahidi kuyaweka matukio hayo kwenye ripoti yake.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema Shirikisho limeyapokea matokeo hayo kwa masikitiko kutokana na ukweli kwamba TFF ilifanya juhudi kubwa katika kuhakikisha safari hii timu za vijana zinapata maandalizi mazuri na ya muda mrefu, lakini juhudi hizo zimekwamishwa na mazingira mabaya kama yalivyoripotiwa na viongozi wa msafara wetu.
“Katika kutafuta mafanikio hakuna njia ya mkato. Ni lazima tuamini katika program tunazozitekeleza na kuboresha pale tunapoona pana udhaifu. Tunaamini kuwa itafika wakati juhudi hizi zitazaa matunda na Watanzania watanufaika na mipango hii ya muda mrefu,” alisema katibu huyo.

1 comment:

  1. Sisi wakazi wa Congo tulioshuhudia mchezo tumeona jinsi hawa wenyeji walivyoonesha ushirikiano kwa timu yao. Inabidi sisi Watanzania tuipende nchi yetu na pia tuzipende timu zetu zote klabu au timu za Taifa. Yaliyotokea Congo Brazzaville ni hujuma kwetu sisi wageni lakini kwao wenzetu walifanya hivyo kwa uzalendo wa kuipenda nchi yao, hawakuihujumu timu yao hata kidogo. Yaani kuanzia washabiki, askari na viongozi wa mpira wa Congo wao lao likuwa moja kuhakikisha kwamba Serengeti Boys inaondoka bila ushindi. Kwa watazamaji walianza kuizomea timu yetu hata kabla haijacheza. Askari walipokuwa wanawazuia akina Julio kuingia malangoni askari wote walikuwa kitu kimoja wanateteana na washangiliaji walikuwa wanawashangilia askari kwa kitendo walichokuwa wanawafanya na kuwazomea viongozi wa Serengeti Boys, sasa cha ajabu wakati wa sakata hili viongozi wa mpira wa Congo wote walijificha kitendo kilichoonesha kuwa wanunga mkono vurugu za kuivuruga Seerengeti Boys kisaikolojia. Ile penati ilopigwa kwa Serengeti Boys haikuwa penati, refa alisita kupiga filimbi kwa sekunde kadhaa akiwa na kigugumizi kwa sababu hakukuwa na kosa, kilichomfanya refa kuamua penati ni baada ya washangiliaji wa Congo woote kushanglia na kupiga kelele penatii,penatii,penatii ndipo refa kwa kelele za washangiliaji akavutiwa na kuamua penati wakati alipomtazama mshika kibendera yeye bendera yake ilikuwa chini hakuonesha kwamba kuna kosa limetendeka. Ninachotaka kusema hapa ni kwamba Watanzania tuzipende timu zetu, tusifanye fujo kama wenzetu bali kuanzia washangiliaji, waandishi wa habari na wadau wote tuhakikishe kuwa tunaziunga mkono timu zetu zinapocheza viwanja vya nyumbani, ni utovu wa uzalendo kuishangilia timu ya wageni na kuizomea timu ya nyumbani, wenzetu hawafanyi hivyo. Waandishi wa habari wetu wasiwe wa kwanza kuzivunja moyo timu zetu kwa kuandika eti ushindi kiduchu, ushindi mwembamba, katika mchezo hakuna ushindi mwembamba, ushindi wa goli 1-0 ni ushindi mkubwa sana, hata sare ni hatua muhimu katika mchezo haifai kubezwa. Wenzetu japokuwa tuliwafunga goli 1 vyombo vya habari vyao vyote vilikuwa vinawapa moyo kuwa wataitoa Serengeti Boys katika uwanja wao wa nyumbani. TFF nao lazima wafuatilie inakuwaje wanaopanga fixture mara nyingi huzipangia timu zetu michezo ya kuanza nyumbani na kumalizia ugenini? Je fixture hupangwa kwa kurusha shilingi au huamuliwa tu na kamati? Kama huamuliwa na kamati, mbona bahati ya kumalizia michezo nyumbani huwa sisi tunaikosa, kama ni kwa kurusha shilingi kweli shilingi kila siku haitupi sisi fursa ya ndiyo?. Mara nyingi ni nchi fulani fulani huwa zinapata upendeleao huu, kunani huko CAF?

    Mdau Manyundo.

    ReplyDelete