Search This Blog

Saturday, December 29, 2012

KABANGE TWITE AZUIWA KUCHEZA YANGA NA TFF


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limemzuia kiraka Kabange Twite kuchezea Yanga hadi pale suala lake litakapoamuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Saad Kawemba,aliiambia Mwanaspoti jana Ijumaa kuwa Kabange hatacheza kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kwani suala lake liko mikononi mwa Fifa baada ya Yanga kushindwa kupata idhini ya FC Lupopo ya kumsajili mchezaji huyo aliyesaini mkataba wa miaka miwili Jangwani.

Kamati ya Haki za Wachezaji ya Fifa ndio itatakiwa kumuidhinisha kwani muda wa mwisho wa kuwasajili wachezaji wa kigeni ulikuwa Desemba 15 ilivyokuwa imepangwa na TFF.

Licha ya kwamba atakuwapo kwenye msafara wa Yanga utakaoondoka kesho Jumapili alfajiri kwenda kambini Uturuki, Tekinolojia ya Uhamisho wa Wachezaji kwa Kompyuta (TMS) ndio imetibua mipango ya Kabange kujiunga na pacha wake Mbuyu Twite, ambaye alijiunga na Yanga mwezi Agosti mwaka huu.

Kawemba alisema kuwa viongozi wa Yanga walifanya mawasiliano na watu wa Lupopo kwa TMS, lakini hawakupata majibu yoyote.
 Yanga waliwasiliana na Lupopo masaa mawili kabla ya dirisha dogo la usajili wa wachezaji wa kigeni kufungwa Desemba 15,  alisema Kawemba.
 Hata hivyo walikwama kwani hawakupata majibu yoyote kutoka kwa watu wa Lupopo. 

Fifa ilianzisha utaratibu wa uhamisho wa wachezaji kwa njia ya TMS, ambayo husaidia klabu kuwasiliana moja kwa moja
na pia vyama vya soka vya nchi husika vikifuatilia mawasiliano hayo kwa ukaribu.

Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ndio ilikuwa inammiliki mchezaji huyo kama ilivyokuwa kwa pacha wake, Mbuyu.

Kawemba alisema kufuatia hali hiyo, Yanga wanapaswa kusubiri mawasiliano kutoka kwenye klabu hiyo kwenye TMS.
Alisema, hata hivyo, pale watakapopata majibu ya Lupopo ndio taratibu zitaanza kushughulikiwa na TFF lakini wenye maamuzi ya mwisho watakuwa Fifa.

 Yanga wakipata mawasiliano na Lupopo watapaswa kurudi kwetu ili tupeleke suala lao Fifa, alisema.

 Itabidi tuwaeleza sababu za kuridhisha Fifa kuwa kwanini Yanga waliingia TMS muda mfupi kabla ya muda wa mwisho wa usajili, pia (Fifa) watapenda kujua sababu za Lupopo kuchelewa kujibu. 

Kawemba alidokeza ikiwa Kamati ya Haki za Wachezaji itaridhika na maelezo ya pande hizo mbili basi watatoa kibali lakini wasiporidhika basi watamzuia Kabange kuchezea Yanga.

Aliongeza kuwa Kamati ya Haki na Uhamisho Wachezaji ndio yenye uamuzi wa mwisho na kuongeza ikiwa Yanga watanyimwa kibali basi hawatakuwa na ubavu wa kukata rufaa kokote.

 Hakuna chombo chenye mamlaka juu ya Kamati ya
Haki na Usajili ya Fifa. Kwa hiyo Yanga wanapaswa kuelewa hilo, aliongeza. 

Ninawashauri Yanga wafanye kila njia wawapate Lupopo kwani kadiri watakavyochelewa ndio watakuwa wanajiweka pabaya zaidi.

Hatua hiyo itakuwa pigo kwa Yanga kwani ilikuwa inamtegemea Kabange angeimarisha kikosi chao kutokana na umahiri wake wa kucheza nafasi nyingi.

Kama ilivyokuwa Mbuyu, kiraka huyo alikuwa ametolewa kwa mkopo kwenye timu ya APR ya Rwanda na Lupopo.

Lupopo ndio ilikuwa inatakiwa kuidhinisha uhamisho wa nyota huyo kwa njia ya TMS lakini bahati mbaya utaratibu huo umekuwa ukitumika kwa nadra nchini Congo kwa kuwa timu zao nyingi ni za ridhaa.

Kama ikishindikana, Yanga itakuwa ina wachezaji wanne tu wa kigeni baada ya kumwachia kipa Yaw Berko, ambaye amejiunga na Lupopo.

Mwenyekiti wa Kamati ya mashindano na usajili wa Yanga Abdallah Binkleb aliiambia Mwanaspoti jana akisema: Sisi tulikamilisha kila kitu, tatizo liko kwao Lupopo na tumeshawaeleza TFF tunasubiri jibu nadhani kesho (leo Jumamosi) tutapata ufafanuzi zaidi.

SAMSON MFALILA - MWANASPOTI

No comments:

Post a Comment