Search This Blog

Wednesday, October 10, 2012

STARS INGEKUWAJE ENDAPO VIJANA HAWA WA MAXIMO WANGEKUWEPO HADI SASA?


 Wakati aliyekuwa kocha wa timu ya soka ya Taifa ya Tanzania kwa kipindi cha miaka mine (2006 - 2010), Marcio Maximo alipokuja nchini aliingia na mtazamo tofauti kuhusiana na soka la Tanzania, Maximo aliamini kuwa nchi yoyote amnbayo inahitaji mafanikio ya kweli ya soka ni lazima ijizatiti zaidi katika soka la vijana.

 Hata nchini kwao, Brazil soka la vijana ndiyo msingi wao mkubwa wa mafanikio waliyonao, lakini alitambua kwa nchi changa kama Tanzania si rahisi kuingia haraka katika soka la vijana na kupata mafanikio. Aliamini uchumi na aina yetu ya utekelezaji mambo huwa ni ya taratibu sana, lakini hiyo haikuwa sababu ya yeye kushindwa kuingiza vijana wadogo kutoka katika baadhi ya shule za secondary nchini katika timu ya Taifa kwa nia ya kujifunza kwa manufaa ya siku za usoni ya kikosi hicho.

Wakati wachezaji waliokuwa wakitegemewa na Watanzania kuingia katika matatizo ya kinidhamu, Maximo aliona ni vyema kutembea kila nchi na vijana wadogo kama Jerry Tegete, Kiggy Makassy, Himid Mao Makami, Tumba Sued na wengineo na si wachezaji nyota kama kina Juma Kaseja, Haruna Moshi, Mussa Mgosi, Athuman Idd “Chuji”, Amir Maftah na wengineo ambao kwa mujibu wake walikuwa wavurugaji wakubwa wa program zake za ufundi katika timu hiyo.

Ni miaka takribani sita sasa na ni Himid Mao na Salum Abubakary "Sure Boy" ambao bado wanacheza soka la kiwango cha juu, kuanzia kwa wachezaji vijana walioaminiwa na kupewa thamani kubwa na kocha huyo kama Abdulhalim Humud, Jabir Aziz, Ramadhani Chombo, Salum Telela walioingia katika matatizo ya mara kwa mara ya kinidhamu katika klabu zao, Taifa Stars imeshindwa kusonga zaidi japo vijana hao tayari wameshacheza zaidi ya misimu mitano katika ligi kuu ya Tanzania. Wengi wameshuka viwango na wengine hawapo kabisa katika soka la ushindani.

Wakati Tanzania ikipiga hesabu za kufuzu kwa michuano mikubwa kuanzia mwaka 2006 wengi walitarajia jambo hilo kutokea walau kwa miujiza kutokana na aina ya wachezaji vijana ambao walionesha mwanga wakiwa tayari na uzoefu wa mashindano makubwa ya kiafrika.


JERRY TEGETE; Yeye amekwama kabisa ndani ya timu yake ya Yanga. Kosa kubwa kwake ni pale alipoamua kurudi Tanzania kucheza mechi ‘isiyo na maana’ ya Simba na Yanga, April mwaka 2010, japo alifunga mabapo mawili katika mchezo huo, Jerry aliishia hapo na wala mabao yake hayakuisaidia timu yake kwani walilala 4-3. Amekuwa na miaka miwili migumu katika maisha yake ya soka na kuna wakati alifikiria kuachana na soka, aliingia timu ya Taifa akitokea shule ya Makongo Sekondary mwaka 2006 na mwaka mmoja baadaye akasajiliwa na Yanga ambako yupo hadi sasa. Aliweza kujitambulisha kama mfungaji mahiri zaidi katika soka la Tanzania, kwa kutumia kichwa, kuvizia na daima ni mchezaji ambaye hujipanga vizuri katika nafasi yake, mfungaji wa wafungaji anaendea mwishoni akiwa bado kijana mdogo huku akipigwa benchi mara kadhaa ndani ya Yanga baada ya kukimbia na ofa ya kucheza soka la kulipwa barani ulaya Sweden.
KIGGY MAKASSY KIGGY; Sulley Ally Muntari wa Bongo, alifunga bao kali pale, Cairo miaka mitatu iliyopita huku golini akiwepo kipa bora barani Afrika, Essam El Haidary, Kiggy alifunga bao la umbali wa zaidi ya mita 25 tena akiwa chini ya miaka 22, lilikuwa bao ambalo pengine bado halijafungwa tena katika uwanja wa kimataifa wa Cairo na liliwaaacha watangazaji wa mechi hiyo wakisema ni bao bora kati ya mabao sita ambayo yalifungwa katika mchezo baina ya Misri na Tanzania siku hiyo. Stars ilifungwa mabao 5-1 lakini kuna kitu ambacho kilionesha tulichonacho, vipaji. Mara kadhaa alifunga hivyo katika ardhi ya Tanzania, lakini baada ya misimu miwili ya taabu ndani ya Yanga amekimbilia Simba msimu huu lakini hana makali aliyokuwa nayo kipindi kile.
JUMA JABU; Alipoitwa kwa mara ya kwanza katika timu ya Taifa alikuwa mchezaji wa Ashanti United, alisajiliwa na Simba mwaka 2008 na kudumu hapo kwa miaka minne. Kwa mujibu wa pasipoti yake yupo chini ya miaka 26 lakini Jabu hakuwa na makali kwa kipindi cha miaka miwili ya mwisho akiwa Simba, mara kadhaa alijaribu kuibuka lakini majeraha yakawa yanamrudisha chini. Nahodha wa timu ya Taifa ya vijana ambayo ilifuzu na kuondolewa katika michuano ya Afrika mwaka 2005 kwa kudanganya umri kwa kiungo Nurdin Bakary, amekimbilia timu ya Coastal Union ya Tanga na anafanya vizuri kiasi tofati na alipokuwa Simba, akicheza namba sita Jabu alijitambulisha kama mpigaji mzuri wa mipira ya ‘free kick’ na mipira ya penati na kona. Alikutana na kipindi kigumu cha maumivu akiwa Simba na inawezekana ikiwa sababu kubwa ya yeye kuanguka kisoka akiwa bado kijana.

TUMBA SUED; Kuna wakati, Azam FC ilikuwa na wachezaji watu ndugu katika kikosi chao cha kwanza, Tumba Sued alikuwa ni beki mzuri wa kati ambaye alikuwa anaitwa mara kwa mara katika timu ya Taifa kwa nia ya kuendelezwa alikuwa akitokea timu ya vijana ya Azam na haraka akawa ‘patna’ mzuri na kaka yake Salum Sued katika ngome ya kati ya Azam, wakati Said Sued akifanya vizuri katika nafasi ya kiungo, Tumba akatokea kuwa beki bora kijana nchini mbele ya majeruhi Dickson Daudi, haraka alipopata mafanikio katika msimu wake wa kwanza akiicheza timu kubwa ya Azam, Tumba akiingia katika maisha ya ndoa na mara kadhaa akaingia katika matatizo ya kinidhamu na klabu yake na hata alipoenda timu ya Moro United hakuwa yule ambaye alitajwa mara kwa mara na kocha, Maximo katika kikosi chake kwa nia ya kuja kuisadia timu hiyo katika siku za usoni, amepotea na wala hasikiki tena.

DICKSON DAUD; Rafu mbaya ambayo alichezewa na mmoja wa wachezaji wa timu ya JKT Ruvu katika mchezo wa ligi kuu ndogo kituo cha Dodoma mwaka 2007, inawezekana kabisa ndiyo iliyommaliza, wakati Maximo akitamba na ukuta wa nidhamu wa Victor Costa, Salum Sued, Hamis Yusuph na Nadir Haroub hakuwa na mashaka na warithi wa nafasi zao hata kama kungetokea majeraha yoyote, Dickson Daud alikuwa beki bora zaidi wa kati U23 katika miaka ya mwanzo ya kocha maximo alikuwa mlinzi shupavu na aliyekuwa na uwezo mkubwa wa kuruka juu na kufunga mabao ya vichwa, anahitaji kujiamini tena kama anataka kuwa mchezaji mzuri tena, ameanza vizuri msimu huu na tayari ameonesha mwanga mkubwa kuwa ataibuka tena, alifunga bao zuri katika mechi ambayo timu yake ya Mtibwa iliifunga Yanga mabao 3-0.

SALUM KANONI; Huyu alichukuliwa kama mbadala wa muda mrefu wa beki namba mbili wa Stars, Shadrack Nsajigwa, lakini mara baada ya kujiunga na Simba mwaka 2005 akitokea Bandari ya Mtwara, Kanoni akawa namba mbili mbadala wa walinzi Said Sued na Nurdin Bakary walipokuwa na majeraha, lakini hata pale nyota hao walipokuwa wazima ilibidi wapambane kugombea nafasi ya kucheza mbele ya kinda huyu, taratibu akachukua nafasi ya kudumu ndani ya Simba na kuitwa Stars na kucheza baadhi ya michezo chini ya makocha, Maximo na hata wakati wa Jan Poulsen, Tatizo lake kubwa ni kuridhika na kujiona tayari amefika safari yake ya soka ndani ya Simba, na baada ya miaka saba, akiwa ndani ya klabu hiy, Kanoni ameondolewa na sasa yupo Kagera Sugar akijaribu kupigania kurudisha makali yake, ameshafunga mabao mawili katika ligi kuu hadi sasa, so far anaendelea vizuri.

ABDULHALIM HUMUD; Gaucho wa Tanzania, alikuwa ni kiungo ‘maestro’ ambaye aliweza vyema jukumu la kushambulia na kuzuia ‘box to box’ aliyekuwa na uwezo na mapafu yasiyochoka, tabia mbaya na kujiona ni mkali zaidi ya hata, Mohammed Aboutrika, Ricardo Kaka’, Alex Song na hata Yaya Toure vimemmaliza alitua Simba na kushindwa kuchomoza mbele ya wachapa kazi kama Jery Santo na Hillary Echessa na kukimbia benchi, akaenda Azam lakini tayari ameonekana kuzidiwa nguvu na Ibrahimu mwaipopo katika kiungo wa ulinzi ndani ya Azam na wakati vijana Himid Mao na Salum Abubakary wakihitaji mafanikio ya mchezo wao Humud anapigana kurudisha makali yake chini ya kocha Boris Bunjuk ambaye ameonekana kumuamini kiungo huyu.

2 comments:

  1. Kama unakumbuka vizuri radio clouds (sports xtra)wakiongozwa na wewe mlikuwa mnamponda sana uwezo wa maximo na kitendo chake cha kuwatema wachezaji wenu mnaowapenda hata kama hawana nidhamu,kaseja,chuji,maftah na boban.leo mnatuwekea makara ndefu kuonesha maximo alikuwa sahihi.Upuuzi mtupu

    ReplyDelete
  2. Hakuna kitu, haya wachezaji wote juu hawana kiwango ...timu ya sasa imejaa vijana akina Ulimwengu, Samatta, Kapombe, Domayo, Mkude, Sure boy n.k. Msitake kuturudisha kwa Maximo. Asante.

    ReplyDelete