Gervas Kago |
MAMIA ya mashabiki wa soka walijitokeza kwenye mitaa mbalimbali Dar es Salaam jana wakati wachezaji wa Simba wakipita na Kombe lao la Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Msafara wa wachezaji wa Simba pamoja na baadhi ya viongozi wao wa benchi la ufundi ulianzia mchana makao makuu ya klabu hiyo mtaa wa Msimbazi na kupita mitaa mbalimbali ya Dar es Salaam na kisha kuelekea ukumbi wa Dar Live, Mbagala ambako umati mkubwa ulijitokeza.
Simba jana iliandaa sherehe ya kujipongeza kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa mwaka 2011/2012.
Hata hivyo baadhi ya wachezaji nyota wa Simba hawakuwepo katika msafara huo kutokana na wengine kuwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzanai ‘Taifa Stars’ kinachojiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Ivory Coast Jumamosi.
Wakati huohuo, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alisema klabu yake haina mpango na wachezaji Ferick Walulya wa Uganda na Gervais Kago wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Alisema wachezaji hao mikataba yao imeisha, hivyo Simba haitahitaji kuwaongezea na kwamba watakuwa huru kujiunga na timu nyingine.
Akizungumzia vipaumbele katika usajili wa mwaka huu, alisema ina mkakati wa kuboresha zaidi usajili katika safu ya beki wa kati.
Pia alisema wanahitaji kupata mrithi wa kiungo mahiri wa timu hiyo aliyefariki hivi karibuni kwa ajali ya gari, Patrick Mafisango.
Aliongeza kuwa klabu yake imejipanga kuhakikisha kuwa usajili wa mwaka huu unafanyika kiumakini zaidi huku akisisitiza kuwa nguvu pia itawekwa katika kuwasajili wachezaji wa kikosi cha vijana cha timu hiyo.
tuludishieni patrick ochan km mnahitaji mtu wa kuziba pengo la mafisango its me slasher kwanja from ilala boom fc
ReplyDelete