Search This Blog

Friday, May 11, 2012

Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’-2

Nonda Shabani 'Papii ' watatu waliosimama kutoka kushoto,Bakari Malima wapili waliochuchumaa kutoka kushoto

*Nonda Shaaban alishangaa kuniona nipo pale Kinshasa
*Siku chache akaniachia mamilioni, nikamalizia nyumba yangu
*Wakati naanza kuzoea, nikaambiwa nindoke Congo si salama
Na Saleh Ally
LEO ASUBUHI, Malima alikuwa ameungana na kundi la waandishi wa habari waliokuwa wanamsubiri Nonda atoke kwenye chumba cha hoteli. Hakujua la kufanya kwa kuwa alibakiwa na dola 50 ambayo isingetosha kumpeleka kokote?
WAKATI nikiwa pale na waandishi ninasubiri, mara mdogo wake aliingia kwenye maegesho ya hoteli yaliyokuwa upande wa nyuma, taratibu akashuka kwenye lile gari aina ya Range Rover Vogue.
Baada ya kuniona akanikumbuka, nilimsogelea na kuanza kuzungumza naye na kumueleza niliamua kuwahi kuja pale hotelini. Haraka nilipata wazo, nikatoa zile picha nilizopiga na Nonda wakati tukiwa Dar es Salaam na Afrika Kusini.
Zilimshangaza sana, akaonekana kuamini kuwa kweli mimi na kaka yake ni marafiki. Aliniambia nimuachie aingie nazo akampe Nonda ili amuulize kama angeweza kuniona. Mara moja nikakubali wazo lake na akaondoka nazo kwenda ndani.
Baada ya muda niliona waandishi wakiongezeka upande niliokuwepo, baadhi walianza kuweka vifaa vyao sawa, kwangu ilikuwa ni dalili kwamba Nonda alikuwa anakuja upande wetu.
Nilijaribu kujumuika na waandishi, kila mmoja alitaka kuzungumza naye. Nilijaribu kuinuka juu ili akitokea anione. Kundi la waandishi lilikuwa kubwa sana na baada ya muda mchache nilimuona akija upande wetu akiwa anaongozana na yule mdogo wake.
Nilijitahidi kukaza macho upande wake, lakini niliona asingeweza kuniona. Nilichoamua ni kufanya lolote na liwe, nilipanda juu, sehemu ambayo niliamini ataniona na mara moja nikamuita kwa sauti ya juu. Aligeuka upande wangu na aliponiona akashituka na kusema: “Bakari, vipi! Siku hizi unaishi hapa?”
Sikujali kama waandishi walikuwa wanatusikiliza, nilimueleza nilitoka Lubumbashi kwa ajili ya kumfuata yeye. Aliniambia ingekuwa vizuri tukaongozana pamoja hadi nyumbani kwake. Nikamuacha aendelee na mkutano na waandishi na baada ya hapo, tukaungana na kupanda gari lake.
Baada ya muda mchache tulikuwa nyumbani kwake, hatukukaa muda mrefu sana ingawa aliniuliza maswali kadhaa na alishangazwa na namna nilivyopata shida hadi kufikia kulala nje.
Tulipofika kwake hatukukaa muda mrefu, mara moja alinionyesha sehemu ambayo nilioga na kuvaa nguo nzuri ambazo zilikuwa zake. Baada ya hapo, tukaondoka pamoja kuelekea sehemu maalum kwa ajili ya chakula na baadaye akanipeleka nyumbani kwao.
Baba yake ni raia wa Burundi na mama yake ni Mkongo, nilifika hadi nyumbani kwao ambako alinitambulisha kwa wazazi na ndugu zake na kuwaeleza namna tulivyoishi vizuri kwa kuelewana wakati tukiishi Tanzania na Afrika Kusini.
Akawaambia wazazi wake wanichukulie kama mtoto wao hata kama ikitokea nimeenda pale yeye akiwa hayupo Kongo basi wanipokee vizuri. Wazazi walifurahi sana na baada ya kuzungumza nao kwa kipindi fulani, mimi, Nonda na mdogo wake tukatoka na kuingia mtaani.
Kwa kuwa nilikuwa nikikatiza naye mitaa, baada ya muda mfupi tu nikawa maarufu pale Kinshasa, ilikuwa lahisi sana kujulikana kutokana na umaarufu wake katika eneo hilo.
Siku zake za kurejea Ufaransa ziliwadia, hivyo Nonda akaniambia lazima ataondoka, akanitaka niendelee kubaki pale nyumbani kwake hata kama itakuwa ni mwezi au zaidi ili niendelee na maisha yangu kama nitaona inafaa. Kwangu niliona bora nifanye hivyo.
Kilichotokea kizuri ni kwamba, Nonda alinipa fedha, kwa kweli siwezi kutaja lakini ilinisaidia sana. Ilikuwa ni fedha nyingi ambayo kiasi fulani ilisaidia kuimalizia nyumba yangu ya Kinondoni. Kwa wakati huo sikuwa na sababu ya kuondoka haraka.

Baada ya kupokea fedha, niliamua kubaki, nikamueleza. Siku iliyofuata nilimsindikiza uwanja wa ndege nikiwa na yule mdogo wake na baada ya hapo wote tukarejea nyumbani. Maisha yakaendelea Kinshasa na safari hii nilikuwa mwenyeji kila kona.
Nikiwa nimeanza kuzoea hasa mji wa Kinshasa, kikajitokeza kitu kimoja cha ajabu sana. Watu walikuwa wakiniomba fedha kila waliponiona, maana nilikuwa maarufu kama rafiki wa Nonda. Unajua kabla hajaondoka alikuwa akikutana na watu, aliwagawia fedha.
Kwa kuwa alishaondoka, ikawa ni zamu yangu kuombwa fedha. Kiana nikawa najitutumua lakini nilipozidiwa nikaanza kujikausha. Yule mdogo wake akanishauri kitu kimoja cha msingi.
Akaniomba bora niondoke na kurejea Dar es Salaam maana Kinshasa haukuwa mji salama na kitu kibaya zaidi watu wengi waliamini huenda Nonda aliniachia mamilioni ya dola. Akasema wangeweza kunivamia siku yoyote wakidhani nina mamilioni nimehifadhi.
TAYARI MALIMA AMEPEWA USHAURI WA KUONDOKA JIJINI KINSHASA. JE, ATAKUBALIANA NAO AU ATAAMUA KUENDELEA KULA RAHA NA WASHIKAJI ZAKE. endelea kufuatilia http://www.shaffihdauda.com/

3 comments:

  1. Dah kama zali namaliza kusoma sehemu ya kwanza nakutana na sehemu ya pili, Shaffih kwa kukata hadithi sehemu iliyokolea nakuvulia kofia yaani timing yako kama ya MR.Shigongo anapoweka nukta unatamani kuchukua simu umpigie umuulize nini kiliendelea ila si mbaya mdogo mdogo.
    Yaani aliposema Nonda alimkumbuka na kumuita nimejikuta nimeanza kushangilia kama vile tukio linatokea live.
    Ila hapo alipoanza tena kusahau maisha yake ya kupigika na akaanza upedeshee kinshasha alilikoroga, jombaaa na kusota kote kule akaanza tena kuzigawa kwa dirishani badala ya kukimbilia bongo fasta kuja kuweka mambo sawa, ila alichokizungumza ndicho haswaaa kinachotekeaga.
    Episode three mkuu.
    Mdau
    Mike

    ReplyDelete
  2. Shaffi hii imetulia safi sana, lakini kwa nini umei ondoa sehemu ya kwanza? kuna wengine hawakuisoma hivyo ili mtiririko uwe mzuri weka full kisa.

    Besides, hii ndio aina ya blogging tunayo miss watanzania, sina haja ya kutaja majina lakii blog nyingine ni photo album tu watu wanatungukia mapicha hakuna uchambuzi hata wa mistari miwili! kibaya zaidi hata vichwa vya habari mtu anakosea spelling sijui huwa wanakimbilia nini?

    Back to the story, kuna somo zito sana kwa wachezaji wetu wa kibongo, jamani mpira unalipa na mcheze kwa malengo sio kuifunga Yanga?simba ndio iwe ultimate goal, mfano wa Nonda na Haruna Moshi (samahani nimeshindwa kujizuia kutaja jina) unatupa somo zito. Nonda alipoipata zali akaitumia, lakini Boban kaitupia kwenye dirisha anadai eti kodi kubwa, sijui uwanja unajaa hela hapewi ushakuwa unalipwa mamilioni mambo ya gey=t collection yanakuhusu nini?

    Jirani zetu Kenya na Uganda washaanza kutuacha kwenye kucheza pro. Tukaze buti tu catch up nao, sisi tuna kila kitu soka letu la sasa lina udhamini mzuri kwa timu zote Stars wakubwa, Ngorongoro, Serengeti mpaka wanawake wa Twiga! Ligi ina udhamini wa nguvu timju binafsi Simba na Yanga, Azam, Mtibwa/Kagera sugar, timu za majeshi kuna academy sasa kila kona, alimuradi mambo ya mshiko sio issue tena watoto chezeni ball acheni mabangi hayo (samahani naandika kwa hasira)

    Mtaishia kuwafata akina Nonda and the likes na kulala magetin mpaka lini? Haya baada ya taabu yote baada ya kupewa fungu tu matanuzi!

    ReplyDelete
  3. Ni bonge la story.((HUSSEIN FROM TMK))

    ReplyDelete