Search This Blog

Wednesday, May 23, 2012

BAADA YA BOBAN KUANGUKA NA KUZIMIA - DAKTARI ASHAURI WACHEZAJI WA SIMBA KUPEWA TIBA YA SAIKOLOJIA

Baada ya Haruna Moshi kuzimia kwenye Uwanja wa Ndege wa Kinshasa juzi,  Daktari wa Timu ya Taifa 'Taifa Stars', Mwanandi Mwankemwa amesema wanawapa ushauri wa karibu wachezaji wa Simba waliopo katika timu hiyo ili warejee katika hali zao za kawaida.

Haruna 'Boban' presha yake ilishuka ghafla Jumatatu asubuhi alipokuwa Uwanja wa Ndege wa Kinshasa na kulazimika kupatiwa huduma  haraka na daktari wa uwanjani hapo kwa zaidi ya saa 1:30.

Daktari aliyemtibu, alimpa kahawa na chumvi na alimshauri asifikirie mambo mengi wala kufanya kazi ngumu kwa vile presha yake itashuka na kugharimu maisha yake.

Dk Mwankemwa alisema tukio la kifo cha ghafla cha Patrick Mafisango haliwezi kusahaulika mapema kwa wachezaji wenzake, na kwa sababu hiyo wanahitaji uangalizi wa karibu kiushauri ili kuhakikisha wanarejea kwenye hali yao ya kawaida.

Alisema kuna athari kubwa kwa mchezaji kucheza uwanjani huku akikosa utulivu wa akili kichwani kutokana na msongo wa mawazo juu ya tukio lolote la kusikitisha linaloweza kumgusa kwa karibu.

"Ni rahisi hata mchezaji kuumia anapocheza uwanjani, huku akili yake ikijaa kumbukumbu ya tukio baya kama ajali iliyosababisha kifo cha Mafisango," alisema Mwankemwa.

Daktari huyo alisema zaidi kuwa, ili mchezaji aweze kushiriki vizuri kwenye mchezo ni lazima aingie uwanjani akili yake ikiwa imetulia bila kuwa na msongo wa mawazo kwa jambo lolote lile.

"Kwa maana hiyo, tunachofanya kwa sasa ni kuwapa ushauri kila wakati ili kuwaondoa katika hali, tunatarajia hali itakuwa nzuri baada ya siku kadhaa, ingawa mwisho wa siku mwalimu wao (Kocha Kim Poulsen) ataamua ni wachezaji gani anaweza kuwatumia," alisema Mwankemwa ambaye pia ni daktari wa timu ya Azam FC.

Kauli ya kocha huyo imekuja siku chache tangu kiungo wa Simba, Moshi 'Boban' aliyeonekana kuguswa zaidi na kifo cha Mafisango kupata matatizo ya kiafya muda mfupi baada ya kushiriki mazishi Jumapili iliyopita.

Mchezaji huyo wa Simba tangu alipopokea taarifa ya kifo cha Mafisango alikuwa hawezi kuzungumza lolote zaidi ya kububujikwa na machozi ya uchungu, jambo ambalo linaweza pia kumwathiri kiuchezaji.

Boban ni miongoni mwa wachezaji walioitwa na Kocha Kim Poulsen kuunda kikosi cha timu ya Taifa (Taifa Stars) kinachojiandaa na mchezo wa ugenini dhidi ya Ivory Coast kuwania tiketi ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia.

1 comment:

  1. ni kweli kabisa wanahitaji tiba ya kisaikolojia ili waweze kucope up na situation, sijui kama Tanzania tuna pyschotherapy waliobobea, maana wanahitaji kweli counselling sababu kupoteza mtu wako wa karibu sio jambo jepesi kuvumilika

    ReplyDelete