Search This Blog

Friday, March 9, 2012

TALIB HILAL ATAKA KURUDI SIMBA KUENDELEZA HISTORIA

Beki wa zamani wa Simba SC, Talib Hilal amesema kwamba yupo tayari kurudi kuifundisha Simba kwa ajili ya mechi za Raundi ya Pili ya Kombe la Shirikisho Afrika, dhidi ya  ES Setif ya Algeria. Akizungumza na bongostaz mchana huu kutoka Oman, beki huyo mrefu ambaye alimalizia soka yake Oman, alisema kwamba Simba wakimuita atakuja kupiga kazi kumsaidia Mseriba Milovan Curkovic aweke historia Afrika.
Talib alierejea kutoka Oman na kujiunga na benchi la Ufundi la Simba mwaka 2003 kuinoa timu kwa ajili ya michezo ya Raundi ya Tatu ya Ligi ya Mabingwa, dhidi ya waliokuwa mabingwa watetezi, Zamalek ya Misiri.
Talib alikwenda kuiweka Simba kambini Oman kwa wiki moja ambako ilifunfishwa mbinu za kucheza na Waarabu.
Ikiwa inajivunia ushindi wa awali nyumbani 1-0 kwa bao pekee la Emmanuel Gabriel, Simba ilikwenda ‘kukomaa’ na kufungwa moja tu baaada ya dakika 120, hivyo mchezo kuhamia kwenye mikwaju ya penalti.
Juma Kaseja alicheza penalti moja ya Waarabu kabla ya Christopher Alex Massawe kwenda kukwamisha nyavuni penalti ya mwisho na kuivusha Simba kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza nay a mwisho katika historia ya klabu hiyo.
Katika benchi la ufundi, Simba ilikuwa chini ya Kocha Mkuu James Aggrey Siang’a kipa wa zamani wa kimataifa wa Kenya, aliyekuwa akisaidiwa na Jamhuri Mussa Kihwelo, beki mwingine wa zamani wa Simba SC.
Mwaka 1993 ikifika Fainali ya Kombe la CAF, zamani likijulikana kama Kombe la Abiola kwa sababu lililotolewa na Chifu Mashood Abiola wa Nigeria, Simba iliitoa Al Harrach ya Algeria katika Nusu Fainali, ikifungwa 2-0 Algiers na kushinda 3-0 Dar es Salaam.  
Simba imesonga mbele Kombe la Shirikisho baada ya kuitoa Kiyovu Sport ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2, wakianza na sare ya 1-1 Kigali kabla ya kushinda 2-1 Dar es Salaam na sasa itamenyana na 
ES Etif kati ya Machi 23 na 25 mwaka huu mjini Dar es Salaam kabla ya kurudiana wiki mbili baadaye ugenini. 

Je, Talib atapewa nafasi arudie maajabu yake ya 2003? Alhaj Ismail Aden Rage na Kamati yake ya Utendaji ya Simba, watatoa jibu.


Source:  bongostaz.blogspot.com/

No comments:

Post a Comment