Search This Blog

Saturday, March 17, 2012

HAMIS KIIZA AIPANDISHA YANGA NAFASI YA PILI NA GOLI LA DK. ZA MAJERUHI

  Goli la dakika ya 89 lililofungwa na Hamisi Kiiza jioni hii wakati Yanga ilipocheza na Villa Squad Uwanja wa Taifa,  Dar es Salaam katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, liliiwezesha Yanga kutoka kifua mbele kwa kujipatia pointi tatu muhimu katika ligi hiyo.
Yanga sasa inapanda hadi nafasi ya pili, kwa kutimiza pointi 43 baada ya kucheza mechi 20, sawa na vinara Simba SC wenye pointi 44, ambao leo wanacheza mechi ya 21 na Mtibwa Sugar. Azam yenye pointi 41, inashuka hadi nafasi ya tatu na kuwaachia ‘wanaume’ anga zao.
Kiiza aliipatia timu yake bao hilo pekee baada ya kumalizia kazi nzuri iliyoanzishwa na Haruna Niyonzima kisha Godfrey Taita kuachia shuti kali la mbali lililomkuta mfungaji aliyekwamisha wavuni  na kuwainua mashabiki wao katika dakika hizo za lala salama ambao walikuwa vichwa chini wakitarajia mechi hiyo ingekwisha kwa suluhu.
Hasa baada ya Davies Mwape kuwakatisha tamaa kwa kukosa nafasi nyingi za kufunga hasa ile ya dakika 69 baada ya Pius Kisambale kumtengenezea mpira mzuri hivyo kuwakera mno mashabiki wao.
Mbali ya Mwape, Kenneth Asamoah naye alikosa bao la wazi akiwa yeye na kipa wa Villa Squad, Daudi Mwasongwe dakika ya 57 aliposhindwa kuitendea haki krosi ya Haruna Niyonzima.
Villa itabidi ijilaumu kuruhusu nyavu zao kutikiswa dakika za lala salama kwani walikuwa wameishawabana Yanga kwa kuonyesha kandanda safi na kuufanya mchezo huo kuwa mgumu kwa pande zote lakini wakishindwa kuhimili vishindo.
Katika nafasi ambazo Villa itazijutia, ni dakika ya 22 baada ya mchezaji wao, Martin Rupert kupiga mpira nje ya lango  la Yanga akiwa peke yake na kushindwa kucheka na nyavu huku mchezaji huyo akiendelea kufanya makosa ya kushindwa kucheka na nyavu dakika 71 baada ya kumpoka mpira Oscar Joshua.
Hata hivyo pambano hilo ambalo matokeo yake yalikuwa yakisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka, lilikuwa zuri na kuwa kivutio kwa mashabiki waliojitokeza uwanjani.
Katika mchezo mwingine leo, Coastal Union imefanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya maafande ya JKT Orjolo huo pia ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu.
Bao la Coastal Union lilifungwa dakika ya 18 na Salum Sued kwa penati baada ya  mchezaji mwenzake, Daniel Lyanga kukwatuliwa katika eneo la hatari na mchezaji wa JKT Orjolo, Omary Mswaki.
Ligi hiyo itaendelea leo katika viwanja viwili ambapo katika Uwanja wa Jamhuri Morogoro, Simba itatoana jasho na Mtibwa Sugar huku katika dimba la Chamazi, wenyeji Azam FC ikiwakaribisha maafande wa Ruvu Shooting.

1 comment:

  1. Tunakuomba Shafii Dauda Uitangaze page yetu kwani tunaamini wapo mashabiki wako wengi tu katika blog yako na ACCOUNT YAKO ya facebook ambao wanaipenda clabu yetu lakini hawaifahamu page yetu ya Coastal union
    www.Facebook.com/CoastalUnion

    ReplyDelete