Search This Blog

Friday, February 10, 2012

TAARIFA KUTOKA TFF

LIGI KUU YA VODACOM 2011/2012

Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaingia raundi ya 17 kesho (Februari 11 mwaka huu) kwa mechi tano huku ile ya Kagera Sugar na Mtibwa Sugar iliyokuwa ichezwe Februari 12 mwaka huu ikilazimika kusogezwa mbele kwa siku moja. Mechi za kesho (Februari 11 mwaka huu) ambazo zitaanza saa 10 kamili jioni ni kati ya Simba na Azam (Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam), Toto Africans na Moro United (Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza), Polisi Dodoma na Villa Squad (Uwanja wa Jamhuri, Dodoma), Coastal Union na African Lyon (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga) na JKT Oljoro na JKT Ruvu (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha). Kagera Sugar na Mtibwa Sugar sasa zitacheza Februari 13 mwaka huu kwa vile Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba siku ya Februari 12 mwaka huu umetolewa kwa shughuli za kijamii. Mabadiliko hayo pia yamesababisha mechi kati ya Toto Africans na Mtibwa Sugar iliyokuwa ichezwe Februari 15 mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba sasa kuchezwa Februari 16 mwaka huu. Nayo mechi namba 119 kati ya Yanga na Ruvu Shooting iliyokuwa ichezwe Februari 12 mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam- Chamazi, sasa itafanyika siku hiyo hiyo kwenye Uwanja wa Taifa. Mechi hiyo imehamishiwa Uwanja wa Taifa kutokana na maombi ya Yanga kwa vile itakuwa ni sehemu ya sherehe za maadhimisho ya miaka 77 tangu kuasisiwa kwa klabu hiyo.

MGAMBO, MORANI KUCHEZA FEB 12

Mechi ya Kundi A ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kati ya Mgambo Shooting ya Tanga na Morani ya Manyara iliyokuwa ichezwe Februari 11 mwaka huu kama ilivyokuwa ile ya Kundi C kati ya AFC ya Arusha na Polisi ya Morogoro zimesogezwa mbele kwa siku moja.Mabadiliko hayo yametokana na mechi hizo kuingiliana na za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zinazochezwa kwenye viwanja vya Mkwakwani, Tanga na Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha. Mechi nyingine za FDL zitaendelea kesho (Februari 11 mwaka huu) kama ratiba inavyoonesha. Kundi A, Burkina Faso itakuwa mwenyeji wa Polisi Dar Salaam kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro wakati Temeke United na Transit Camp zitaoneshana kazi Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi. Kundi B litashuhudia mechi kati ya Mbeya City na Majimaji kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya huku JKT Mlale wakiwa wenyeji wa Small Kids kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea. Nayo Tanzania Prisons itakuwa mgeni wa Polisi Iringa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora. Mechi ya Kundi C itakuwa moja ambapo Rhino FC itakaikaribisha 94 KJ ya Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

 KOZI YA MAKOCHA NGAZI PEVU YAAHIRISHWA

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeahirisha kozi ya ukocha ngazi pevu (Advanced Level) iliyokuwa ifanyike jijini Dar es Salaam kuanzia Februari 12- 25 mwaka huu. Kozi hiyo imeahirishwa kwa vile wengi wa makocha walioomba hawakufikia vigezo vilivyowekwa. Vigezo vya msingi vilikuwa mwombaji awe na cheti cha ukocha ngazi ya kati (Intermediate Level), wawe wanafanya kazi hiyo ya ukocha (active) na kuwasilisha cheti cha elimu ya sekondari (kidato cha nne). Mwisho wa kuwasilisha maombi kwa ajili ya kozi hiyo ilikuwa Februari 5 mwaka huu. Makocha 34 waliwasilisha maombi kwa ajili ya kushiriki kozi hiyo, lakini waliokidhi vigezo ni 12 tu. Makocha waliokidhi vigezo kwa ajili ya kozi hiyo ni Sospeter Vedasto kutoka mkoani Pwani, Beatus Manga (Temeke), Renatus Shija (Pwani), Ntungwe Selemani (Pwani), William Mamiro (Kinondoni), Ngawina Ramadhan (Temeke), Khatib Mtoo (Temeke), Hamisi Chimgege (Temeke), Selemani Mkumya (Temeke), Idd Cheche (Azam), Mohamed Mayosa (Temeke) na Imam Mbarouk (Shinyanga). Wawezeshaji wa kozi hiyo ambayo sasa tarehe yake ya kufanyika itatangazwa baadaye ni Mkufunzi wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Jan Poulsen, Mkufunzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Sunday Kayuni na Mkufunzi wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Denmark (DBU), Kim Poulsen. 

KIPRE BOLOU WILFRIED RUKSA AZAM

Mshambuliaji Kipre Bolou Wilfried aliyejiunga na Azam kutoka Ivory Coast sasa ni ruksa kuichezea timu hiyo michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inayoendelea kwenye viwanja mbalimbali nchini. Shirikisho la Mpira wa Miguu la Ivory Coast (FIF) jana (Februari 9 mwaka huu) limetoa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa mchezaji huyo aliyeombewa uhamisho katika dirisha dogo la usajili kutoka timu ya Sewe Sport ya nchini humo.

YANGA, MTIBWA SUGAR ZAINGIZA MIL 49/-

Pambano la Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Yanga na Mtibwa Sugar lililochezwa Februari 8 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh. 49,510,000. Jumla ya watazamaji 14,604 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo namba 112 kwa kiingilio cha sh. 3,000, sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 15,000 kwa VIP A. Baada ya kuondoa gharama za awali za mchezo na asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 7,552,372.88 kila timu ilipata sh. 8,933,048.14, uwanja sh. 2,977,682.71.  Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,191,073.08, TFF sh. 2,977,682.71, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 1,488,841.36, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 297,768.27 na asilimia 10 ya gharama za mechi ni 2,977,682.71. Gharama za awali za mechi zilikuwa nauli ya ndani kwa waamuzi sh. 10,000, nauli ya ndani kwa kamishna wa mchezo sh. 10,000. Posho ya kujikimu kwa kamishna na waamuzi sh. 160,000, mwamuzi wa akiba sh. 30,000, tiketi sh. 4,000,000, maandalizi ya uwanja (pitch) sh. 400,000, umeme sh. 300,000, usafi na ulinzi kwa uwanja sh. 2,350,000 na Wachina (Beijing Construction) sh. 2,000,000.  Gharama nyingine ni Jichangie ambayo ni sh. 200 kwa kila tiketi; kila klabu ilipata sh. 1,022,280 wakati Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kilipata sh. 876,280. 

MECHI ZA YANGA, SIMBA CAF

Klabu za Zamalek ya Misri na Kiyovu Sport zimekataa maombi ya mechi zao za marudiano za Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho dhidi ya Yanga na Simba kusogezwa mbele kwa wiki moja kutoka wikiendi ya Machi 2, 3 na 4 mwaka huu. Baada ya mazungumzo na klabu za Simba na Yanga, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) lilituma maombi Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuomba mechi hizo zisogezwe ili wachezaji wapate fursa ya kutosha kuzitumikia klabu zao na timu ya Taifa (Taifa Stars). Februari 29 mwaka huu Taifa Stars itacheza mechi ya mchujo ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa ajili ya fainali za mwakani nchini Afrika Kusini dhidi ya Msumbiji kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Wikiendi ya Machi 2, 3 na 4 mwaka huu Yanga itakuwa inarudiana na Zamalek ugenini wakati Simba itarudiana na Kiyovu Sport jijini Dar es Salaam. CAF ilikuwa tayari kuridhia maombi hayo iwapo Chama cha Mpira wa Miguu cha Misri (EFA) na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Rwanda (FERWAFA) wangekubali. Lakini EFA na FERWAFA wamekataa ombi hilo kwa vile litavuruga ratiba ya mechi za ligi katika nchi hizo

Boniface Wambura

Ofisa HabariShirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment