Search This Blog

Wednesday, October 12, 2011

WAMBURA: TFF NDIO WALIOIUA STARS MICHUANO YA AFRIKA


Mgombea nafasi ya uenyekiti katika chama cha soka cha soka mkoani Mara ambaye amewahi kuwa katibu mkuu wa chama cha soka nchini TFF zamani FAT, Michael Wambura amedai kuwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), linapaswa kubeba lawama kutokana na timu ya soka ya Taifa ‘Taifa Stars’ kushindwa kufuzu fainali za Afrika mwaka 2012.


Wambura alisema TFF haiwezi kukwepa lawama kwani baadhi ya viongozi wao wameshindwa kusimamia vyema majukumu ya timu hiyo badala yake nguvu zao wamezielekeza zaidi kwenye Uchaguzi Mkuu wa shirikisho hilo utakaofanyika mwakani.

“Taifa Stars ilikuwa na nafasi nzuri ya kufuzu kabla hata ya mechi ya Algeria Juni mwaka huu
hapa Dar es Salaam, lakini baadhi ya viongozi mambo yao ni uchaguzi wa TFF utakaofanyika
mwakani.

“Hivi sasa mipango mingi ni kuhusu uchaguzi huo, wanajipanga namna ya kudhibiti watu, wanapanga namna ya kumdhibiti Wambura (yeye), huwezi ukaendesha mpira kwa jinsi hiyo.

“Matokeo yake tulishindwa kuifunga Algeria nyumbani tukatoka sare, Jumapili iliyopita bado
tulikuwa na nafasi lakini ugonjwa wetu ukaendelea, badala ya kuelekeza nguvu kuiua Morocco
unasafiri kwenda Mara kuona namna ya kumzuia Wambura asiwanie uongozi Mara.

“TFF wananisikitisha sana, yaani wakisikia Wambura anataka kuwania uongozi
wanachanganyikiwa kabisa, matokeo yake ndiyo hayo Taifa Stars imekwama, Watanzania hatuna haja ya kumlaumu Poulsen (Jan-Kocha Mkuu wa Taifa Stars), sababu zinajulikana wazi,” alisema.

Alieleza kuwa hata kukosekana kwa mchezaji Nizar Khalfan anayecheza soka nchini Canada ni
kutokana na kuchelewa kutumwa taarifa kwa timu yake ya Vancouver Whitecaps, kwa sababu
mawazo ya watu ni uchaguzi wa mwaka 2012.

“Unaweza ukabeza kauli yangu, lakini ukweli ni kuwa hivi sasa kuna chaguzi za vyama vya
mikoa, sasa baadhi ya viongozi wa TFF mawazo yao ni uchaguzi na kuona mikoani wanaenda
watu gani na kama ni wafuasi wao au la, kama sio wao wanawadhibiti na kuweka wao, hii ni hatari,” alisema Wambura.

Wambura amejitosa kuwania uenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mara
(FAM), ambacho awali ilikuwa kifanye uchaguzi Jumamosi ijayo, lakini umesogezwa mbele na TFF hadi mwezi ujao kutokana na kuelezwa kuwa baadhi ya taratibu za uchaguzi hazikufuatwa.


No comments:

Post a Comment