Search This Blog

Monday, October 3, 2011

TFF inahitaji Mkurugenzi bora wa Masoko na si bora mkurugenzi…

NI siku nyingine ambayo nimepata nafasi ya kutoa hoja kuhusu mambo mbalimbali yahusuyo soka la Tanzania.
Kikubwa hasa ni masikitiko makubwa niliyoyapata baada ya kulipotiwa mapato ya mchezo wa ligi kuu ya Vodacom kati ya Villa Squad na Moro Utd yalikuwa kama ifuatavyo (
Mapato: Vila Squad vs Moro Utd Tzs 396,000
Waamuzi wakachukua posho Tzs 40,000 ( nauli ya kamishna 20,000,waamuzi 20,000 na kila klabu ikipata Tzs 9,240
)

Moja kati ya vitu ambavyo tunaweza kuvibadili haraka ni mfumo halisi wa uongozi katika baadhi ya nafasi ili baadhi ya kazi ziweze kutekelezwa kwa ufanisi zaidi.
TFF inahitaji kuwa na Mkurugenzi wa Masoko au Meneja Masoko mwenye uwezo na si bora kuwa na mkurugenzi wa masoko.
Mkurugenzi wa masoko anapaswa kuwa na uelewa wa hali ya juu wa mbinu za kutengeneza mipango ya muda mfupi na mrefu na pia kutengeneza timu ya watendaji wa kuitekeleza na kusimamia mipango husika.
Mipango ya muda mrefu ni kama kuhakikisha kuwa wadhamini wachache waliopo wanapata “manufaa makubwa zaidi ya uwekezaji ili kuwahamasisha wengine ama kutaka kununua mikataba, au kuongeza udhamini, ni ajabu Ligi kushindwa kurushwa na televisheni hasa mechi kubwa kama ile kati ya Simba na Yanga.
Ni ajabu mechi za Ligi Kuu kukosa promosheni ya kuhamasisha mashabiki kuhudhuria viwanjani. Utamaduni wa kufanya mikutano na waandishi mbele ya kuta za matangazo ya wadhamini na mambo mengine yataifanya Ligi kuwa nadhifu na kuwavutia wawekezaji kuweka fedha za udhamini.
Badala ya kuongeza mapato kwa kutoa kibali kwa kampuni ya Catering kuuza vitafunwa vya VIP kwa bei ya juu kwa waheshimiwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa waheshimiwa wote akiwemo Rais wa TFF wananunua tiketi za kuangalia mechi, TFF imekuwa ikinunua vitafunio na kugawa bure kwa waheshimiwa walioingia bure uwanjani unyonyaji kama huu unaumiza klabu na kudidimiza maendeleo ya soka.
Blog yako kama kawaida yake inaainisha majukumu ya Jumla ya Meneja au Mkurugenzi Masoko wa TFF, majukumu haya yatatoa picha halisi ya faida ya kuwa na mtu kama huyo.
Majukumu ya Jumla
• Kuandaa mipango ya Matangazo, Mauzo na Masoko kufikia malengo ya TFF
• Kutafiti, kuainisha, na Kuorodhesha vyanzo vyote vya mapato ya TFF kama haki za matangazo ya redio na Televisheni, Udhamini wa makampuni, Mapato yatokanayo na mauzo ya Tiketi, na Mauzo ya vifaa vyenye nembo ya TFF kama Bendera, Kalenda, Nguo nk
• Kutafiti, Kuandaa, Kutengeneza Mipango na michanganuo yote, kutafuta wadhamini na kisha kuisambaza kwa makampuni yaliyokusudiwa.
• Kujenga hoja kwa wadhamini waliopo ili kuiboresha mikataba iliyopo.
• Kuhakikisha kuwa ni wadhamini tu wanaonufaika na fursa zozote zilizopo kwenye mpira wa miguu kwa kudhibiti Taasisi, Kampuni au mtu binafsi anayeweza kunufaika na matangazo au fursa bila kuchangia maendeleo ya soka (Mfano mzuri ni redio zinazotangaza mechi, au makampuni yaliyoweka matangazo viwanjani kama Aboud Soap Industries & Bus Services, Hood Bus services, Masumin Printways & Stationery, Castle Lager, Cocacola etc kama Ligi ni ya Vodacom basi tunatarajia kuona matangazo ya Vodacom na Klabu husika tuu)
• Kutafiti na kuandaa utaratibu wa kisayansi wa kudhibiti wizi wa mapato milangoni kama kutumia mashine maalum za kukatishia tiketi.
• Kutengeneza mikakati ya kuhakikisha wapenzi wa mpira wa miguu wanajaa viwanjani, (kufanyia promosheni michezo ya Ligi Kuu kwa kuongeza burudani kama za muziki kabla ya mechi na kutumia redio na televisheni katika kufanya promosheni, sanjari na kuimarisha ulinzi wa wapenzi wa soka na mali zao.
• Kufanyia utafiti wa mahitaji ya wateja (watazamaji wa mechi na Wadhamini), kulisoma soko na washindani waliopo.
• Kufanyia kazi (marketing plan) aliyoitengeneza
• Kutengeneza mahusiano mazuri baina ya wadhamini ikiwa ni pamoja na kuongeza wadhamini
• ili kupunguza mzigo wa gharama kwa wadhamini waliopo
• Kuandaa bajeti ya kitengo chake, kuisimamia bajeti yake na kuhakikisha kuwa bajeti aliyopewa inafanyakazi kwa tija
• Kutengeneza timu ndogo ya watendaji wa moja kwa moja watakaokuwa wakilipwa kamisheni (Direct Sales Agents) isiyozidi watu watatu. Kuwapa mafunzo watendaji hawa, kuwasimamia na kuwaongoza.
• Kujenga, Kusimamia na Kuboresha kuendeleza mahusiano bora baina Shirikisho na vyombo vya habari.
• Kujenga utaratibu wa kusaidia miradi ya maendeleo ili kuliweka shirikisho jirani zaidi na Jamii
Elimu, Uzoefu na Sifa za Mkurugenzi wa Masoko
Taasisi nyingi zilizo makini huzingatia zaidi uzoefu na rekodi za muhusika anayetaka nafasi ya Ukurugenzi masoko.
Ndiyo maaana mara nyingi tumeshuhudia wakurugenzi masoko wakinunuliwa kama wachezaji mahiri wanavyohamishwa toka timu moja kwenda nyingine.
Hapa Tanzania benki, kampuni za bia na makampuni ya simu za mikononi wamekuwa wakitumia mfumo huu, lakini kimsingi Mkurugenzi wa Masoko wa TFF lazima awe na Digrii ya Mauzo na Masoko (Degree in Sales and Marketing) ni vizuri pia kama mhusika atakuwa na nyongeza ya cheti toka katika taasisi za masoko (Chartered Institute of Marketing ‘CIM’).
Uwepo wa Mkurugenzi mwenye uwezo wa Masoko utaliwezesha Shirikisho kujipatia mapato hata mara nne ya mapato yanayopatikana leo.

1 comment:

  1. Pia Rais wa TFF anatakiwa awe mtendaji sio kuwepo tu kama Mfalme tu na kula posho tu. Inabidi pia waajiri watu wenye mapenzi, ujuzi wa masoko (soko la Tanzania) na kuwajua vizuri wapenda soka wanataka nini, Naamini tupo watu ambao hatujacheza mpira kwenye madaraja ya juu au timu kama simba na yanga kwa sababu za kimsingi zaidi. meneja masoko sijui yupo kwa ajili ya nani? haiwezekani ligi kuu ichezwe kama kombe la mbuzi mtaani. nani wa kuangalia muda wa kazi? Yapo mengi sana. Peter Ngassa

    ReplyDelete