Search This Blog

Thursday, October 20, 2011

NIGERIA NA CAMEROON ZAJITOA CECAFA CHALLENGE CUP 2011


Timu za soka za mataifa ya Cameroon na Nigeria yametangaza kujitoa katika kinyang'anyiro cha michuano ya Baraza la Vyama vya Soka la Nchi za Afrika Mashariki na Kati(CECAFA)iliyopangwa kufanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Novemba 24 hadi Desemba 10.

Jumla nchi 11 wanachama wa baraza hilo zinatarajia kushiriki katika patashika hiyo ikiwemo Sudan, Ethiopia, Uganda, Kenya, Eritrea, Rwanda, Burundi, Zanzibar, Djibouti, Somalia na wenyeji Tanzania.

Kabla ya kutangaza kujitoa, Cameroon na Nigeria zilikuwa miongoni mwa nchi tano kutoka nje ya ukanda huo zilizowasilisha maombi zikitaka kushiriki michuano hiyo ambayo itafanyika kwa mara ya pili mfululizo katika ardhi ya Tanzania.

Nchi nyingine zilizowasilisha maombi hayo ni pamoja na Malawi, Afrika Kusini, Zimbabwe, Zambia na Ivory Coast ambayo pia ilishiriki kama nchi mwalikwa katika michuano iliyopita iliyofanyika pia nchini.

Akizungumza kwa simu kutoka Naironi jana, Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholaus Musonye alisema kuwa ofisi yake imepokea taarifa za kujitoa kwa nchi hizo pasipo maelezo mengine ya ziada kuhusu sababu za kujitoa kwao.

"Kwa ujumla sisi tunaendelea na maandalizi kama kawaida labda tu jambo jipya ni kwamba Cameroon na Nigeria ambazo awali ziliomba kushiriki zimetoa taarifa ya kujiondoa,"alisema Musonye.

Hata hivyo Musonye alisema kuwa ni nchi mbili tu kati ya tatu zilizosalia ndizo zinazoweza kupewa nafasi ya kushiriki michuano hiyo ambayo bingwa mtetezi ni Kilimanjaro Stars.

"Kimsingi tuna nafasi mbili tu kwa nchi waalikwa na hii ni kutokana na suala zima la bajeti iliyopo hii ina maananisha si nchi zote zilizoomba zitakubaliwa,"alisema Musonye.

Alisema kuwa viongozi wa baraza lake wanatarajia kukutana jijini Dar es Salaam wiki ijayo na kuchagua timu zitakazoalikwa kushiriki michuano hiyo.

Kwa upande mwingine kujitoa kwa Cameroon na Nigeria kunaweza kukawa na uhusiano na matokeo mabaya iliyokutana nayo nchi hizo ambapo hazikufanikiwa kufuzu kushiriki katika fainali zijazo za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwakani katika nchi za Guinea ya Ikweta na Gabon.

No comments:

Post a Comment