Search This Blog

Saturday, September 24, 2011

SENDEU APIGWA FAINI SH. 500,000


Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inayoongozwa na Kamishna wa Polisi mstaafu Alfred Tibaigana imempiga faini ya sh. 500,000 na kuwekwa chini ya uangalizi kwa miezi sita Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu baada ya kumuona ana hatia kwa mashtaka yaliyowasilishwa dhidi yake na TFF.

Uamuzi wa kamati hiyo iliyokutana leo (Septemba 24 mwaka huu) umetokana na ushahidi uliowasilishwa na TFF, na pia Sendeu mwenyewe kukiri kuwa alifanya makosa.

Sekretarieti ya TFF ilimshtaki Sendeu kwenye kamati hiyo kutokana na matamshi yake dhidi ya mwamuzi Alex Mahagi mara baada ya mechi kati ya Yanga na Ruvu Shooting iliyochezwa Septemba 10 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Sendeu aliita mkutano na waandishi wa habari na kumshutumu Mahagi kuwa alisababisha timu yake ikose ushindi kwa kuwabeba wapinzani wao na kudai anamfahamu Mahagi kuwa ni mwanachama wa Simba, kadi nyekundu aliyompa kiungo wao Haruna Niyonzima si halali na alifanya hivyo kwa lengo la kuisadia Simba ili iendelee kukaa kileleni mwa ligi.

Kauli hiyo ililenga kumjengea chuki Mahagi mbele ya mashabiki wa Yanga kama ilivyo kwa viongozi na watendaji wa TFF wakati Sendeu akiwa ofisa wa Yanga alikuwa anajua taratibu za kufanya pale klabu yake isiporidhishwa na uamuzi wa mwamuzi au suala lingine lolote.

Kamati hiyo haikusikiliza mashtaka dhidi ya Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage kwa vile hakufika kwenye kikao kutokana na kuwa katika kampeni za uchaguzi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwania ubunge wa Jimbo la Igunga mkoani Tabora.

Pia kamati hiyo haikusikiliza mashtaka ya kwanza ya Sendeu kwa vile yanakwenda pamoja na yale ya Rage. Kamati itapanga tarehe nyingine kwa ajili ya kusikiliza mashtaka dhidi ya viongozi hao ambapo watapewa taarifa.

LIGI DARAJA LA KWANZA KUANZA OKT 15
Wakati michuano ya Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara inayoshirikisha timu 18 imepangwa kuanza Oktoba 15 mwaka huu timu ambazo hazijakamilisha usajili wa wachezaji zimeongezewa muda hadi Oktoba Mosi mwaka huu.

Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana leo (Septemba 24 mwaka huu) chini ya Mwenyekiti wake Makamu wa Pili wa Rais, Ramadhan Nassib pia imepanga makundi ya ligi hiyo itakayochezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini.

Oktoba 3-9 mwaka huu majina ya wachezaji walioombewa usajili na timu zote 18 yatabandikwa kwenye ubao wa matangazo wa TFF kwa ajili ya pingamizi, na Kamati ya Mashindano itakutana Oktoba 10 mwaka huu kwa ajili ya kupitia majina hayo.

Kundi A litakuwa na timu za Mgambo Shooting Stars ya Tanga, Morani ya Manyara, Polisi Dar es Salaam, Temeke United ya Dar es Salaam, Transit Camp ya Dar es Salaam na Burkina Faso ya Morogoro.

Timu zinazounda kundi B ni Majimaji ya Songea, Mbeya City Council, Mlale JKT ya Ruvuma, Polisi Iringa, Small Kids ya Rukwa na Tanzania Prisons ya Mbeya. Kundi C ni 94 KJ ya Dar es Salaam, AFC ya Arusha, Polisi ya Morogoro, Polisi ya Tabora, Rhino Rangers ya Tabora na Samaria ya Singida.

No comments:

Post a Comment