Search This Blog

Wednesday, August 24, 2011

wapi ambako Mancini anataka kumchezesha Nasri?


Kocha wa Manchester City Roberto Mancini ana sifa moja ambayo waitaliano wengi wanayo , kwa lugha ya kigeni Mancini unaweza kumuita ‘perfectionist’ , yaani mtu anayetaka mambo yaende sahihi pasipo na chembechembe yoyote ya makosa ndani yake.
Wakati huo huo unaweza pia kumuita Mancini mtu mwenye tama,Hebu pata picha unapokwenda na mtoto wako wa miaka minne kwenye duka la vitu vitamu vitamu kama keki , ice-cream , koni , juisi , pipi na ‘mazagazaga yote unayojua watoto wanayapenda kutokana na utamu wake , halafu ukamwambia achague kitu kimoja aondoke nacho , usishangae dogo akikwambia ‘baba tuhamishie hili jumba lote nyumbani kwetu’, yote hii ili awe karibu na vitu hivyo vitamu awe anaonja kimoja baada ya kingine siku hadi siku, Mancini ni mfano wa hili.

Angalia alivyoanza ligi kwa kuifunga Swansea City mabao 4-0 halafu ushindi dhidi ya Bolton wanderers ugenini wa mabao 3-2 halafu masaa 48 baada ya ushindi wa mwisho anafanya usajili wa kumuongeza Samir Nasri kwenye kikosi chake.

Labda urudi nyuma na kujiuliza ushindi huo ulipatikanaje kwenye hizo mechi mbili? na Kama kocha unapata picha gani baada ya michezo hiyo miwili ?
Picha ya kwanza ni ukweli kuwa hii ni timu ambayo haina shida kwenye safu ya ushambuliaji kwani kwenye mechi mbili tu wamepachika wavuni mabao 7.

Picha ya pili unayoipata ni kwamba kuna matatizo kwenye safu ya ulinzi na kwa jinsi yalivyoonekana kwenye mchezo wa Bolton.
Kweli majibu ya maswali haya ni kumsajili nasri ? Mancini acha masihara!
Kwenye mchezo dhidi ya Bolton Mario Balotelli,Carlos Tevez ,Adam Johnson wote walikaa benchi siku iyo.


Ukiacha hao kuna wachezaji wengine ambao hatma zao hazijajulikana mfano kama Craig Bellamy, Nedum Onuoha ,Dedryck Boyata , Michael Johnson , Shaun Wright Philips halafu bado unamsajili Samir Nasri.

Emanuel Adebayor ameenda Totenham kwa mkopo na Craig Bellamy wameshindwa kuuzwa kwa sababu wanalipwa mishahara mikubwa na pia walinunuliwa kwa fedha nyingi hivyo ni lazima wauzwe kwa fedha nyingi pia kwa timu itakayokuwa tayari kuwalipa mishahara mikubwa , la sivyo Man City inalazimika kuwapeleka wachezaji hawa kwa mkopo huku ikiendelea kuwalipa mishahara mpaka watakapomaliza mikataba yao.

Tatizo hili hili ndio limesababisha Sergio Aguero anunuliwe. Kumbuka ‘timbwili’ la Carlos Tevez ambaye kwa mdomo wake amesema kuwa anataka kuondoka, Corinthians walikuwa tayari kumsajili lakini suala la fedha likazuia.

Inter Milan walikuwa wanataka kumsajili lakini fedha nyingi watakazolazimika kulipa kwa ajili yake na zile watakazolazimika kumpa kama mshahara zimewafanya washindwe na ndio maana leo hii Carlos Tevez na Sergio Kun Aguerro wamejikuta wakiwa kwenye timu moja ambayo haina nafasi ya wote wawili kuwemo kwenye kikosi cha kwanza .

Samir Nasri amekuwa akitumika Arsenal kama kiungo wa kati na wakati mwingine akitokea upande wa kushoto , vivyo hivyo kwenye timu yake ya taifa Ufaransa .

City kuna David Silva , mchezaji ambaye anaweza kucheza kwenye winga zote na anaweza kujaza nafasi ya kiungo wa kati tena zaidi hata ya Nasri , ukiacha Silva wapo viungo wa pembeni kina James Milner na Adam Johnson.

Kauli ya Mancini baada ya mchezo dhidi ya Bolton ilikuwa ni Man City kuhitaji kuongeza umakini kwenye eneo la ulinzi, mara akaibuka na kauli nyingine eti Man City inahitaji kusajili walau mchezaji mmoja ili kikosi kikamilike.

Kwa kuoanisha kauli hizo mbili ungeweza kudhani kuwa Mancini tayari ameshazungumza na Gary Cahill na anajiandaa kumsajili ili aje kucheza na Vincent Kompany japo wapo mabeki wa kati kina Boyata na Onuoha ambao wana uwezo mkubwa tu lakini unapotea taratibu.
Hakuna anayejua kinachoendelea kwenye kichwa cha Mancini zaidi yake mwenyewe lakini Samir Nasri ni mchezaji ambaye City walikuwa hawamhitaji kwa kuwa wana aina ya wachezaji kama yeye .

No comments:

Post a Comment