Search This Blog

Tuesday, August 30, 2011

Nii Lamptey, Pele aliyepotezwa na kupotea



. Aliteswa na baba yake kila kukicha
. Alitapeliwa mamilioni na wakala wake
. Kila siku anajifungia chumbani akilia

ILIKUWA ni katika mji wa Motherwell Juni 1989 wakati kwa mara ya kwanza dunia ilipomtambua Nii Ordety Lamptey. Ilikuwa ni katika pambano la ufunguzi la michuano ya kombe la dunia kwa vijana chini ya umri wa miaka 16.
Akiwa na miaka 14, Lamptey alionyesha kiwango cha kuishangaza dunia wakati huo katika pambano la ufunguzi kati ya Ghana na Scotland lililokwisha kwa suluhu ya bila kufungana.
Wakati mfalme wa soka Ulimwenguni Pele akimkabidhi kikombe kidogo Lamptey mara baada ya kumalizika kwa pambano hilo ikiwa ni ishara ya kuchaguliwa mchezaji bora wa mechi hiyo, alijikuta akimsifu kuliko kiasi huku akisema huyo alikuwa kinda pekee duniani ambaye alifanana kwa kila kitu nayeye mwenyewe enzi za usakataji wa soka lake.
Lamptey alionekana kujiandaa na safari ya kufanya mambo makubwa duniani. Lakini katika historia ya kusikitisha kupindukia, leo miaka 20 baadaye, maisha yake ya soka yamemalizika kimya kimya.
Akiwa amecheza chini ya mechi 200 tu, Lamptey amekumbana na mikasa mizito na nuksi zilizopindukia katika namna ambayo mwenyewe amefikia hatua ya kuamini kuwa alitolewa mhanga au kurogwa na baadhi ya watu.
Hata hivyo, moyo wa Lamptey bado haujavunjika moja kwa moja. Ingawa bado analia kwa matukio mabaya yaliyomtokea, lakini sasa anaendesha shule jijini Accra akiwa amepania kuwafundisha wengine kutodanganywa kama ilivyotokea kwake.
Maisha yake kwa sasa yamebaki kuwa Shule tu. Ukiwa unatembea katika madarasa unaweza kuona yote ameyapachika majina ya nchi alizochezea soka ambazo ni Uholanzi, Ubelgiji, Uingereza, Italia, Argentina, Uturuki, Ureno, Ujerumani, China, Dubai, Afrika Kusini na mwishowe nyumbani Ghana.
Lakini mji wa Motherwell unasimama kama nguzo imara kwa sababu uliibua kipaji chake na kumuondoa katika historia ya kusikitisha iliyomgubika siku za utoto wake.
>Kipaji cha Lamptey kilikuwa wazi tangu angali akiwa mdogo. Tangu akiwa na umri wa miaka minane tayari klabu mbalimbali zilikuwa zinasaka saini yake. Akiwa na umri wa miaka 13 tu tayari alikuwa anacheza katika michuano ya vijana chini ya miaka 20.
Alikuwa mwepesi, mwenye nguvu, akili na kipaji kikubwa cha kuusoma mchezo. Alikuwa mfupi na mwenye uwezo wa ajabu. Lakini maisha yake ya Accra , mji mkuu wa Ghana hayakuwa rahisi. Yalikuwa magumu sana .
“Sikuwa na uhusiano mzuri wa kifamilia” anasema Lamptey. “Nilikuwa kila sehemu. Wakati mwingine nisingerudi nyumbani. Ningekwenda kucheza soka lakini kurudi nyumbani ingekuwa matatizo. Lazima ningepigwa na Baba, au kutumwa kwenda kuchota maji kabla ya kunipatia chakula. Wakati mwingine usiku ningelala chini ya gari au Kioski fulani na kesho yake maisha yangeanza upya tena. Maisha yalikuwa magumu kwangu hata katika hatua za mwanzo za maisha. Sijawahi kujua habari ya uhusiano wa baba na Mama”
Wazazi wa Lamptey waliachana wakati akiwa na miaka nane, na mwenyewe aliamua kumfuata baba yake aliyekuwa anaishi mji wa Kumasi .
“Kulikuwa na ndoa nyingine kwa baba na kitendo cha mimi kuwa pale kilikuwa tatizo. Mke wake hakunipenda. Baba yangu alizoea kunipiga lakini na mimi nikaanza kuzoea pia kupigwa na wala sikuwa nalia. Wakati mwingine angeweza kuvuita Sigara na kunichoma nayo.” Anasema Lamptey.
Mambo yalizidi kuwa magumu mpaka akaamua kuondoka zake nyumbani na kwenda sehemu ambayo alitafutiwa na klabu yake aliyokuwa akichezea wakati huo, Kaloum Stars. Hata hivyo, hilo lilizidi kumuweka pabaya kwa baba ambaye wakati huo alikuwa anatawaliwa na tabia ya ulevi.
“Walikuwa waislamu. Na kwa sababu hiyo ilibidi niwe muislamu. Ningeweza kwenda Msikitini kusali lakini baba angekuja na kuanza kunipiga”
Hata hivyo, nchi ya Scotland ndiyo iliyompa fursa ya kwanza ya maisha Lamptey kwa sababu kwa mara ya kwanza alipewa kiasi fulani kikubwa cha fedha, lakini pia alikutana na Steven Keshi, mwanasoka wa kimataifa wa Nigeria na klabu ya Anderletch ya Ubelgiji.
Keshi alimpa Lamptey kadi iliyokuwa ya maelezo ya wakala mmoja wa jiji la Lagos na kisha akamwambia kwamba kama angewasiliana vema na mtu huyo basi angeweza kumuandalia safari ya kwenda Ulaya kucheza soka la kulipwa.
Huku klabu za Rangers, Vasco da Gama na Anderletch zikiwa zimevutiwa na kile walichokiona kutoka kwa Lamptey katika michuano hiyo, Chama cha soka cha Ghana kilikuwa bado kinataka kukiweka pamoja kikosi hicho mahiri wakati timu iliporudi Ghana .
Matokeo yake FA ya Ghana iliwanyang’anya wachezaji wote hati zao za kusafiria. Hata hivyo, Lamptey akiwa amepania kuondoka zake, alitumia nafasi yake vema wakati wachezaji walipovunja kambi ya mazoezi.
“Sikumwambia mtu yoyote, hata wazazi wangu. Nilichukua kiasi kidogo cha fedha nilichokuwa nacho na na kwenda kituo cha basi ambako nilikutana na dereva aliyekuwa anakwenda Nigeria ” anasema Lamptey.
“Nilimwambia yule dereva hivi ‘ebwana hali iko hivi, mimi sina hati ya kusafiria lakini nataka kwenda Lagos ’, akasema kuwa kama ningemlipa vizuri basi angesema kuwa mimi nilikuwa mwanae”
Kuanzia hapo, Lamptey alifanikiwa kukaa nyuma ya siti ya dereva akijisingia kuwa amelala kila walipopita katika mipaka ya nchi, kutoka Ghana , kupitia Togo na kwenda Nigeria .
“Kulizuka kasheshe kubwa nchini Ghana ” anasema Lamptey. Watu wa GFA na Kaloumu Stars walikuwa wamekasirika kwa sababu walikuwa wamempoteza mchezaji wao kipenzi.
“Ilibakia kidogo wamtie mbaroni baba yangu kwa sababu walihisi kuwa alijua sehemu niliyokuwepo. Nilipowasili Ubelgiji nilimpigia simu mama yangu na nadhani alikuwa katika wodi ya wazazi. Hakujua nipo wapi. Niliwasili Lagos na kumpa kadi dereva wa Taksi ambaye alinipeleka moja kwa moja mpaka katika nyumba ya wakala. Alimpigia simu Keshi ambaye wakati huo alikuwa Ubelgiji kumwambia kwamba nilikuwa nimewasili na nilimsikia Keshi akipiga makelele ya furaha”
Tatizo kubwa lilikuwa namna ya kumtoa Lamptey nje ya Nigeria . Baada ya siku chache Keshi aliwasili Lagos kwa ajili ya kucheza pambano la kimataifa la kirafiki. Huku akisingizia kuwa Lamptey alikuwa mwanae, Keshi alifanikiwa kupata hati ya kusafiria kwa ajili ya Lamptey na wakaenda zao Ubelgiji pamoja.
“Kila mtu alimjua” anasema Lamptey akimzungumzia Keshi “Kwa hiyo ilikuwa rahisi kupita uhamiaji. Tulipofika Ubelgiji kitu cha kwanza kufanya ilikuwa ni kutupa hati yangu ya kusafiria. Mimi ni Mghana kwa hiyo tuliwapigia simu maofisa na rais wa Anderlecht . Wao ni timu kubwa kwa hiyo wana nguvu sana . Nilikwenda katika ubalozi wa Ghana na wakanipa makaratasi”
Hata hivyo, bado alikuwa na kazi ngumu ya kuthibitisha kwa klabu yake kwamba alikuwa anastahili juhudi walizomfanyia.
“Mwanzoni Anderlecht hawakuwa na uhakika kama mimi nilikuwa Lamptey ambaye walikuwa wanamtafuta. Katika Luninga walikuwa wananiona mkubwa zaidi. Walibishana sana na Keshi na wakamwambia ‘Si yeye’ lakini Keshi akawaambia ‘Ndiye yeye’. Baada ya siku mbili tatu za kupumzika nikiwa nyumbani kwa Keshi, hatimaye nikaanza mazoezi na wachezaji wengine wa umri wangu.kila mtu alikuwa pale, maofisa wa bodi na Rais. Baada ya kuugusa mpira mara mbili waligundua kuwa nilikuwa Lamptey halisi”
Alisaini mkataba wa miaka mitano na Anderlecht na kwa wakati huo kila kitu kilikwenda sawa. Lamptey alicheza mechi 14 katika msimu wa 1990-91 na alifunga mabao saba kitu ambacho kilikuwa kinadhihirisha kipaji chake.
Wakati Ghana ikitwaa michuano ya kombe la dunia chini ya miaka 17, Lamptey alitajwa kuwa mchezaji bora wa michuano akiwashinda Juan Sebastian Veron wa Argentina na Alessandro del Piero wa Italia.
Alicheza mechi yake ya kwanza kwa timu ya taifa ya wakubwa mwaka huo huo na kuanzia hapo ndipo mambo yalipoanza kwenda kombo.
“Nilikuwa natapika damu uwanjani.” Anasema Lamptey huku lawama zake akizielekeza kwa wachawi wa klabu yake ya Ghana , Kaloumu Stars ambao aliamini kuwa walikuwa wamemroga ikiwa ni adhabu yake kwa kuitoroka timu hiyo. Lakini pia kulikuwa na matatizo mengine katika timu yao .
“Hakukuwa na umoja katika kikosi cha mwaka 1992. kingeweza kushinda kombe la dunia lakini kulikuwa na mambo mengi yaliyokuwa yanaendelea. Niliwekwa matatizoni lakini niliamua kukaa kimya”.
Kuumwa, majeruhi na kushuka kwa kiwango chake kulipelekea Lamptey acheze mechi moja tu msimu wa 1992-93, lakini klabu ya PSV Eindhoven ikiwa inatafuta mchezaji wa kuziba pengo la Romario aliyeoondoka kwenda Barcelona ilikuwa imejiandaa kumchukua kwa mkopo msimu mmoja baadaye.
Msimu huo, kwa mujibu wa Lamptey mwenyewe anauelezea kama ni msimu bora katika maisha yake ya soka. Ingawa kilikuwa kipindi cha mpito wa PSV alifanikiwa kuwa mfungaji bora wa klabu akifunga mabao nane katika mechi 22 katika Ligi.
Kumbukumbu kubwa ilikuja katika pambano dhidi ya wapinzani wao Ajax ambapo alifunga mabao mawili katika ushindi wa 4-1. Hata hivyo, pamoja na kuonyesha matumaini ya kuwa staa wa baadaye, PSV iligoma kulipa kiasi cha paundi milioni nane kumnunua Lamptey kama Anderlecht walivyotaka.
Mawakala walikuwa katika mazungumzo mazito, lakini mwishowe akajikuta akiangukia katika kikosi cha Aston Villa kilichokuwa kinafundishwa na kocha Ron Atkinson mwaka 1994. mwenyewe anasema ilikuwa ni kwa mkopo ingawa mpaka leo bado haieleweki vizuri.
Katika siku yake ya kwanza Aston Villa, Atkinson alimuita chemba na kumuuliza namna anavyotaka alipwe kiasi chake cha fedha za uhamisho. Lamptey alishangaa sana . Kamwe hakuwahi kusikia chochote kuhusu kiasi cha fedha za uhamisho hapo awali. Ndipo alipofahamu kuwa kumbe wakala wake alikuwa amemdhulumu kiasi cha fedha wakati alipozichezea Anderlecht na PSV.
“Niliwapa akaunti yangu na wakaniwekea fedha moja kwa moja. Wiki mbili baadaye wakala wangu alikuja kutaka kuchukua fedha hizo. Walimwambia kuwa fedha hizo nilikuwa nimepewa mimi moja kwa moja na alionekana kuudhika sana . Alisema watu wengi walikuwa wamo ndani ya dili hilo ”
Mpaka leo, Lamptey anamshukuru sana Atkinson na alimpigia simu ya kumtia moyo wakati kocha huyo alipokumbwa na kashfa ya kutoa maneno ya kibaguzi kwa mlinzi wa zamani wa Ufaransa, Marcel Desailly katika kituo cha televisheni cha ITV.
“Big Ron alikuwa mtu mzuri sana katika maisha yangu. Amenisaidia sana na namuheshimu mno. Namjua Big Ron, angeweza kufanya kitu kama hicho lakini asimaanishe. Wakati nilipokuwa Villa kulikuwa na wachezaji weusi kama John Fashanu, Dalian Atkinson, Ugo Ehiogu, Dwight Yorke na mimi mwenyewe. Vipi kuhusu ubaguzi? Ron ni mtu mchekeshaji, anapenda utani. Labda alisema hivyo lakini hakumaanisha”
Katika kipindi chake akiwa Villa, Lamptey alihitaji msaada wa Atkinson, wakati akijaribu kujenga upya uhusiano wake na baba yake mzazi.
“Baada ya kusafiri kiasi alijua nilichotaka kwa hiyo alitulia kidogo. Baba yake alipenda kunywa pombe na hilo lilikuwa tatizo. Siku moja nilirudi nyumbani likizo nikamkuta amelewa chakari huku akiwa amezimia. Nilimchukua katika hospitali ya kulipia na wakamtibu vizuri. Madaktari walimwambia aweke ahadi kuwa hatakunywa tena. Walimwambia ‘bila ya mwanao ungekufa kwa sababu ini lako lilishapoteza nguvu”
Lamptey alikuja kufunga ndoa, lakini hilo lilileta matatizo zaidi. “Kitendo cha kukutana na mke wangu Gloria kilikuwa ni tatizo jingine. Wengi walipinga. Wazazi wangu walipinga, sijui kwa nini?”. Marafiki zake pia kutoka Kumasi walipinga suala hilo .
“Watu wote hawa walitaka nioe mtu kutoka katika familia zao. Walisema nisimuoe angeniibia fedha zangu tu. Baadaye wakaniuliza kwa nini nina haraka. Waliniambia ningeweza kumuoa mtoto wa Rais kama ningetaka”
Katika soka mambo yalianza kumuendea kombo. Lamptey alijikuta akipata wakati mgumu kuzoea soka la Kiingereza huku pia akishindwa kumudu majukumu ya timu ya taifa.
“Ron ilibidi agombane na FA ya Ghana . Nilikuwa nachezea timu ya taifa chini ya miaka 20, na pia nilikuwa nachezea timu ya chini miaka 23. unaweza kufikiria mzigo niliokuwa naubeba? Ilikuwa hatari sana .”
Atkinson alifukuzwa Villa mwaka 1994, lakini haraka haraka akachaguliwa kuwa kocha wa Coventry City . Ingawa Lamptey alikuwa ameichezea Villa mechi 10 tu, lakini Atkinson alikuwa na imani naye na akamsajili Coventry . Hata hivyo, Lamptey alikuwa karibu sana na baba yake.
“Tulikuwa karibu tena katika mwaka ambao nilichezea Coventry . Halafu akafariki dunia. Nilikuwa nimemnunulia nyumba na alikuja kuishi na mimi. Kitu kimoja alichoniambia ni kwamba alitamani niache imani ya Kiislamu na ndiyo maana niliacha. Kwa sasa mimi ni Mkristo kamili”
Kifo cha baba yake kilisababisha Lamptey ajikute katika wakati mgumu katika mahusiano na wanafamilia wenzake.
“Nilikuwa England wakati niliposikia kuwa amefariki, kwa hiyo nilirudi na ilibidi nimzike peke yangu. Sisi kina kaka hatuko pamoja. Sidhani kama ni wivu lakini huwa hatuwi pamoja. Nilikuwa na kitu mfukoni kwa hiyo kaka zangu na mama walikuwa wananitazama mimi. Unajua barani Afrika, watu wakijua una fedha wanakuachia kila kitu. Hata mama yangu nilimzika peke yangu. Nimepitia katika matatizo makubwa”
Kulikuwa na matatizo pia katika mahusiano ya Lamptey na timu ya taifa ya Ghana sana sana baada ya kutolewa nje katika pambano la nusu fainali za kombe la mataifa ya Afrika mwaka 1996.
“Katika kombe la mataifa ya Afrika kuna kitu cha kusikitisha kilitokea.” Anasema Lamptey.
Ingawa katika maongezi haya alionekana kuwa muwazi, lakini kusita kwake kuelezea kitu kilichotokea kunadhihirisha kwamba tukio hilo lilikuwa kubwa sana huku pia likimuhusisha nyota wa zamani wa Ghana na timu ya Marseille ya Ufaransa, Abeid Pele.
“Mimi na yeye si marafiki kabisa. Anajua kwa nini”
Lamptey aliichezea Coventry mechi sita tu kitu ambacho kilisababisha kibali chake cha kazi kisiongezwe muda. Aliondoka na kwenda zake Venezia. Kiwango chake kilikuwa cha hali ya chini sana . Akiwa amevunjika moyo huku akiwa anajaribu kuishi katika nchi ya nne ndani ya kipindi cha miaka minne alihamia Boca Junior huku bado akijua kwamba ulikuwa ni mkopo tu kutoka Anderlecht .
Wakati huo alikuwa anaonekana kama mchezaji wa kigeni wa tano wakati ni wachezaji wanne tu waliokuwa wanaruhusiwa. Hatimaye alipelekwa Union de Santa Fe . Ilikuwa ni wakati yupo hapo ndipo mtoto wake wa tatu alipozaliwa na kumpa jina la Diego ikiwa ni heshima yake kwa Maradona.
“Alizaliwa mwezi mmoja kabla. Madaktari walisema kuwa alikuwa hana tatizo, lakini baada ya wiki mbili tukiwa nyumbani matatizo yalianza. Kama angelia ungeweza kuona machozi tu yakitoka, lakini usingesikia kilio.” Madaktari walishangaa sana na walimwambia aende katika hospitali kubwa jijini Buenos Aries
“Ilibidi nisimame kucheza mpira na mimi na mke wangu pamoja na watoto wetu wawili ilibidi tumwangalie mtoto kwa karibu. Tulipanga katika hoteli iliyokuwa karibu na hospitali. Madaktari walifanya kila walichoweza, walichukua vipimo vyote, lakini hakuweza kupumua. Alikuwa pale kwa miezi miwili na nusu kwa hiyo alikuwa na miezi minne wakati alipofariki huku akiwa katika usimamizi wa hali ya juu” katika tukio hili, Lamptey anaamini kulikuwa na ushirikina ndani yake.
Akiwa amevunja mkataba wake, Lamptey alirudi kwanza Ghana kabla ya kwenda tena Ulaya ambako aligundua kuwa hakuwa na mkataba tena na Anderlecht . Mpaka sasa hajui kilichotokea lakini inaonekana kuwa wakala wake alikuwa amemnunua na kummiliki bila ya yeye mwenyewe kujijua.
Alifanikiwa kuvunja mikataba yote na kubaki mwenyewe ingawa mpaka sasa hajui kabisa kilichotokea wakati akihamishwa kutoka timu moja kwenda nyingine miaka ya 1990. bado hajielewi mpaka leo na ingawa ana uwezo wa kuongea lugha tisa, anajichukulia kama mtu asiyeweza kuandika walau barua tu.
Klabu ya Ankaragacu ya Uturuki ilimchukua, lakini kiwango chake bado kilikuwa chini sana . Baadaye alikwenda Uniao Leiera ya Ureno na kisha Greuther Furth ya Ujerumani. Aliichezea timu hii mechi nyingi zaidi (36) kuliko timu nyingine yoyote. Lakini janga jingine lilitokea.
Mkewe Gloria alimzaa mtoto mwingine wa kike, Lisa. “Ilikuwa ni kama mwanzo. Mtoto huyu pia alikuwa na miezi minne wakati alipofariki.” Hakutaka kujihatarisha kutafuta mtoto mwingine, lakini Gloria alimshawishi na sasa ana mtoto mwingine wa kike ambaye atatimiza miaka minne mwaka huu.
Lamptey alikwenda Dubai na China akijaribu kuendelea kutafuta maajabu yake ya soka la utotoni bila ya mafanikio. Mwishowe alirudi nyumbani kuichezea timu ya Asante Kotoko ya Kumasi .
“Niliamua kurudi nyumbani na kusajili katika timu moja ambako nilicheza kwa miezi sita kwa ajili ya kutengeneza CV yangu tu. Nilitaka kufanya hivyo. Nilikuwa niko sawa pale, lakini kama unavyowajua Waghana, siku zote matazamio yao yako juu. Mengi yalisemwa. Walisema nilikuwa nafanya hivyo kwa sababu nilikuwa nataka kurudi katika timu ya taifa.”
Kotoko ilichukua ubingwa wa Ligi na Lamptey akaamua kujiunga na klabu ya Jomo Cosmos ya Afrika Kusini. Mwishowe aliamua kuachana na soka baada ya kusmbuliwa na goti lake.
Alikuwa na miaka 31 na kama angeweza kufanya vitu vyake basi ingekuwa rahisi tu kwake kuichezea timu ya taifa ya Ghana katika kombe la dunia.
“Majuto?, najua kama watu wangeachana na mimi, kama Mungu alivyoniumba, sasa hivi ningekuwa nachezea Real Madrid. Lakini watu walitaka nianguke. Mambo mengi…..”
Mapema mwaka huu, Lamptey alirudi katika soka kama kocha msaidizi wa Eleven wise Men . Maumivu ya mchezo wa soka bado anayo na fikra za angekuwa nani kama angefanikiwa bado ziko katika kichwa chake.
“Wakati mwingine nitakuwa katika chumba changu na nitalia. Unajiona kwamba kuna kitu unaweza kufanya lakini kitu hicho kimechukuliwa kutoka kwako. Inauma sana . Lakini utafanya nini? Kuna uchawi katika soka.
“Nakumbuka nilikuwa Kumasi wakati nilipokutana na mke wangu, watu fulani, Waislamu ambao nilikuwa nasali nao walikuwa wanawaambia watu ‘Tutaona kama ataichezea timu ya taifa tena’. Na imekuwa kweli. Tangu mwaka 1996 sijaichezea Ghana na labda, labda, labda haikuwa sehemu yangu”.
Badala yake anaamini kuwa labda sehemu yake ilikuwa kuendesha shule yake na kuwapa elimu vijana wa Ghana ambayo yeye alinyimwa

3 comments:

  1. Hatari sana kaka...AFRICA MISUMARI ASILI KUMBE...Hatari sana kaka...AFRICA MISUMARI ASILI KUMBE...

    ReplyDelete
  2. Dah sad sad story...imenikumbusha mbali sana aisee...ni vizuri tumesikia kwake mwenyewe, otherwise, dunia nzima ilishindwa jua nini haswa kilimkuta Mii Lamptey! Kuna dogo mwingine wa Ghana, naye alianza kwa cheche kibao, Dereck Boateng, siavi mtu mzima (hata AFCON 2012 ya uzi alikuwepo, na dreads), naye alishindwa kabisa kurealise his full potential, kama vipi naye tupe story yake. Shukrani!

    ReplyDelete
  3. Alipokuja Abeid Pele hapa Tanzania nilitaka kumuuliza kuhusu huyu kijana lakini sikupata nafasi hiyo.

    ReplyDelete