Search This Blog

Saturday, August 6, 2011

MAMELODI: BOTSWANA INAPIGA HATUA BAADA YA KUWEKEZA KATIKA SOKA LA VIJANA


ASHFORD Mamelodi ni Ofisa Maendeleo wa FIFA kwenye Kanda ya Kusini mwa bara la Afrika. Nilikutana naye tukazungumza mambo mengi yanayohusu mchezo wa soka na namna unavyowezeshwa na FIFA, Serikali na shirikisho la soka la nchi husika. Mazungumzo yetu yalikuwa hivi:

Ashford wewe unatoka Botswana tungependa utufahamishe jinsi ligi ya huko inavyoendeshwa.
Ashford: Ligi ya Botswana bado sio ya kulipwa lakini lengo ni kujaribu na kuifanya iwe hivyo. Cha ziada ni kwamba ni ligi huru ambapo klabu zinaendesha ligi zenyewe na zinasaidiwa na shirikisho la soka kwenye mambo ya kiutendaji.

Klabu zinaendeshaje ligi zenyewe?
Kwa kila namna, zinatafuta wadhamini zenyewe, zinapanga ratiba zenyewe, kanuni na taratibu za mashindano; na sio vilabu vyote, vilabu vimejiwekea utaratibu ambapo ligi inaongozwa katika utaratibu unaoeleweka, kikubwa ni kwamba vilabu vinajengewa uwezo ambapo vyote vinapaswa kuwa vinajitegemea .

Kwa kutazama jinsi michuano ya kufuzu kwa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, timu ya taifa ya Botswana iko kwenye nafasi nzuri na hii inaonyesha mmepiga hatua kisoka.
Naweza kusema kuwa Botswana imeendelea sana baada ya kuwa tumewekeza kwa vijana kwa miaka mingi. Nakumbuka kuwa tulimleta jamaa mmoja toka Ghana ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Ufundi na katika kipindi hiki kulikuwa na mipango ya makusudi kabisa ya kuendeleza vipaji vichanga, kuwaendeleza makocha na mipango mingine mingi thabiti ambayo naweza kusema imesaidia sana.

Kwa hapa Tanzania tuna Mkururgenzi wa Ufundi ambaye machoni kwa wengi hafanyi wajibu wake ipasavyo, je, kwenu Botswana Mkurugenzi wa Ufundi ana majukumu gani?

Majukumu ya Mkurugenzi wa Ufundi ni rahisi sana; nayo ni kutekeleza mipango ya maendeleo; maendeleo ya soka kwa upande wa vijana, soka la wanawake na pia maendeleo ya makocha na anapaswa kuzingatia eneo hilo tu na si vinginevyo. Anahusika na kuunda au kubuni mifumo ambayo timu za taifa zitafaidika na jinsi wachezaji wapya wanavyopatikana lakini hiyo haimaanishi kuwa anahusika moja kwa moja na timu za taifa. Hiyo ni kwa sababu timu za taifa ni taasisi huru ambazo zinajiendesha zenyewe na makocha wake .

Wewe ni Ofisa Maendeleo wa FIFA, kuna huu mradi wa GOAL, unaweza kutueleza kuwa huu ni mradi gani?
Mradi wa GOAL ni moja ya mambo mengi ambayo yanafanywa na FIFA, GOAL ni mradi ambao FIFA imeuanzisha makusudi kabisa ili kuendeleza mchezo wa mpira wa miguu sehemu mbalimbali ulimwenguni. Kwa mfano kuanzia mwaka jana FIFA imekuwa ikitoa miundombinu mbalimbali kama vile fedha taslimu Dola Laki Tano, ambazo kama shirikisho husika la nchi wanapaswa watoe maelezo juu ya matumizi ya fedha na miundombinu ambayo inatolewa na FIFA pamoja na kuonyesha jinsi nchi iliyopewa msaada inavyofaidika na miundombinu ya FIFA.

Je, nchi yako Botswana imefaidika kwa chochote kile na huu mradi wa GOAL.
Kabisa, kabisa. Botswana hivi tunavyozungumza imekamilisha kituo cha ufundi ambacho kina sehemu kama vile ofisi, sehemu kwa ajili ya masuala ya ufundi na tulikuwa na bahati kwa sababu kwenye mradi wa mwanzoni FIFA ilitoa Dola laki Nne ambazo serikali iliongeza fedha nyingine kiasi hicho na kufanya kiasi kuwa Dola laki Nane ambazo Botswana imefaidika nazo sana. Pamoja na fedha, serikali pia ilitoa ardhi ambayo ndio ilitumika kujengea jengo ambalo ndio makao makuu ya BFA yalipo, kumbi za mikutano pamoja na kituo ambacho kina viwanja pamoja na sehemu za kulala. Na kwenye mradi wa pili BFA ilijenga jengo ambalo liko kama hoteli ya kitalii ambalo linaweza kutumika hata na timu ya taifa pale inapoweka kambi.
Kwenye swali la awali ulitueleza kuwa mradi wa GOAL ni moja kati ya miradi mingi, unaweza kutueleza chochote kuhusu miradi mingine pembeni na huo?
Kuna maafisa 12 wa maendeleo ya soka ulimwenguni kote na wote hawa wana eneo la kijiografia ambalo wanafanya kazi na sisi ni mawakala wa FIFA linapokuja suala la maendeleo na hii inamaanisha kuwa pale ambapo FIFA inataka kuingilia kati mradi wa maendeleo kwa kawaida inakuwa jukumu letu kuhakikisha mradi huu unasimama. Kazi yetu ni kuhakikisha kuwa misaada yote inakuwa sawa pamoja na miundo mbinu yote inayohusika. Kwa ujumla tuna jukumu la kusaidia vyama husika vya soka kuendeleza mchezo huu lakini vyama ndio vinakuwa mstari wa mbele, vinatakiwa kuwa na falsafa ambayo inalenga kwenda mbele na sisi tunakuja kama wasaidizi wawezeshaji.

Kombe la Dunia lililochezwa Afrika Kusini mwaka jana lilikuwa kama baraka kwa mchezo wa soka barani Afrika, nchi yako Botswana imefaidika vipi na Kombe la Dunia la kwanza barani Afrika?
Ashford: Ni vigumu kueleza moja kwa moja jinsi nchi ilivyofaidika lakini nadhani kwa Waafrika wote ambao walikuwepo watashuhudia kuwa kila Mwafrika alifaidika na Kombe la Dunia lakini kwa upande wa FIFA tulikuwa na kaulimbiu ambayo inasema ‘WIN IN AFRICA WITH AFRICA’ yaani ‘SHINDA AFRIKA NA AFRIKA’ ambapo FIFA ilitenga kitita cha fedha kiasi cha Dola milioni 7 za Kimarekani ambazo zilililega kuendeleza soka barani Afrika baada ya Kombe la Dunia kwa kuwa hili ni Kombe la Dunia la kwanza Afrika na wazo lilikuwa kuacha kumbukumbu ya tukio hili. Fedha hizi zilitumika katika vitu mbalimbali kwa mfano viwanja ambapo kila moja kati ya nchi 53 za Afrika zilisaidiwa kuendeleza viwanja husika ambapo kila kiwanja kiligharimu Dola Laki Saba. Hii ilikuwa moja; pia tulikuwa na issue ya uongozi wa vilabu, tumefanya semina mbalimbali ambapo tuliweka azimio ambapo tumemua kuwa ni lazima ligi mbalimbali barani Afrika ziendeshwe kwa mfumo wa professional. Kimsingi ni kwamba fedha hizi ni nyingi sana na bara la Afrika limefaidika na fedha hizi na Kombe la Dunia kwa ujumla.

FIFA wana sera ambayo inapiga marufuku serikali kuingilia masuala ya soka, sera ambayo imekuwa ngumu kidogo kwa Afrika kuzingatia, vipi kwa Botswana imekuwa vigumu kama sehemu zingine au imekuwaje?

Ashford: Bostwana wamejitahidi sana kuzingatia kanuni hii na FIFA haina huruma katika suala hili, kumbuka kuwa serikali si mwanachama wa FIFA, mwanachama ni shirikisho ama chama, tumejaribu kuhakikisha kuwa shirikisho liko huru kujiendesha lenyewe kwa uhuru, japo kwetu serikali ni mdau mkubwa wa masuala ya michezo, hivyo ule mwingiliano ambao ni wa hasi, yaani mzuri haukatazwi lakini si mwingiliano chanya, huo ndio FIFA inaupinga.

Unazungumziaje mchango wa rais wa FIFA Sepp Blatter kwa mchezo wa soka barani Afrika.
Sepp Blatter amekuwa na baraka kwa soka letu, amekuwa msaada mkubwa sana, kumbuka kuwa haya maendeleo yote tunayozungumza, ‘goal project’ na mengineyo ni mawazo yake, ni yeye aliyeanzisha, ametuunga mkono sana, ni yeye alihakikisha kuwa Kombe la Dunia linakuja Afrika kwa mara ya kwanza na bado anaendelea, nadhani tuna deni la shukrani kwa mtu huyu kusema kweli.

No comments:

Post a Comment