Search This Blog

Wednesday, August 24, 2011

AZAM FC NA MATARAJIO MAKUBWA YASIYO RAHISI KUYAFIKIA..

Mojawapo ya vivutio ambavyo mashabiki na wadau wa soka la Tanzania walikuwa wanavingoja kwa hamu kubwa ni kutazama ujio mpya wa klabu ambayo imetokea kuleta mapinduzi kama si mageuzi kwenye soka la Tanzania , nao si wengine bali ni Azam Fc.

Wakati wa ‘Pre-season’ ya hapa Bongo Azam walifunga safari hadi magharibi mwa Afrika ambako walisajili ‘nyota’ kadhaa kama Kipre Tchetche , Wahab Yahya na Nafiu Awudu wakitokea nchi za Cote d’Voire na Ghana .

Kana kwamba hiyo haitoshi wakamsajili kipa toka Serbia Obren Curkovic japo huyu anafahamika kwani ameshawahi kuicheza Yanga.

Kwa hali ya kawaida kwenye mchezo wa Soka ‘A proffessional player’ kabla ya sifa yoyote ile anapaswa kuwa na kitu cha ziada ambacho kinakosekana kwa wachezaji wazawa.
Watu wengi walikuwa na matumaini makubwa juu ya uwezo wa Wachezaji waliosajiliwa na Azam toka nje ya nchi, lakini baada ya michezo miwili ya ligi kuu ya Vodacom wachezaji hawa wanaonekana kuwa wa kawaida mno na kushindwa kuiongoza Azam kupata matokeo mazuri mwanzoni mwa msimu.
Kwa michezo miwili ambayo Azam imeshacheza kwenye ligi ya Vodacom wameshinda bao 1-0 dhidi ya Moro United na kupoteza mchezo wa pili dhidi ya African Lyon kwa bao 1-0.

BLOG yako imejaribu kuangalia baadhi ya vitu vilivyosababisha timu hii kupata ushindi wa taabu dhidi ya Moro Utd,kufungwa na African Lyon na pia kuangalia baadhi ya mambo ambayo yanaweza kuwazuia kufikia malengo yao ya kuchukua ubingwa wa Ligi kuu ya Vodacom msimu huu.



SALEMBE ANACHEZA KWA MKOPO AFRIKAN LYON AKITOKEA AZAM FC


1. Suleiman Kassim Salembe na Sino Agostino
Azam ilikuwa na wachezaji kadhaa ambao wana vipaji halisi na kwa hali ya kawaida kama klabu ambayo inakuwa na malengo ya kufika mbali walipaswa kuendelezwa ili wakue sambamba na klabu .



Mfano mzuri ni Suleiman Kassim Salembe na Sino Agostino ambao wamekuwa na Azam tangu msimu uliopita na Salembe alifikia mpaka kuitwa kwenye timu ya taifa , cha kushangazwa ni kwamba wachezaji hawa wametolewa kwa mkopo ili kupisha wachezaji wengine baada ya kuonekana kuwa hawana nafasi .



Wachezaji hawa wamepelekwa African Lyon . Kwa bahati nzuri waliruhusiwa kucheza dhidi ya Azam na ‘perfomance’ waliyoionyesha haiwezi kumuingia mtu akilini kuwa hawa jamaa wameonekana hawana nafasi .



Sino Agostino alitoa pasi ya goli lililoiua Azam , unasemaje kuwa mtu huyu hana nafasi kwenye timu yako?Walichofanya Salembe na Sino ni kama alichofanya Fernando Morientes wakati alipotupiwa virago na Real Madrid na akaja kuwaua akiwa na klabu ya Monaco .Katika hali ya kawaida wachezaji wanaokuwa kwenye mkopo



2. kuwa ‘over-ambitious’



Moja ya vitu ambavyo Azam imevifanya kama kosa kubwa ambalo hakuna mtu aliyeliona ni kuwa ‘over-ambitious’. Hakuna mtu anayekatazwa kuwa na malengo kwani hata binadamu amewahi kufika mwezini , ni kwa sababu ya kuwa na malengo lakini malengo haya yanapaswa kuwa na ukweli unaoonekana . Azam wana miaka mitatu kwenye ligi ya Vodacom , ni vyema wangekuwa wanajijenga taratibu pasipo kuwa na papara.



Ujenzi unaanzia chini na si juu na vile vile kabla mtoto hajatembea huanza kwa kutambaa, inawezekana kuwa Manchester CITY wameweza kucheza Champions League kwenye miaka mitatu ya umiliki wa Sheikh Mansour lakini hiyo ni England na hapa ni Tanzania.Kuna misingi mingi ambayo Azam imeiruka na mojawapo ni kutowapa nafasi wachezaji wadogo ambao kiukweli kutokana na usajili ambao Azam imeufanya wanakosa nafasi .






3. Usajili haukuzingatia wachezaji kuwa na sifa tofauti…matokeo yake wanajikuta wana kikosi kikubwa sana.

Usajili wa Azam haukuzungatia wachezaji kuwa na sifa tofauti . Siku zote timu inapaswa ‘kubalance’, yaani kama kuna wachezaji wenye sifa ‘x’ lazima wawepo wenye sifa ‘Y’.



Azam kuna viungo kama Jabir Aziz, Ramadhan Chombo , Khamis Mcha, Abdulhalim Humoud, Ibrahim mwaipopo,Jamal Mnyate,gullam Abdallah,Himid Mao na wengineo wengi ambao ukiwatazama wana sifa zinazofana, unapata picha kuwa suala la ufundi halikuzingatiwa hapa.



Unategemea nini kuwachezesha kikosi kimoja nafasi ya kungo Ramadhan Chombo,Mrisho Ngassa,Salum Abubakar na Jabir Aziz ?
Kila mmoja wao mpira ulipokuwa kwenye imaya yake ilikuwa ni lazima akae nao sekunde kadhaa, kama ilikuwa ni mbinu ya timu kuwatumia wote ili kumiliki mpira basi ilishindikana.



Kwenye mchezo dhidi ya African Lyon moja kati ya sababu iliyowakaba na kuwanyima fursa ya kutengeneza nafasi nyingi ilikuwa ni kila mmoja wao kutaka ku-dribble kwanza hata katika wakati ambao ilitakiwa ipigwe pasi moja moja.



Zaidi ya hapo Azam inajikuta kuwa na kikosi kikubwa sana ambacho mwisho wa siku kitakuwa kinapotea chenyewe bila kujua ni ipi timu ya kwanza na ipi timu ya pili na badala yake wanaweza kujikuta wakijaribu msimu mzima wa ligi wasipokuwa makini .

4. Kuwachezesha wachezaji kwenye nafasi zisizokuwa zao..



Mojawapo ya hasara za kuwa na kikosi kipana kuliko mahitaji ya kawaida ni hali inayotokea sasa Azam, Kipre Tchethe ni mshambuliaji kiasili lakini kwa kuwa Azam tayari wana John Bocco, Kipre Tchetche analazimika kuchezeshwa kama winga . Matokeo yake anashindwa kuperfom kwa kuwa hayuko ‘comfortable’ na ataonekana hana mchango kwa timu yake.
Kipre Tchetche anaweza kucheza vizuri akiwa kama ‘Second Striker ‘yaani nyuma ya Bocco,
Nakumbuka kwenye mashindano ya CECAFA Challenge Cup akiwa na kikosi cha Ivory Coast maara nyingi alikuwa akiingia akitokea benchi na kwenda kufunga, alikuwa mara nyingi anacheza ‘shimoni’ na kusubiria mipira inayozagaa zagaa kwenye eneo la nje ya penalty kwasababu ana uwezo mkubwa wa kupiga mashuti na kutoa pasi za mwisho pia,


5. Kutokuwa na aina ya watu kama Habib Kondo na Herry Mzozo..



Kabla ya kumalizika msimu uliopita Azam Fc walifanya mabadiliko makubwa kwenye benchi lao la ufundi. Mabadiliko hayo yalikuwa kuwaondoa aliyekuwa kocha msaidizi Habib Kondo na aliyekuwa kocha/msimamizi wa timu za vijana za Azam Herry Mzozo.



Watu hawa waliondolewa na kwenye nafasi ya msaidizi wa mwalimu aliwekwa Kali Ongara. Kali ana uzoefu mkubwa sana kama mwanasoka na ametembea na kufika sehemu nyingi ambazo wachezaji wengi wa nchi hii hawajafika,
Lakini ana ufahamu mdogo sana wa soka la hapa bongo.



Amekulia kwenye mazingira tofauti na waliyokulia wachezaji wengi wa Tanzania , japo alicheza Abajalo ya Sinza na Yanga lakini ukweli unabaki pale pale Kali hajakaa kwa ukaribu na wachezaji wa kitanzania na pia ufahamu wake wa soka la Bongo ni mdogo, hivyo hata kama amepewa nafasi ya kuwa msaidizi wa moja kwa mmoja wa Stewart Hall umuhimu wa aina ya watu kama Kondo na Mzozo unabaki pale pale.



Watu hawa wanaweza kuwa hawana ufahamu mkubwa wa mambo ya kiufundi lakini wana ufahamu na mazingira ya soka la hapa , kuwajua wachezaji wanaocheza soka la hapa kitu ambacho ni muhimu sana kwa Stewart Hall na Kally Ongara .
Ni vyema Azam wakatambua kuwa hapa ni Tanzania na si England , mambo ambayo Azam wanajaribu kuyafanya ni kama kuyakimbia mazingira yanayowazunguka .



Kitakachowaangusha ni kushindwa kwenye masuala madogo ya soka la hapa Tanzania kwa kuwa inaonekana kwa sasa wamewekeza akili na nguvu nyingi kwenye vitu vinavyohitaji nguvu chache na akili za kawaida.



Hakuna anayeiombea timu hii mabaya kwani imeonyesha nia thabiti ya kutaka kulipeleka soka la nchi hii mbele lakini ni vyema mawazo sahihi yakafanyiwa kazi na si kufanya vitu kwa sifa na mwisho wa siku vikashindwa kufanikiwa, itakuwa hali ya kuvunja moyo sana.


3 comments:

  1. Duuh! somo zuri sana hili kwa Azam fc,i wish sterwatt hall angekuwa anajua kiswahili asome hapa ingemsaidia sana brother shaffih.Duuh! somo zuri sana hili kwa Azam fc,i wish sterwatt hall angekuwa anajua kiswahili asome hapa ingemsaidia sana brother shaffih.

    ReplyDelete
  2. Ushauri huu ulitakiwa utolewe kabla ligi haijaanza, hakika suala la Solembe mm nilishangazwa nalo sana.

    ReplyDelete