Search This Blog

Thursday, July 7, 2011

WASHAMBULIAJI WAKALI AMBAO HAWAJAWAHI KUTOKEA TANZANIA



1970-1976
Tukiangalia kwa makini historia ya soka la Tanzania kuanzia mwaka 1970 hadi 1976 inaelezwa ndiko walipokuwapo washambuliaji wakali walioweza kufanya vema katika timu zao na ile ya Taifa, hao wanaongozwa na Gibson Sembuli, Adam Sabu, Kitwana Manara, Abdallah Kibaden, Jumanne Hassan ‘Masimenti’ na wengine ambao waliweza kutoa changamoto ya soka nchini.

Hawa waliweza kufanya vizuri kutokana na vitu vingi, ikiwemo utayari wao kwa mchezo wa soka. Pia ni kipindi ambacho wachezaji walipatikana kutoka mashuleni na mitaani.

Kwa mfano Sembuli aliweza kufanya vizuri kutokana na uwezo binafsi wa kumiliki mpira, kutekeleza kile alichokuwa anaelezwa na kocha kila wakati awapo uwanjani, mwili uliojengeka vema kimichezo kuweza kuhimili shuruba za mabeki wakorofi.

Sembuli anaelezwa kuwa, alikuwa na uwezo wa kukaa na mpira kwa muda mrefu zaidi na kuleta madhara langoni kwa adui wakati wowote awapo uwanjani.

Lakini yatasemwa yote kuhusu washambuliaji wa wakati ule, kubwa zaidi ni akili yao kuzama katika soka zaidi kuliko jambo jingine lolote. Hiki ni kitu pekee kinachoweza kumfanya mchezaji kuwa katika kiwango chake wakati wote.

Kati ya wote aliokuwa akicheza nao wakati huo, Sembuli anatajwa kuwa mshambuliaji bora wa ‘enzi’ zake akiwaacha kina Manara, Kibaden na Masimenti.




1977-1982
Hiki ndicho kipindi zilipochomoza timu nyingi za maeneo yaliyohamasika kisoka kama Coastal Union, African Sports, Mseto na nyinginezo ambazo zilikuwa na wachezaji mahiri walioweza kutandaza vema kabumbu.

Miongoni mwa wachezaji hao ni Mohamed Salim (Coastal), Thuwen Ally (Simba), Peter Tino (African Sports), Omar Hussein (Mseto-Yanga), George Kulagwa, Rashid Hanzuruni na wengineo.

Ndani ya kipindi hiki timu zilizoweza kutoa wachezaji wengi kwa timu ya taifa ni Simba na Pan African pekee. Ikumbukwe kuwa, Pan ilipata uhai baada ya baadhi ya wachezaji kujiengua kutoka Yanga na kuunda timu hiyo.






1982-1985
Baada ya Tanzania kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1980, wachezaji wengi kwa ridhaa yao waliachana na soka, hivyo kutoa nafasi kwa wanasoka wengine kujitokeza katika timu mbalimbali.

Miongoni mwa nyota wapya waliojitokeza ni Innocent Haule, Madaraka Selemani, Makumbi Juma, Richard Lumumba, Juma Mgunda, Zamoyoni Mogela, Gebo Peter, Malota Soma bila ya kumsahau mchezaji aliyekuwa kinda wakati huo Edward Chumila ‘Edo Boy’.

Kizazi hiki kinaelezwa kupokea vema kijiti kutoka kwa kaka zao wa 1977-1982, nguvu ya kampuni na mashirika mbalimbali ya umma iliweza kuwafanya waonekane bora katika soka wakati huo.

Katika kipindi hiki, unaweza kukumbuka jinsi kina Edo Boy walivyoweza kuinusuru Simba isishuke daraja baada ya kuwa katika hali mbaya kufuatia kufanya vibaya kwenye Ligi Daraja la Kwanza—Tanzania Bara.

Hiki ni kipindi ambacho wachezaji hawakuwa na shaka juu ya maisha yao kwani fedha kutoka katika mashirika waliyochezea ziliweza kuwainua kimaisha; pia hakukuwapo na tamaa ya fedha miongoni mwao bila kuwajibika kwanza.

Ni kipindi ambacho, timu kama Majimaji, Pamba, Coastal Union na African Sports ziliweza kuchomoza.




EDIBILY LUNYAMILA AKIWA NA MOHAMED HUSSEIN.


1985-1991
Ndani ya kipindi hiki hakukuwapo na wachezaji wengi sana waliojitokeza, zaidi ya wale waliovuma katika kipindi cha 1982-1985 kuendelea kusakata soka, lakini kwa kiasi kikubwa utawala wa Simba na Yanga katika soka uliweza kupungua kidogo.

Timu za Majimaji, Pamba, African Sports, CDA, Tukuyu Stars, Bandari na nyinginezo ziliweza kufanya vizuri katika ligi na kuonyesha msisimko mpya, lakini nyingi ya timu hizo zikipata msaada mkubwa kutoka kwa mashirika yaliyokuwa yakizimiliki.

1991 – sasa
Hiki ndicho kizazi asilia cha soka; kimeweza kupotea na kutuletea wachezaji wachache ambao mpaka leo wangali wanajaribiwa kuweza kuwa na mshambuliaji wa kuisaidia nchi.

Mwanzoni mwa 1991, wakongwe kama Mogela, Madaraka na Edo Boy waliweza kushirikiana na chipukizi kama Nteze John, Edibily Lunyamila, Thomas Kipese, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’, Dua Said, Said Sued ‘Scud’, Mao Mkami, Fumo Felician, Kitwana Suleiman, Beya Simba na wengineo kuleta changamoto katika nafasi za ushambuliaji miongoni mwa timu zao, lakini hali haikuwa kama zamani.

Baadaye kidogo kikaja kizazi cha kina Maalim Saleh, Nonda Shaaban ‘Papii’, Clement Kahabuka, Bitta John, Victor Bambo na wengineo ambao walionekana kama watu wa kupita wasiokuwa na malengo ya kufika; badala yake wakaendelea kutoa nafasi kwa kina Lunyamila, Madaraka, Nteze, Edo Boy na wengine kuendelea kutamba.

Baadaye kidogo kikaja kizazi cha kina Athuman Machupa, Athuman Macheppe, Emmanuel Gabriel, Abdallah Juma, Monja Liseki, Akida Makunda, Steven Mapunda ‘Garincha’ na baadhi yao kidogo, lakini hawakuweza kufikia uwezo na kasi ya kina Sembuli, Mogela na hata Mohamed Salim.

Ikumbukwe ya kuwa hicho ndicho kipindi ambacho wafanyabishara walijitokeza kwa wingi kudhamini timu mbalimbali ili ziweze kufanya vizuri, bado baadhi ya wachezaji wa wakati huo wangali wanacheza soka hadi leo hii.

No comments:

Post a Comment