Search This Blog

Friday, June 10, 2011

MICHUANO YA COPA COCA COLA 2011





TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Juni 10, 2011

MICHUANO YA COPA COCA COLA 2011
Msimu wa Tano wa michuano ya Copa Coca Cola kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 unaanza kesho (Juni 11 mwaka huu) katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani katika viwanja vinne tofauti.

Uzinduzi rasmi wa michuano hiyo utafanywa saa 8 mchana kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Emmanuel Nchimbi. Mikoa yote 28 ya Tanzania Bara na Visiwani inashiriki katika michuano ya mwaka huu.

Mechi maalumu ya uzinduzi itakuwa kati ya bingwa mtetezi Kinondoni na Dodoma na itaanza saa 10 jioni. Viwanja vitakavyotumika katika mashindano hayo ni Tamco na Nyumbu vya Mkoa wa Pwani, na Karume na Tanganyika Packers (Kawe) vya Mkoa wa Dar es Salaam.

Siku hiyo ya uzinduzi pia kutakuwa na mechi kati ya Temeke na Ilala itakayofanyika Uwanja wa Tanganyika Packers, Kigoma itapambana na Pwani kwenye Uwanja wa Nyumbu wakati Mjini Magharibi itaoneshana kazi na Morogoro katika Uwanja wa Tamco. Mechi hizo zitachezwa saa 2.30 asubuhi.

Ukiondoa mechi hizo rasmi za ufunguzi, kila siku kutakuwa na mechi mbili kwenye viwanja vyote. Mechi ya kwanza itaanza saa 2.30 asubuhi wakati ya pili itachezwa saa 10 jioni.

Hatua ya awali inachezwa katika makundi manne ya timu saba saba ambapo nne za kwanza katika kila kundi ndizo zitakazoingia hatua ya 16 bora.

Fainali itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati waamuzi 20 ambao wana umri chini ya miaka 17 wakiwemo wasichana wawili ndiyo watakaochezesha michuano hiyo.

Boniface Wambura

No comments:

Post a Comment