Search This Blog

Thursday, June 9, 2011

Kiko wapi kikosi cha Stars kilichonyakuwa Kombe la Chalenji mwaka 1974:

OMARI MAHADHI AKIOKOA MCHOMO GOLINI KWAKE.




“Kikosi cha Taifa Stars kilichotwaa Kombe la Chalenji kwa mwaka huo 1974 kilikuwa ni, golini alikuwa ni Omari Mahadhi (marehemu), beki wa kulia alicheza Zaharani Makame, beki wa kushoto alicheza Mohamed Chuma (marehemu), namba nne alicheza Salim Amir, wakati sentahafu alisimama Mohamed Bakari ‘Tall’ na namba sita alicheza Jella Mtagwa.
“Namba saba alicheza Godfrey Nguruko ambaye baadaye kipindi cha pili alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Shiwa Lyambiko, namba nane alicheza Sunday Manara ‘Computer’, wakati sentafowadi alisimama Mwinda Ramadhani, namba kumi alicheza Gibson Sembuli na kumi na moja alicheza Lucas Nkondola.
KIKOSI CHA TAIFA STARS KILICHOTWAA KOMBE LA
CHALENJI MWAKA 1974:
1.Omari Mahadhi
2.Zaharani Makame
3.Mohamed Chuma
4.Salim Amir
5.Mohamed Bakari ‘Tall’
6.Jella Mtagwa
7.Godfrey Nguruko/Shiwa Lyambiko
8.Sunday Manara
9.Mwinda Ramadhani
10.Gibson Sembuli
11.Lucas Nkondola.
1.OMARI MAHADHI:
Alikuwa ni kipa mahiri na wakutumainiwa wa timu ya Taifa Stars katika miaka ya 1970 katikati mpaka miaka ya 1980 mwanzoni. Licha ya kuwa na umbo la kawaida, lakini alikuwa hodari mno awapo golini na kutokana na umahiri aliokuwanao ilikuwa sio rahisi kufungwa bao kirahisi.
Mahadhi alichaguliwa kuchezea Taifa Stars akitokea klabu ya African Sports ya Tanga. Pamoja na kuichezea klabu ya African Sports, pia ameichezea kwa mafanikio makubwa klabu ya Simba SC na alikuwa langoni katika kikosi cha Simba cha mwaka 1977 kilichoifunga Yanga mabao 6-0.
Baada ya kustaafu kucheza soka la ushindani miaka ya themanini alijishughulisha na kazi ya ukocha akifundisha baadhi ya timu zikiwemo Simba SC na Waziri mkuu FC ya Dodoma. Kwa hivi sasa hatunaye tena, kwani amefariki dunia katika miaka ya 1980 mwishoni.
2. ZAHARANI MAKAME:
Makame alikuwa beki mahiri aliyemudu kucheza vyema nafasi ya ulinzi namba mbili. Alichaguliwa kujiunga na timu ya Taifa Stars mwaka 1974 akitokea klabu ya Coastal Union ya Tanga ambayo ilikuwa daraja la kwanza wakati huo.
Pamoja na kuichezea timu ya Taifa Stars na Coastal Union kwa mafanikio makubwa, pia ameichezea timu ya mkoa wa Tanga. Kwa hivi sasa inasemekana Makame anaishi Tanga.
3. MOHAMED CHUMA:
Unapotaja mabeki mahiri waliowahi kuichezea timu ya Taifa Stars sio rahisi kusahau kulitaja jina la beki mahiri na shupavu Mohamed Chuma, kwani mlinzi huyo ameichezea timu ya Taifa Stars kwa kipindi kirefu kuliko walinzi wengine wote.
Umahiri wa mlinzi huyu ambaye alikuwa anamudu kucheza vyema nafasi ya ulinzi wa namba tatu ulitokana na aina ya uchezaji wake, kwanialikuwa anacheza kwa kujituma, asiyekata tamaa na ilkuwa sio rahisi kwa washambuliaji kumpita kirahisi.
Chuma alichaguliwa kujiunga na timu ya Taifa Stars akitokea klabu ya Nyota FC ya Mtwara. Pamoja na kichezea timu ya Taifa Stars kwa kipindi kirefu, Chuma alimudu kuichezea klabu yake ya Nyota Afrika FC ya Mtwara mpaka alipostaafu soka la ushindani katika miaka ya 1980 mwanzoni. Kwa hivi sasa hatunaye tena Chuma, kwani amefariki dunia mwaka 1984.
4. SALIM AMIR:
Amir naye kama alivyokuwa Chuma alikuwa ni beki mahiri wa timu ya Taifa Stars miaka ya 1970 katikati aliyemudu kucheza vyema nafasi ya ulinzi namba nne.
Amir alichaguliwa kuichezea timu ya Taifa Stars akitokea klabu ya Coastal Union ya Tanga. Amir alikuwa anatumia akili sana awapo uwanjani hali iliyowafanya washambuliaji wa timu pinzani aliokuwa akikabiliana nao kupata wakati mgumu kumpita. Kwa hivi sasa Salim Amir inasemekana anaishi Tanga akijishughulisha na shughuli zake binafsi.
5. MOHAMED BAKARI `TALL`:
Bakari alikuwa ni mmoja wa mabeki wa kati wa kutegemewa wa timu ya Taifa Stars katika miaka hiyo ya 1970 katikati. Bakari alichaguliwa kuchezea timu ya Taifa Stars akitokea klabu ya Cosmopolitan FC ya Jijini Dar es Salaam iliyokuwa moja ya klabu kubwa Jijini Dar es Salaam wakati huo ukiondoa klabu za Simba na Yanga.
Pamoja na kuvuma akiwa na timu ya Taifa Stars na Cosmopolitan FC, pia katika vipindi tofauti vya nyuma ameichezea klabu ya Simba SC, timu ya mkoa wa Dar es Salaam maarufu kama Mzizima United na timu ya Taifa ya Vijana.Kutokana na umbo lake la urefu alilokuwa nalo na kumudu kucheza vyema nafasi ya ulinzi wa kati na kuwa kikwazo kikubwa kwa washambuliaji wa timu pinzani alizokuwa akikabiliana nazo wapenzi wa soka nchini walimbatiza jina la ‘Tall’.Kwa hivi sasa Bakari ni mkufunzi wa michezo na ni mkuu wa kitengo cha michezo katika shule ya Yamen English Midium Primary School iliyopo Chang`ombe Jijini Dar es Salaam.
6. JELLA MTAGWA:
Kama alivyokuwa Bakari, Mtagwa naye alikuwa ni mlinzi wa kati na kiungo mahiri wa kutegemewa wa timu ya Taifa Stars katika miaka ya 1970 katikati mpaka 1980 katikati. Mtagwa ameichezea timu ya Taifa Stars miaka 10 mfululizo kuanzia mwaka 1974 mpaka 1984.Licha ya kuichezea kwa mafanikio makubwa timu ya Taifa Stars, pia katika vipindi tofauti vya nyuma ameichezea klabu ya Nyota Afrika ya Morogoro, Yanga, Pan African na timu ya Taifa Vijana. Mtagwa anakumbukwa na wapenzi wa soka nchini kuwa ni mchezaji pekee picha yake iliyowahi kuwekwa katika Stempu za Posta. Kwa hivi sasa Mtagwa anaishi Friends Corner Magomeni Jijini Dar es Salaam.

7. GODFREY NGURUKO:
Nguruko alikuwa ni mashambuliaji mahiri na wa kutegemewa wa timu ya Taifa Stars aliyemudu kucheza vyema nafasi ya winga ya kulia namba saba katika katika miaka hiyo ya 1970 katikati.Nguruko alichaguliwa kuchezea timu ya Taifa Stars akitokea klabu ya Coastal Union ya Tanga moja ya klabu iliyokuwa na wachezaji mahiri wakati huo. Katika mechi hiyo ya fainali ya michuano ya Chalenji baina ya Taifa Stars na Uganda Cranes, Nguruko kipindi cha pili alipumzishwa na nafasi yake kuchukuliwa na Shiwa Lyambiko. Kwa hivi sasa inasemekana Nguruko anaishi Mkoani Tanga akijishughulisha na shughuli zake binafsi.

8. SHIWA LYAMBIKO:
Huyu Lyambiko alikuwa ni mshambuliaji wa timu yaTaifa Stars katika kipindi hicho cha miaka ya 1970 katikati. Lyambiko alikuwa akipokezana kucheza nafasi ya winga ya kulia namba saba na Godfrey Nguruko.Katika fainali hiyo ya mashindano ya Chalenji baina ya Taifa Stars na Uganda Cranes, Lyambiko aliingia kipindi cha pili, lakini alikuwa ni mmoja wa wachezaji waliofunga penalti kati ya zile tano ambazo Taifa Stars walizipata siku hiyo.Lyambiko alichaguliwa kuchezea timu ya Taifa Stars akitokea klabu ya Mseto FC ya Morogoro moja ya klabu kubwa nchini wakati huo iliyokuwa inatandaza soka safi. Kwa hivi sasa Lyambiko anaishi Mkoani Morogoro.

9. SUNDAY MANARA:
Unapozungumzia wachezaji waliowahi kuvuma na kutamba hapa nchini kwa kucheza kandanda safi na la uhakika huwezi kuacha kulitaja jina la Sunday Manara.Kutokana na kucheza soka safi na la kimahesabu katika miaka hiyo ya 1970 pamojana ‘Computer’ kutotumiwa nchini Tanzania kwa wakati huo,lakini yeye wapenzi wa soka walimbatiza jina la ‘Computer’, wakimaanisha kuwa ana uwezo mkubwa wa kucheza soka vizuri na kwa uhakika kama ‘Computer’.Pamoja na kucheza soka kwa mafanikio makubwa hapa nchini Tanzania, Sunday inasemekana alikuwa mchezaji wa kwanza Mtanzania kucheza soka la kulipwa Ulaya.Sunday pamoja na kung’ara akiwa na timu ya Taifa Stars,pia katika vipindi tofauti vya nyuma ameichezea klabu ya Yanga, Nyota Afrika ya Morogoro na Pan African. Sunday ni ndugu ya wachezaji wengine mahiri wawili waliowahi kutamba hapa nchini Kitwana Manara na Kassim Manara ambao wote walichezea kwa mafanikio makubwa klabu za Yanga na Pan African. Kwa hivi sasa Sunday anaishi Jijini Dar es Salaam akijishughulisha na shughuli za biashara.

10. MWINDA RAMADHANI:
Mwinda alikuwa ni mmoja wa washambuliaji wa kutegemewa sana na timu ya Taifa Stars katika miaka hiyo ya 1970 katikati. Mwinda alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuchezea timu ya Taifa Stars mwaka 1974 akitokea klabu ya Pamba FC ya Mwanza.Pamoja na kuichezea kwa mafanikio makubwa timu ya Taifa Stars na timu ya Pamba FC ya Mwanza, pia ameichezea timu ya Taifa ya vijana na klabu ya Yanga SC na alikuwa katika kile kikosi cha timu ya Yanga ha mwaka 1977 kilichofungwa mabao 6-0 na Simba.Kutokana na uwezo mkubwa aliokuwa akiuonyesha akicheza nafasi ya ya ushambuliaji wa kati sentafowadi na kufunga mabao, wapenzi wa soka nchini walimbatiza jina la ‘Maajabu’ wakimaanisha kuwa alikuwa akifunga mabao kimaajabu mno. Kwa hivi sasa inasemekana Mwinda anaishi nchini Uingereza.

11. GIBSON SEMBULI:
Kati ya washambuliaji wachache mahiri waliowahi kutokea nchini kwa upigaji mashuti makali ni huyu Gibson Sembuli, kwani katika miaka ya 1970 kulikuwa hakuna mpigaji mashuti makali kama yeye.Sembuli alichaguliwa kuchezea timu ya Taifa Stars mwaka 1974 akitokea klabu ya Jogoo FC iliyokuwa na maskani yake makuu Mjini Morogoro.Pamoja na kuichezea timu ya Taifa Stars na Jogoo FC ya Morogoro kwa mafanikio makubwa, pia katika vipindi tofauti ameichezea klabu ya Yanga SC, Nyota Afrika FC ya Morogoro na Pan African. Kwa hivi sasa hatunaye tena Sembuli, kawani amefariki dunia mwaka 1979.

12. LUCAS NKONDOLA:
Kati ya wachezaji wachache waliokuwa na uwezo wa kucheza nafasi nyingi wawapo uwanjani ni huyu Lucas Nkondola,kwani alimudu kucheza vyema nafasi ya ulinzi wa kushoto namba tatu, kiungo namba sita na nane na nafasi ya ushambuliaji wa kushoto namba kumi na moja.Pamoja na kutamba akiwa na timu ya Taifa Stars katika miaka hiyo ya 1970, pia kutokana na umahiri wake wa kusakata soka ameweza kuichezea klabu ya Pamba FC ya Mwanza, Sungura FC ya Tabora, Simba SC, timu ya Mkoa wa Mwanza, timu ya Mkoa wa Shinyanga, timu ya Mkoa wa Dar es Salaam na timu ya Taifa ya Vijana.Katika mchezo wa fainali wa mashindano hayo ya Chalenji mwaka1974, Nkondola ndiye aliyefunga bao pekee kwa upande wa Taifa Stars katika dakika ya 25 ya kipindi cha kwanza, kabla ya Uganda Cranes kusawazisha bao katika dakika ya 85.Pia katika upigaji wa penalti Nkondola alifunga penalti moja kati ya tano zilizopatikana kwa upande wa Taifa Stars siku hiyo. Kwa hivi sasa Nkondola anaishi Magomeni Jijini Dar es Salaam akijishughulisha na shughuli zake binafsi

1 comment:

  1. Je ni kikosi kipi kilikuwa na akina Haidari Abed, Khalid Abed, Athman Mambosasa, Kajole, Kibadeni, Digongwa, Zimbwe nk. Nakumbuka mwaka 1973 kikosi kama hiki pamoja na uliyo wataja hapo juu kilifanya maandalizi mjini Bukoba kabla ya kwenda Uganda. Sasa sikumbuki ilikuwa ni mwaka 1973 au 1974? Katika mazoezi, kombaini ya Mkoa wa Ziwa Magharibi wakati huo ilifungwa goli 8 -0.

    ReplyDelete