Jumla ya mechi sita zimepigwa hivi leo kwenye ufunguzi wa michuano hiyo, ambapo zimepigwa mechi tatu kwa kila uwanja, kuanzia saa tatu za asubuhi hadi saa kumi na mbili za jioni.
Asubuhi saa tatu ulipigwa mchezo baina ya Azam FC dhidi ya Kagera Sugar kwenye uwanja wa Mbande, na muda huo huo kwenye uwanja wa Karume ukapigwa mchezo baia ya Ruvu shooting starz, mabingwa watetezi dhidi ya JKT Oljoro ya jijini Arusha.
Baadae saa nane mchana wakati Dar es salaam Young Africans wakikabiliana na Moro United kwenye uwanja wa Mbande, katika uwanja wa Karume ukawa ukipigwa mchezo baina ya Ruvu starz dhidi ya Polisi Dodoma.
Mwisho saa kumi alaasiri, wakati Simba wakimaliza udhia na wagosi wa Ndima Coastal Union toka jijini Tanga kwenye uwanja wa Mbande, Toto Africans ya jijini Mwanza wakawa wanapapatuana na waalikiwa wa michuano hiyo, Serengeti Boyz.
Tukianzia na mchezo wa kwanza kule Mbande hapo asubuhi, Azam dhidi ya Kagera ni kuwa dakika tisini zilimalizika kwa Azam FC kuilaza Kagera Sukari mabao mawili kwa moja.
Baadae saa nane mchana kwenye uwanja huo huo Young Africans, walikiona cha mtemakuni mbele ya vijana wa Moro United, baada ya kuzabwa mabao matatu kwa moja, wakionekana kushindwa kabisa kustahmili vishindo vya vijana wa Moro United.
Na hapo saa kumi za jioni kibarua kwenye uwanja huo kwa siku ya leo kikakamilishwa kwa mchezo baina ya Simba dhidi ya Coastal Union na pambano likimalizika kwa Simba kuisasambua Coastal Union mabao matatu kwa sifuri.
Mabao ya Simba kwenye mchezo huo yakiwekwa kimiani kwa ustadi mkubwa na washambuliaji Edo Christopher, Miraji Madenge na Rashid, huku vijana hao wa msimbazi wakipiga soka ya uhakika kabisa.
Vijana wa Moro United wanaonekana kuwa wamejipanga sana na wakiwa na timu ambayo inaonekana kuzoeana kabisa, kama ilivyo kwa wekundu wa msimbazi Simba sports club, ambao inavutia kuwatazama kutokana na kucheza soka la pasi nyingi za uhakika na kuvutia.
Bado yaonekana kana kwamba litakalowakuta Young Africans litakuwa kama lile la msimu uliopita, kutokana na kutokuwa na timu inayocheza kama timu zaidi ya vipaji binafsi, tofauti na timu kama za Moro, Azam, na Simba.
Kati mwa mji kwenye uwanja wa Karume, asubuhi Ruvu shooting dhidi ya Oljoro pambano hilo lilimalizika kwa mabingwa watetezi wa taji hilo Ruvu shooting starz kulambwa mabao mawili kwa moja.
Na saa nane za mchana JKT Ruvu starz dhidi ya Polisi Dodoma..
Mwisho saa kumi za jioni Toto Africans dhidi ya Serengeti Boyz wakaumiza nyasi za uwanja wa Karume jijini kwa kwenda sare ya kufungana mabao mawili kwa mawili, ambapo Serengeti Boyz walilazimika kutoka nyuma na kusawazisha mabao yote mawili.
Kesho ni mapumziko katika michuano hiyo, na jumla ya michez9o mingine sita itapigwa hapo siku ya jumatatu, kwenye viwanja vya Mbande huko Chamazi na uwanja wa Karume kati mwa jiji.