Na Baraka Mpenja
NDOTO kubwa ya wanandinga wa Tanzania na Afrika nzima ni kucheza soka la kulipwa katika ligi kubwa duniani kama vile ligi kuu nchini England, Hispania, Ujerumani, Ufaransa, na Italia.
Hakuna mwanasoka mwenye malengo asiwaze kucheza katika ligi hizo zilizosheheni klabu zenye mvuto mkubwa zaidi duniani na wanasoka bora wa Dunia.
Hakika ni sifa kubwa sana kwa mchezaji wa Kiafrika kuonekana katika runinga akisakata kabumbu anga za kimataifa. Simaanishi anaishia kupata sifa tu, bali hata `mkwanja` unaopatikana katika soka hilo ni mkubwa.
Nani asiyefahamu utajiri wa Samuel Eto`o, Didier Drogba, Yaya Toure na wengine wengi kutoka nchi za magharibi mwa Afrika.
Hapa Tanzania bado hatujafanikiwa kupata wanasoka mahiri wa kwenda kucheza ligi za wenzetu zaidi ya kuwaona wachezaji wetu wakienda kucheza ligi za kawaida kabisa huko Uarabuni na mataifa ya kiwango cha chini kisoka barani Ulaya.
Wengine kama Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu wamejaribu na wamethubutu na ndio maana unawasikia na kuwaona TP Mazembe ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo.
TP Mazembe ni moja ya klabu kubwa yenye utajiri mkubwa barani Afrika. Kwa wachezaji wa Kitanzania ni moja ya klabu inayowafaa na ndio maana Samatta alitajwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaowania tuzo ya mwanasoka bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani.
Ukiwauliza wachezaji wengi wa Tanzania, nini malengo yao? Jibu huwa ni jepesi sana“nataka kucheza soka la kulipwa”. Sio tatizo kwa jibu hili, lakini bado ipo haja ya kujiuliza tena, huyu anayetaka kucheza soka hilo anaweza kutimiza ndoto hizo?.
Swali hili huwa linanikosesha majibu ya haraka kila nikitafakari hali halisi ya wachezaji wa Kitanzania ambapo wengi wao wana malengo makubwa, lakini utekelezaji wake ni mdogo sana, nidhamu mbovu na kulewa sifa wakati bado hajafanikiwa malengo yake.
Achana na hayo, kwasasa Dunia inajadili sana soka la wanawake.
Hakika Mpira wa miguu kwa wanawake ni moja ya michezo inayokuwa kwa kasi katika bara la Afrika na hata hapa nyumbani.
Idadi ya wasichana wanaoshiriki katika mpira wa miguu imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.
Ukiwasikia TFF /TWFA pamoja na wadau wa soka, wanaamini kuwa ili kuwa na kiwango kizuri na maendeleo katika mpira wa miguu wa wanawake ni lazima kuanza na vijana wadogo.
Wakati mawazo haya yakitawala vichwani mwa viongozi wa soka, tayari Wapenda michezo nchini wameshaanza kushabikia soka la wanawake.
Leo hii mashabiki wanaenda kuishangilia timu ya Taifa ya wanawake, Twiga Stars na wengine kuiombea dua njema ili ifanikiwe katika harakati zake za kulitangaza soka la wanawake.
Sina wasiwasi na vijana wa Twiga stars, nimefanya mahojiano nao mara kwa mara.
Kiukweli ukiwasikia, wana nia ya kucheza soka la kulipwa kama ilivyotokea kwa dada yao na nahodha, Sophia Mwasikili ambaye alibahatika kupata timu nchini Uturuki, ingawa kwasasa amerudini nchini.
Hivi karibuni, Twiga Stars ilikuwa katika mchezo mgumu wa kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika kwa wanawake (AWC) dhidi ya Zambia (Shepolopolo).
Twiga Walifungwa mabao 2-1 mjini Lusaka na waliporudi nyumbani walitoka sare ya bao 1-1 uwanja wa Azam Chamazi na kutolewa kwa wastani wa mabao 3-2.
Matokeo sio ishu ya kujadili kwa sasa, stori kubwa ni taarifa ya jana ya TFF kuwa kuna wachezaji wawili wa Twiga Stars walitimuliwa kambini na kocha mkuu wa timu hiyo, Rogasian Kaijage kwa sababu za utovu wa nidhamu.
Afisa habari wa TFF, Boniface Wambura Mgoyo aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Kocha Kaijage aliwatimua kambini wachezaji Mwapewa Mtumwa na Flora Kayanda kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu wakati Twiga Stars ikijiandaa kwa mechi ya marudiano ya michuano ya Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Zambia.
Akaongeza kuwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatafakari hatua zaidi za kinidhamu dhidi ya wachezaji hao wawili wa kikosi cha Twiga Stars walioondolewa kwenye timu hiyo na Kocha Kaijage.
Hoja ya msingi kujadili ni utovu upi wa nidhamu walioufanya hawa wachezaji.
Ilielezwa na Wambura kuwa kuna siku kocha Kaijage aliwapa mapumziko ya siku moja wachezaji wake ili wakasalimie ndugu na jamaa, huku akiwataka kurejea saa 12 jioni siku hiyo.
Wachezaji hao waliporudi kambini jioni walibainika kuwa wamelewa pombe.
Kwa maana hiyo hawakwenda kusalimia kama walivyoambiwa, bali wao walikwenda kutafuta pombe ili kujiburudisha. Kama walikwenda kusalimia, labda walipata pombe huko.
Sisemi mtu hatakiwa kunywa pombe kama anadhani ina faida kwake. Huo ni uhuru wa mtu. Lakini hoja yangu ni mazingira ambayo wachezaji hawa walikuwa nayo kwa wakati huo.
Walikuwa wanakabiliwa na mechi ngumu ya mashindano, huku watanzania wanaopenda soka, usiku na mchana wakiwatia moyo na kuwaombea dua ili wawafunge Zambia na kusonga mbele.
Najiridhisha kuwa ilikuwa ni wakati wa wachezaji wote wa Twiga kutafakari mchezo huo na kuweka akili yao yote.
Haikuwa wakati sahihi wa kuwaza kunywa pombe endapo watapewa siku ya mapumziko na kurejea kambini jioni.
Hapa ndipo suala la kukosa malengo linapoibuka kwa wanandinga wa Tanzania.
Najaribu kuwaza kinadharia endapo Twiga Stars wangeishinda Zambia na kufanikisha kusogea mbele, hatimaye kufuzu fainali hizo, bila shaka ingekuwa nafasi yao kujitangaza na kuonekana kimataifa.
Huwezi jua, labda ndio ingekuwa bahati ya vijana hao kwenda ulaya kucheza soka.
Hakuna namna ya kufika mbali katika soka kama hujaonekana. TP Mazembe walimuona Samatta ligi ya mabingwa ndio maana walimsajili. CAF walimuona kijana huyo ligi ya mabingwa ndio maana wakamtaja kuwania Tuzo.
Upo umuhimu mkubwa wa kuisaidia timu kufuzu mashindano ya kimataifa kwani itaweza kuwa mlango wa kutokea.
Kwa wachezaji Mwapewa Mtumwa na Flora Kayanda imekuwa tofauti kwao, wakati kila mtu anawategemea, wao wanawaza pombe endapo wakipewa mapumziko. Tutafika? Malengo ya wachezaji wetu kufika mbali yatatimia kama wanavyojieleza mara zote?.
Nimeguswa sana na kitendo hiki. Nimepata nafasi ya kuzungumza na watu wengi kujiridhisha kama nipo sahihi kuchukizwa na tabia hii mbaya. Matokeo yake, wadau wengi wanasema wachezaji hawa wa Twiga wamelitia aibu Taifa na kuwaangusha watanzania wakati huu muhimu kwao.
Nikiwa njiani kurudi nyumbani baada ya tafakuri hiyo ya siku kwangu, nikabahatika kuonana na mchezaji wa zamani wa Yanga na sasa kocha wa mpira wa miguu, Seklojo Johnson Chambua na kumshirikisha jambo hili kwani kwa wakati huo alikuwa hajapata taarifa hiyo.
Baada ya kumsimulia ishu hiyo, Chambua aliuliza mara mbili akisema hajanielewa. Nikadhani labda Kiswahili kimekuwa kigumu kwake. Kumbe alikuwa anahakikisha anachokisikia kutoka kwangu.
Hapo sasa!, Chambua kama nyati aliyejeruhiwa, alianza kueleza kwa masikitiko makubwa sana juu ya kitendo hicho.
“Ninaunga mkono hatua ya kocha Kaijage kuwatimua vijana hawa. Pili nawaomba TFF wachukue hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine’. Alisema Chambua.
Mwanasoka huyo wa zamani aliongeza kuwa tatizo la vijana wetu ni kwamba hawaandaliwi vizuri kutambua wakati waliopo kwani Twiga ilikuwa inahitaji ushindi kwa nguvu zote.
“Kwa mchezaji aliyeandaliwa vizuri hawezi kuwaza pombe wakati muhimu kwa timu. Akili yake inatafakari mechi tu. Sasa linapotokea suala kama hili, ni rahisi kujua kuwa wachezaji wengi wa Tanzania hawana malengo na kazi yao”. Alisema Chambua.
Aidha akashauri kuwa walimu wa soka wawe wepesi wa kuwajenga vijana wao katika misingi bora ya kujitambua na kutambua mchango wao kwa Taifa.
Hayo ni baadhi ya maneno ya Chambua kati ya mengi aliyosema. Hakika mawazo yake yalikuwa sahihi na alionekana kuguswa na utovu huu wa nidhamu.
Lakini wakati huo nikapokea simu nyingi kutoka kwa watu wa mpira wakieleza machungu yao.
Wote walilaani vikali tabia mbovu ya wachezaji wa Tanzania na kusema wanalitia aibu taifa.
Kitendo cha kulewa pombe kiliwakera sana na wamewataka wachezaji hawa kuliomba radhi taifa kwa tabia yao mbaya.
Kutokana na mchango wa watu wengi nilioongea nao, nikagundua kuwa mashabiki wengi wa soka wana hamu ya kuona timu zao zinafanikiwa, lakini wanandinga wao wanaowaangusha vibaya mno.
Wanashindwa kukata kiu kwasababu wanaathiriwa na sababu nyingi za nje ya uwanja. Wanalewa Sifa na kujiona wamefika.
Kwa ujumla, Mwapewa na Flora mmewaudhi Watanzania. Kaeni chini na kutafakari upya. Kama mtagundua kuwa mmekosea, ombeni radhi kwa Taifa.
Kujituma kwenu ndio siri ya Taifa. Kuondolewa kikosini yawezekana mlivuruga mipango ya kocha kaijage kutokana na ukongwe wenu.
Wapo vijana wengi nyuma yenu wanaohitaji kujifunza kutoka kwenu. Tabia hii mliyoionesha inakera kwa mtu yeyote anayependa mpira.
Hatuingilii uhuru wenu, starehe ni haki yenu. Lakini suala la wakati lazima mzingatie.
Sidhani kama tungeyazungumza haya endapo mngeyafanya baada ya mechi na Zambia Chamazi. Hapana.
Lakini kwakuwa mmeyafanya wakati ambao timu inajiandaa kukabiliana na mechi ngumu, lazima tuseme ukweli kuwa mmewakosea Watanzania wanaopenda soka.
Cha msingi wachezaji wote wa Twiga Stars na Taifa stars mnatakiwa kutambua suala la wakati.
Fanyeni kazi kwanza, baaya ya kufanikiwa nendeni mkalewe wakati mnajiweka sawa kwa mambo mengine ya uwanjani.
Sisemi kulewa kuna faida kwenu, lakini najaribu kusema, ni vyema mkaangalia kama pombe inawafaa wakati huu mnaotafuta mafanikio.
Kama mtagundua jibu ni ndiyo, Nendeni, lakini mkiona sio, msiende. Au ulizeni waliotangulia wawaeleze uhusiano uliopo kati ya pombe na mpira.
Lakini kwa busara zangu, nawashaurini msiendekeze starehe wakati huu mgumu kwenu mkihitaji mafanikio.
Twiga Stars itacheza mechi za mchujo za michezo ya 11 ya Afrika (All Africa Games) ambayo itafanyika mwakani nchini Congo Brazzaville.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Twiga Stars, Taifa Stars.
Naomba kuwasilisha…………………