Moja
ya mikakati ya Taifa Stars kwenye mechi ya kesho (Julai 27 mwaka huu)
dhidi ya Uganda kuwania kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Tatu za
Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini
Afrika Kusini ni kushambulia kwa muda mwingi wa mchezo.
Kocha
Kim Poulsen amesema maandalizi ya Taifa Stars jijini Mwanza kwa ajili
ya mechi hiyo ambayo Uganda inaongoza kwa bao 1-0 yalikuwa mazuri,
lakini mabao ni muhimu hivyo watashambulia bila kusahau kulinda lango
lao.
“Unapocheza
mechi za aina hii za nyumbani na ugenini, huku mwenyeji akiwa anaongoza
mabao yana maana kubwa katika mechi. Mabao yanabadili mchezo na pia
wachezaji kifikra,” amesema Kim akizungumza na waandishi wa habari
kwenye hoteli ya Mt. Zion ambayo Stars imefikia.
Amesema
katika mechi ya kwanza walitengeneza nafasi nyingi lakini
hawakuzitumia, hivyo wamekuwa wakifanya mazoezi ya kushambulia, jinsi ya
kutengeneza nafasi, na jinsi ya kumalizia.
“Hivyo
tuko hapa (Kampala) kwa ajili ya kufunga, ni lazima tufunge ili tuweze
kuendelea na mashindano. Lakini ngome yetu nayo ni lazima iwe makini ili
kutoruhusu bao,” amesema Kim na kuongeza kuwa kikosi chake cha kwanza
ni lazima kitakuwa mabadiliko kutoka na Mwinyi Kazimoto kuingia mitini
na Shomari Kapombe kwenda kwenye majaribio Uholanzi.
Amesema
angalau kutakuwa na mabadiliko kwa kuingiza sura mbili mpya katika
kikosi cha kwanza, na kuongeza kuwa wachezaji wanafahamu umuhimu wa
mechi hiyo kwani timu ikienda kwenye Fainali za CHAN itakuwa manufaa
kwao binafsi.
Taifa
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imefanya mazoezi ya
mwisho leo jioni Uwanja wa Mandela ulioko Namboole ambao utatumika kwa
ajili ya mechi hiyo kesho.
Mechi
hiyo itaanza saa 10 kamili jioni kwa saa za Afrika Mashariki na
itachezeshwa na waamuzi kutoka Madagascar wakiongozwa na Kanoso Abdoul
Ohabee wakati mwamuzi msaidizi namba moja ni Andirvoavonjy Pierre Jean
Eric. Mwamuzi msaidizi namba mbili ni Jinoro Velomanana Ferdinand huku
Andriamiharisoa Hubert Marie Bruno akiwa mwamuzi wa mezani (fourth
official). Kamishna wa mechi hiyo namba 38 ni Ismail Kamal kutoka
Ethiopia.
Stars
inatarajiwa kupangwa hivi; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, David Luhende,
Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Athuman Idd, Salum Abubakar, Frank
Domayo, John Bocco, Amri Kiemba na Mrisho Ngasa.