Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
KINYANG`ANYIRO cha ubingwa wa ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa 2013/2014, bado kinabaki kuwa kitendawili kwa timu zilizopo juu katika msimamo.
Sare ya bao 1-1 jana uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam baina ya vinara Azam fc dhidi ya Yanga imezidi kuweka mazingira magumu kwa mabingwa watetezi, Young African.
Katika mchezo huo uliovuta hisia za mashabiki, Yanga walikuwa wa kwanza kufunga bao kipindi cha kwanza kupitia kwa Didier Kavumbagu, lakini Azam fc walisawazisha dakika za lala salama kupitia kwa kinda, Kevin Friday.
Hiyo ilikuwa mechi ya 19 kwa Yanga, wakati kwa Azam fc ilikuwa ya 20, huku wakijikusanyia pointi 44, wakati Wanajangwani wakivuna pointi 40 katika nafasi ya pili.
Yanga SC wamebakiza mechi 7, wakati Azam fc wamebakiza mitanange 6.
Wikiendi hii timu zote zitashuka dimbani. Yanga watasafiri mpaka mkoani Tabora kuwafuata maafande wa Rhino Rangers, wakati jumapili machi 23, Azam fc watawakaribisha JKT Oljoro, uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Rhino Rangers ndio wanaoburuza mkia katika msimamo wakiwa wameshacheza mechi 21 na kujikusanyia pointi 13 tu kibindoni.
Kwa asilimia kubwa, maafande hawa wa Tabora, wameshachungulia kushuka daraja na inawezekana hakuna muujiza wa kubaki ligi kuu msimu huu kwasababu ya mazingira yao.
Mchezo dhidi ya Yanga utakuwa mkali endapo bado Rhino wanahitaji ushindi.
Lakini imani yao imeshuka na wanacheza bora liende na wameshapoteza matumanini ya kuendelea kucheza ligi kuu.
Pointi 13 kwa mechi 21 ni chache sana, zinahitajika nguvu za ziada kushinda mechi zote 5 walizobakiza, hapo sasa tunaweza kuzungumza mengine.
Yanga wataingia uwanjani wakiwa ma matokeo ya sare ya jana na suluhu ya Mtibwa Sugar wiki iliyopita uwanja wa Jamhuri.
Yanga sc hawajafanya vizuri mechi zao mbili tangu watolewe na Al Ahly ligi ya mabingwa kwa penati 4-3, machi 9 mwaka huu, jijini Alexndria, hivyo hawana cha kuwaza zaidi ya ushindi.
Kama watashindwa kupata ushindi katika mchezo huo, watakuwa wanazidi kuweka rehani ubingwa wao msimu huu.
Kwa maana hiyo, kocha mkuu wa Yanga, Hans Van Der Pluijm lazima awaeleze vijana wake umuhimu wa mechi ya jumamosi endapo wanahitaji ketetea taji lao.
Wakati Yanga wakiwa kwenye mawazo mazito juu ya mchezo huo, wapinzani wao, Azam fc watakuwa wanasubiria matokeo ili kujipanga kwa mchezo wa kesho yake.
JKT Oljoro waliopoteza matumanini ya kusalia ligi kuu msimu , wataingia kuwavaa Azam fc ambao hawajapoteza mchezo mpaka sasa kwa lengo la kutafuta pointi tatu.
Mechi za karibuni zinaonesha kuwa Azam fc wamekuwa bora zaidi katika uwanja wao kwasababu wanagawa dozi kubwa kwa wapinzani.
Mechi iliyopita waliwafunga Coastal Union mabao 4-0, hivyo JKT Oljoro wasipokuwa makini watachezea kipigo.
Endapo Azam fc watashinda mechi hiyo, watazidi kujikita zaidi kileleni, nao Yanga wakishinda watandelea kuwa wa pili.
Matokeo ya sare au suluhu hayatakuwa mazuri kwa Yanga, kwasababu Mbeya City waliopo nafasi ya tatu nao watacheza na JKT Ruvu jumamosi uwanja wa Chamazi.
Kama Yanga hawatashinda na Mbeya City wakapata matokeo ya ushindi, basi Yanga watashuka nafasi ya tatu.
Hata kama watatoa sare au suluhu mjini Tabora, bado Yanga watabaki nafasi ya tatu, kwani Mbeya City watakuwa wamefikisha pointi 42, Yanga 41.
Kama Yanga watashinda na Mbeya City watashinda, basi nafasi za pili na tatu zitabaki kama zilivyo.
Matokeo yoyote ya Yanga na Mbeya City hayatakuwa na athari kwa Azam fc katika nafasi ya kwanza, isipokuwa watasogelewa kwa pointi.
Wakati Yanga na Azam fc wakichunao vikali kusaka ubingwa, mechi zilizosalia kwa timu zote ni kama zifuatazo;
Yanga wamebakiza mechi dhidi ya Rhino Rangers itakayochezwa machi 22 mwaka huu uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Baada ya hapo atakuwa na mechi dhidi ya Tanzania Prisons uwanja wa Taifa.
Ugumu wa mechi hizi mbili unatokana na mazingira ya Prisons na Rhino kwa sasa.
Hawataki kushuka daraja, zaidi Prisons wamedhamiria kubakia lihi kuu kuliko Rhino wanaoonekana kukata tamaa.
Haitakuwa kazi nyepesi kwa Yanga kuwafunga wajelajela hao uwanja wa Taifa, jijini Dar es salaam.
Mechi nyingine zilizosalia kwa Yanga ni dhidi ya Mgambo JKT, Uwanja wa Mkwakwani Tanga.
Hii pia itakuwa na changamoto kubwa kwasababu Mgambo wanajinusuru kushuka daraja msimu huu.
Pia Yanga wamebakiza mechi dhidi ya Kager Sugar, Uwanja wa Taifa, mechi dhidi ya JKT Oljoro, jijini Arusha, mechi na JKT Ruvu uwanja wa Taifa.
April 19 mwaka huu Yanga watafunga msimu kwa kuvaana na Simba sc uwanja wa Taifa.
Katika mechi saba zilizosalia kwa Yanga, mechi mbili pekee ndizo atakutana na timu zilizopo salama msimu huu na zinahitaji nafasi nne za juu.
Kagera Sugar mpaka sasa wana uhakika wa kusalia ligi kuu pamoja na Simba sc ambao wanasaka nafasi za juu.
Mechi nyingine zote, Yanga atakutana na timu zinazopambana kukwepa mkasi wa kushuka daraja. Hivyo lazima ajiandae kwa nguvu zote kwasababu kukamiana kutakuwepo.
Kila timu inahitaji kupata ushindi bila kujali inakutana na timu kubwa au ndogo.
Kocha wa Yanga , Mholanzi, Hans Van Der Pluijm akisaidiwa na Charles Mkwasa wanahitaji kutuliza sana akili zao kuelekea mechi hizo.
Azam fc amebakiza mechi sita ambazo ni dhidi ya JKT Oljoro, Mgambo, Ruvu shooting, JKT Ruvu, Mbeya City na Simba sc.
Mechi dhidi yaMbeya City itakayopigwa sokoine Mbeya, itakuwa ngumu zaidi kwa Azam fc kulingana na rekodi ya Mbeya City katika uwanja wake.
Mbeya City hawajawahi kufungwa kwao, hivyo lazima Azam fc wajiandae kama wanataka kuvunja rekodi hii.
Pia Mbeya City wanasaka ubingwa wa kwanza kama ilivyo kwa Azam fc. Tofauti ni umri katika ligi. Azam fc waliingia 2008/2009, Mbeya City waliingia 2013/2014.
Azam fc ameshakuwa makamu bingwa kwa zaidi ya misimu miwili, wakati Mbeya City ndio kwanza wanaanza kutafuta mafanikio.
Mechi hii itakuwa ngumu kwa timu zote mbili, matokeo yatategemea jinsi makocha wote wawili, Juma Mwambusi wa Mbeya City na Mcameroon, Joseph Marius Omog wa Azam fc wamejipangaje.
Pia mechi dhidi ya Simba sc itakuwa mlima mwingine kwa Azam fc kwasababu Simba hawatakuwa na chakupoteza zaidi ya kusaka ushindi.
Kwa mazingira ya mechi za Azam fc, itakuwa ngumu kwake kupata ushindi kwenye baadhi ya mechi kwasababu wapinzani wake wanahitaji kujiweka vizuri katika msimamo.
Simba na Mbeya City wanawania nafasi za juu. Ruvu Shhoting anatafuta nafasi nzuri pia.
Mgambo, JKT Ruvu, JKT Oljoro wapo katika hatihati ya kukwepa kushuka daraja, hivyo mechi zao zitakuwa ngumu zaidi kutokana na kukutana na timu ambayo inaongoza ligi.
Haitakuwa kazi nyepesi kwa Azam fc kuibuka na ushindi katika mechi hizi, lakini kama watajiandaa vizuri basi wataweza kuvuna ushindi na kujihakikishia kutwaa ubingwa msimu huu.
Ligi ya mwaka huu imekuwa na changamoto kubwa kutokana na timu kubwa za Simba na Yaga kushindwa kufua dafu kwa Azam fc na Mbeya City.
Misimu ya nyuma, mpaka sasa ilikuwa rahisi kubashiri bingwa, na wakati mwingine timu ilikuwa inatangaza ubingwa kabla ya mechi tatu au nne.
Kwa msimu huu jambo hilo limebaki kuwa ndoto, ubingwa utaonekana mechi za mwisho, kwani mpaka sasa mbio bado zipo wazi kwa klabu zaidi ya moja.
Katika soka, hii ni hatua nzuri kwasababu inadhirisha zimekuweo timu zaidi ya mbili zenye ubora wa juu, tofauti na miaka ya nyuma iliyokuwa na ufalme wa Simba na Yanga.
Tuzidi kusubiri ili kuona nani ataibuka kidume katika nafasi nne za juu.