YANGA ya Dar es Salaam ilifurahia
hatua ya kusitisha mikataba ya wachezaji na kutimua watendaji wake bila malipo,
lakini sasa klabu inapaswa kuvunja benki ili kulipa fidia.
Yanga inayokabiliwa na kazi
nzito ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara inapaswa kutafuta Sh. 428.5
milioni (karibu nusu bilioni) kwa ajili ya kuwalipa wachezaji wanne, viongozi
wawili na kumpa fedha mmoja akailipe fidia klabu ya Simba.
Wachezaji wanaoidai Yanga ni
aliyekuwa nahodha wa siku nyingi wa klabu hiyo, Shadrack Nsajigwa na beki
Stephano Mwasyika. Hao wanadai malimbikizo ya fedha za usajili zinazofikia Sh.
15.5 milioni.
Nsajigwa peke yake anadai
shilingi milioni tisa (9) wakati Mwasyika anadai shilingi milioni 6.5.
Utaratibu wa klabu hiyo ni kwamba
wachezaji wapya wanaposajiliwa hupewa fedha taslimu wakati wa zamani hupewa
wanapoongeza mikataba yao ila wengi wao hawalipwi mara moja.
Ndiyo maana leo hii Nsajigwa
na Mwasyika wanaidai Yanga malimbikizo ya fedha walizopaswa kulipwa walipokuwa
bado wanaichezea klabu hiyo.
“Bado Yanga naidai na hakuna
lolote nililoambiwa kuhusu malipo yangu, kama wangekuwa wamenilipa nadhani umma
wa Tanzania ungejua,” alisema Nsajigwa ambaye ni kocha mkuu wa timu ya soka ya Lipuli
ya Iringa inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.
Wachezaji wengine wanaoidai
Yanga ni Wisdom Ndlovu raia wa Malawi na Steven Malashi ambao wanadai Sh. 106
milioni kwa kukatishiwa mikataba yao 16 Julai 2010 miezi minne tu tangu watie
saini kuendelea kuichezea timu hiyo ya Mtaa wa Jangwani 18 Machi 2010.
Baada ya kudai bila mafanikio
stahili zao Ndlovu na Malashi, kupitia kwa wakili Godwin Muganyizi, waliamua
kufungua kesi katika Mahakama Kuu kitengo cha Kazi ambako walishinda. Hivi
karibuni Yanga walikwenda Mahakama ya Rufaa kuomba kesi hiyo ipitiwe upya
lakini ilitupwa kwa maelezo ilishamalizika hivyo walipe deni hilo.
Ndlovu anadai Sh. 57 milioni
na Malashi Sh. 37 milioni. Kabla ya kufungua kesi hiyo mahakamani, wachezaji
hao walipeleka malalamiko yao Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambalo baada
ya kupitia vielelezo liliamuru Yanga iwalipe wachezaji hao. Fedha nyingine
wanazodai ni gharama za kesi yao.
“Tuliishinda Yanga mahakamani,
wakaamriwa watulipe fedha zetu, wakaona si haki kutulipa wakaenda kukata rufaa
nako wamegonga mwamba. Lakini bado wanatusumbua kutulipa,” anasema Malashi
ambaye ni kipa wa zamani wa klabu hiyo.
“Sisi tunafuata sheria na sasa
tupo Mahakama ya Rufaa na wakili wetu kuomba ikazie hukumu ili tulipwe haki
yetu.”
Kundi lingine la watu
wanaoidai Yanga ni waliokuwa watendaji wake; aliyekuwa katibu mkuu wake
Celestine Mwesigwa na Louis Sendeu aliyekuwa ofisa habari .
Septemba mwaka jana, watendaji
hao waliondolewa katika ajira zao kwa kile kilichoelezwa kuwa uongozi
haukuridhika na utendaji wao.
Mwesigwa na Sendeu waliomba
bila mafanikio walipwe na Yanga fidia ya Sh. 262 milioni ambapo kati ya hizo,
Sendeu anadai Sh. 79 milioni na Mwesigwa anadai Sh. 183 milioni.
Watendaji hao walifikisha
suala hilo katika Baraza la Kazi ambao walishinda madai yao na hivyo Yanga
imeamriwa kuwalipa kiasi hicho cha fedha.
“Nashangaa Yanga inajipanga
kuajiri watu wengine wakati sisi waliotufukuza bado tunawadai. Hiki si kitendo
cha kiungwana, wao walipaswa kumalizana nasi kwanza halafu wakaendelea na ustaarabu
mwingine na watu wengine,” anasema Mwesigwa.
Mbali ya madeni hayo, Yanga
inalazimika kubeba deni la usajili wa mshambuliaji wake Mrisho Ngassa
anayedaiwa na klabu ya Simba Sh. 45 milioni yaani Sh. 30 milioni alizochukua
Simba na fidia ya Sh. 15 milioni.
Ngassa aliyekuwa amesajiliwa
na Azam, aliichezea Simba kwa mkopo msimu uliopita na aliingia makubaliano ya
kuingia mkataba kamili wa miaka miwili wa kuichezea timu hiyo ya Mtaa wa
Msimbazi msimu huu. Akapewa Sh. 30 milioni lakini ulipofika muda wa usajili
akatia saini Yanga.
TFF ilimwidhinsha kuichezea
Yanga kwa vile alikamilisha taratibu zote, lakini kwa vile nyaraka zinaonyesha
alimwaga wino akachukua fedha Simba, shirikisho hilo limemfungia mechi sita na
hataruhusiwa kukipiga Yanga hadi alipe deni hilo. Habari zimesema Yanga
watalipa.
Akizungumzia madeni hayo, Katibu
Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako, anasema, “Tunakubali deni la akina Nsajigwa
ambalo lazima tulipe, pia hao akina Malashi bado tunafuatilia mambo ya kisheria
ili tuweze kujua nini tunafanya.”
Kuhusu madeni mengine anasema,
“Hata hayo madeni ya watu wengine (akimaanisha akina Mwesigwa) nayo tunayajua
na kuna vitu tunafuatilia ili tuweze kujua tufanyacho, lakini kuhusu Ngassa
sina jibu la kukupa maana ni kitu kinachoweza kujadiliwa na kamati ya utendaji.”