TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Aprili 13, 2012
ULIMWENGU ATUA NGORONGORO HEROES
Mshambuliaji Thomas Ulimwengu ambaye ndiye mchezaji pekee kutoka nje aliyeitwa na Kocha Kim Poulsen kwenye U20 (Ngorongoro Heroes) anatarajia kujiunga na kikosi hicho ambacho kiko kambini kesho (Aprili 14 mwaka huu).
Ulimwengu ambaye anachezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) atawasili saa 1.20 usiku kwa ndege ya Kenya Airways akitokea jijini Lubumbashi.
Ngorongoro Heroes ambayo iliingia kambini Aprili 20 mwaka huu inajiandaa kwa mechi ya mashindano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 dhidi ya Sudan. Mechi hiyo itachezwa Aprili 21 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
Kwa mujibu wa Kocha Poulsen, kikosi chake kesho (Aprili 14 mwaka huu) kitakuwa na awamu (sessions) mbili za mazoezi kwenye Uwanja wa Karume. Awali ya kwanza itakuwa asubuhi nay a pili itafanyika jioni.
Wachezaji wengine walioko kwenye kikosi hicho cha Ngorongoro Heroes ni Saleh Malande, Aishi Manula, Hassan Kessy, Said Ruhava, Carlos Kilenge, Dizzana Issa, Amani Kyata, Issa Rashid, Emily Mgeta na Khamis Mroki.
Wengine ni Ramadhan Singano, Frank Sekule, Frank Domayo, Omega Seme, Abdallah Hussein, Ibrahim Rajab, Hassan Dilunga, Alhaje Zege, Jerome Lambele, Atupele Green na Simon Msuvan.
Mechi ya marudiano dhidi ya Sudan itachezwa jijini Khartoum kati ya Mei 4, 5 na 6 mwaka huu.
Fainali za Afrika kwa vijana zitafanyika Machi mwakani nchini Algeria. Timu nne za juu kwenye fainali hizo zitacheza Fainali za Dunia zitakazofanyika nchini Uturuki kuanzia Juni hadi Julai mwakani.
LIGI KUU YAINGIA RAUNDI YA 23
Raundi ya 23 ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaingia raundi ya 23 kesho (Aprili 14 mwaka huu) kwa mechi nne. Polisi Dodoma wataikaribisha Azam kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Dodoma wakati JKT Ruvu watakuwa wageni wa Mtibwa Sugar mjini Turiani.
Mechi nyingine za raundi hiyo zitakuwa kati ya Kagera Sugar na African Lyon zitakazooneshana kazi kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba. Nayo Moro United inaikaribisha Oljoro JKT katika mechi itakayofanyika Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Raundi ya 23 itakamilika Jumapili (Aprili 15 mwaka huu) kwa mechi kati ya Ruvu Shooting na Simba itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Yanga itakuwa mgeni wa Toto Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza. Villa Squad itapambana na Coastal Union kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Ligi hiyo itaendelea tena Aprili 18 mwaka huu kwa mechi tano. Kagera Sugar vs Yanga mjini Bukoba, Toto Africans vs African Lyon jijini Mwanza, JKT Ruvu vs Simba- Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Ruvu Shooting vs Moro United mjini Mlandizi na Polisi Dodoma vs Coastal Union mjini Dodoma.
BONGO MOVIE KUICHANGIA TWIGA STARS
Timu ya Taifa ya mpira wa miguu kwa wanawake (Twiga Stars) itacheza mechi ya kirafiki na timu ya wasanii wa filamu ya Bongo Movie itakayofanyika Jumamosi (Aprili 14 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Lengo la mechi hiyo ya maonesho (exhibition) ni kuichangia Twiga Stars ambayo hivi sasa iko kwenye mashindano ya mchujo ya Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) ambayo fainali zake zitafanyika Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea.
Pia asilimia mbili ya mapato yatakayopatikana kwenye mechi ya Twiga Stars na Bongo Movie yatakwenda kwenye familia ya mwigizaji nguli wa filamu Tanzania, Stephen Kanumba aliyefariki dunia Aprili 7 mwaka huu.
Kiingilio katika mechi hiyo kitakuwa sh. 10,000 kwa VIP A, sh. 5,000 kwa VIP C na B na sh. 2,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, kijani na bluu. Mechi itaanza saa 10 kamili jioni.
Machi 10 mwaka huu, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara alizindua akaunti ya Twiga Stars kupitia Tigo Pesa kuichangia timu hiyo ambayo inashiriki michuano ya AWC. Wachangiaji wanatakiwa kutuma mchango wao kwenda namba 13389.
RUFANI YA YANGA KWA TIBAIGANA
Kikao cha Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kilichokuwa kifanyike kesho (Aprili 14 mwaka huu) kujadili rufani ya Yanga kupinga kunyang’anywa pointi tatu kwa kumchezesha Nadir Haroub katika mechi dhidi ya Coastal Union kimeahirishwa.
Kamati hiyo chini ya uenyekiti wa Kamishna mstaafu wa Polisi, Alfred Tibaigana sasa kitafanyika Jumanne (Aprili 17 mwaka huu) saa 9 alasiri kwenye ofisi za TFF.
MIKOA 13 YAWASILISHA MABINGWA WAKE
Vyama vya mpira wa miguu vya mikoa 17 ya Tanzania Bara vimewasilisha majina ya mabingwa wake kwa ajili ya Ligi ya Taifa iliyopangwa kuanza Aprili 22 mwaka huu katika vituo vitatu.
Mikoa hiyo na mabingwa wake katika mabano ni Kigoma (Kanembwa FC ya Kibondo), Kilimanjaro (Forest FC ya Siha), Ruvuma (Mighty Elephant ya Songea), Dodoma (CDA), Rukwa, (Mpanda Star ya Mpanda), Iringa (Kurugenzi FC ya Mufindi) na Lindi (Lindi SC).
Mingine ni Mtwara (Ndanda FC), Shinyanga (Mwadui FC), Mara (Polisi Mara), Singida (Aston Villa), Arusha (Flamingo SC) na Tabora (Majimaji FC). Mikoa ambayo haijawasilisha mabingwa wake ni Manyara, Dar es Salaam, Mwanza, Tanga, Morogoro, Pwani na Kagera.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)