Search This Blog

Saturday, April 14, 2012

SAMATA NA ULIMWENGU KUANZAMAZOEZI - UONGOZI WA MAZEMBE WAKANA SAFARI YA DAR KUCHEZA NA SIMBA.

Uongozi wa timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) umesema taarifa kuwa ina mpango wa kuja nchini kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho, Simba hazina ukweli na wameshangazwa na taarifa hizo.

Mdhamini wa zamani wa Simba, Azim Dewji alisema katikati ya wiki hii jijini Dar es Salaam, kwamba alikuwa akifanya mipango ya kuileta timu hiyo ya DRC kuja nchini kujipima nguvu na Wekundu hao wa Msimbazi.

Mbali ya uongozi wa Simba kutoa taarifa za kutoutambua ujio huo, Kocha Msaidizi wa TP Mazembe, David Mwakasu alisema hawana ratiba ya kuja Tanzania kwa ajili ya mechi hiyo na kuonyesha kushangazwa na taarifa hizo.

Mwakasu alisema kwa njia ya simu kuwa timu yao inakabiliwa na mechi ngumu wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya timu ya El Marreikh ya Sudan Kaskazini uliopangwa kuchezwa Uwanja wa Stade de la Kenya wa Jimbo la Katanga mjini Lubumbashi na wiki mbili badaye itacheza mechi ya marudiano mjini Khartoum.

Alisema kama msaidizi wa Kocha Mkuu, Lamine Ndiaye hawajapokea taarifa zozote kutoka kwa uongozi kuhusiana na mechi hiyo.
Sisi ndiyo tunaotoa taarifa kwa uongozi kuwa tunahitaji mechi za kirafiki kwa ajili ya kujua uwezo wa wachezaji wetu, hatujawahi kuzungumzia mechi dhidi ya Simba na wala uongozi haujatoa taarifa kwetu kama kuna maombi hayo, alisema Mwakasu.

Alisema wanafahamu wanakabiliwa na kibarua kigumu na lazima wawe makini katika mechi dhidi ya El Merreikh ambapo mshindi ataingia hatua ya makundi (robo fainali). Timu hiyo leo inacheza mchezo wake wa tano wa Ligi Kuu ya DRC dhidi ya timu ya AS Vita mjini Kinshasa. 

Mbali ya hayo, Mwakasu alisema mchezaji wao, Mbwana Samatta ameanza mazoezi madogo kwa ajili ya kuumia kwenye mechi dhidi ya Dynamo ya Zambia iliyochezwa mjini Lusaka.
Alisema kuwa wanamfuatilia kwa umakini mchezaji huyo ili aweze kurejea uwanjani kwani wanathamini mchango wake unaotokana na uwezo wake mkubwa uwanjani na hasa katika kufunga.
Kuhusiana na Thomas Ulimwengu, kocha huyo alisema alikuwa majeruhi muda mrefu na alitarajia kuanza mazoezi madogo madogo.
Wote ni majeruhi, lakini tulitarajia waanze mazoezi madogo madogo, alisema. Hata  hivyo Ulimwengu alitarajiwa kuwasili nchini jana kujiunga na kambi ya timu ya taifa ya chini ya umri wa miaka 20 kwa ajili ya mechi ya kufuzu dhidi ya Sudan Kaskazini.

source: mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment