Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Joram Biswaro amewataka
wachezaji wa Taifa Stars kuhakikisha wanaipeleka timu hiyo kwenye fainali za
Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazil.
Ametoa changamoto hiyo wakati alipotembelea mazoezi ya timu hiyo
jana (Mei 29 mwaka huu).
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imepiga
kambi nchini Ethiopia na inafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Addis Ababa.
“Watanzania tunafurahi kutokana na uwezo mnaouonyesha, hasa
baada ya kuifunga Morocco mabao 3-1. Kama mliwafunga nyumbani hata kwao mnaweza
kuwafunga. Tunataka kuwaona Maracana (Brazil) mwakani, mimi tayari ninayo
tiketi mtanikuta kule,” amesema Balozi Biswaro ambaye enzi zake aliwahi
kuichezea timu ya Yanga.
Taifa Stars ambayo iko Addis Ababa tangu Jumatatu (Mei 27 mwaka
huu) imeweka kambi katika hoteli ya Hilton ambapo Jumapili (Juni 2 mwaka huu)
itacheza mechi ya kirafiki na Sudan (Nile Crocodile) kwenye Uwanja wa Addis
Ababa.
Balozi Biswaro ameikaribisha Taifa Stars ubalozini Addis Ababa
mara baada ya mechi dhidi ya Sudan ambapo itakutana na baadhi ya Watanzania
wanaoishi Ethiopia kabla ya kuondoka alfajiri kwenda Marrakech, Morocco kwa
kupitia Cairo, Misri.
Kocha Kim Poulsen amesema kikosi chake kinaendelea na mazoezi
vizuri na kitaimarika zaidi baada ya wachezaji Mbwana Samata na Thomas
Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo
(DRC) kujiunga nacho Juni 3 mwaka huu jijini Marrakech kwa ajili ya mechi dhidi
ya Morocco itakayochezwa Juni 8 mwaka huu.
Naye Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe,
akizungumza kutoka Dar es Salaam, alisema wao kama wadhamini wamefarajika kuona
timu inaendelea vizuri Mjini Addis na inaleta
matumaini kuwa watacheza vizuri katika mechi dhidi ya Morocco Juni 8.
“Tuna imani sana na Taifa Stars kwani wameshatuonesha yote
yanawezekana…watanzania waiombee timu yetu ili na sisi tupate nafasi ya kucheza
Brazil mwakani,” alisema.
Wachezaji walioko katika kikosi cha Stars jijini Addis Ababa ni
Juma Kaseja, Aggrey Morris, Mwadini Ally, Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Kevin
Yondani, Erasto Nyoni, Haroub Nadir, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho
Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva, John Bocco,
Vicent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd, Haruni Chanongo na Zahoro Pazi.