Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
SIMBA SC yenye matokeo mabovu kwasasa inaingia kambini maeneo ya Mabibo jijini Dar es salaam kuandaa kikosi cha kuwavaa vinara wa ligi kuu soka Tanzania bara, wana Lambalamba, Azam fc siku ya jumapili uwanja wa Taifa.
Hiyo ni hatua ya Simba kuweka akili sawa ili kukwepa kipigo kwa mara nyingine baada ya kufumuliwa bao 1-0 na Wagosi wa Kaya, Coastal Union ya jijini Tanga mwishoni mwa wiki iliyopita.
Afisa habari wa Simba aliuambia mtandao huo kuwa uongozi wa Simba unasikitishwa na matokeo mabaya wanayozidi kupata msimu huu licha ya kuwaweka wachezaji wao katika hali nzuri kuanzia mishahara, kambi na posho.
“Hakuna mchezaji mwenye tatizo na benchi la ufundi au uongozi. Wote wanalipwa vizuri mishahara na posho zao. Mengi yanazungumzwa kuwa hawalipwi, Si kweli, hakuna mchezaji anayeidai klabu”.
“Hata sisi hatuelewi kwanini tunapata matokeo mabovu. Hatuna jinsi, lazima tukubali ukweli kwasababu mpira unachezwa uwanjani. Lakini kuumia kuko palepale”. Alisema Asha.
Afisa habari huyo aliwaomba mashabiki wao kukubali na hali halisi inayotokea uwanjani, kwasababu kuna wakati mpira unawakataa wachezaji.
“Benchi la ufundi wanafanya kazi kubwa kuandaa kikosi chetu. Lakini tukiingia uwanjani mambo yanakuwa magumu. Ni upepo mbaya tu msimu huu. Tunajipanga kwa nguvu zote kushinda mechi zilizosalia.
Kuhusu mchezo wa jumapili dhidi ya Azam fc, Asha alisema itakuwa mechi ngumu kwao, lakini wanajiandaa kupata matokeo ili kuepuka kipigo ambacho kitawavunja moyo zaidi mashabiki wao.
Wakati hayo yakijiri kwa upande wa Simba sc, Azam fc wameendelea kufanya vizuri zaidi msimu huu kufuatia ushindi wa mabao 2-0 huko Tanga dhidi ya Mgambo JKT katikati ya wiki.
Afisa habari wa Azam fc, alisema kikosi cha Mcameroon, Joseph Marius Omog kina nia ya kutwaa ubingwa msimu huu na sivinginevyo.
“Mechi zote ni ngumu kwetu. Tunawashukuru wachezaji wetu kwa kuelewa malengo ya Azam fc msimu huu”.
“Wamekuwa wakipigana sana uwanjani. Tunawaheshimu Simba sc, lakini tunajiandaa kuwavaa kwa lengo la kutafuta pointi tatu”. Alisema Jafar.
Azam fc wamekuwa na safu nzuri ya ushambuliaji kutokana na mabao mengi wanayofunga kwa mechi za karibuni.
Wakati huo huo wataingia katika mchezo wa jumapili wakiwa na kumbukumbu ya kuwafunga Simba sc mabao 2-1 mzunguko wa kwanza.
Kipindi hicho, Azam fc walikuwa chini ya kocha, Muingereza, Sterwat John Hall, wakati Simba walikuwa chini ya kocha wake, Abdallah Kibadeni `King Mputa`.
Itakuwa ni vita kali baina ya mabeki wa Simba sc, Haruna Shamte, Issa Rashid `Baba Ubaya` Joseph Owino, Donald Mosoti dhidi ya washambuliaji wa Azam fc John Bocco `Adebayor`, Kipre Tchetche.
Katikati Henry Joseph, Said Ndemla, Omary Salum, William Lucian ‘Gallas’ na Jonas Mkude watakuwa wanachuana na Michael Bolou, Himid Mao, na Salum Abubakar `Sureboy`.
Erasto Edward Nyoni, Michael Gardiel, Aggrey Morris na David Mwantika, watakuwa na kibarua kizito cha kuwazuia Haroun Chanongo, Amisi Tambwe na Ramadhani Singano ‘Messi’ ambao wanategemewa kupangwa siku hiyo.
Kocha wa Azam fc, Joseph Marius Omog amefanikiwa kuifanya Azam kuwa kileleni kwa kutofungwa mechi yoyote msimu huu.
Matajiri hao wa Bongo wameshuka dimbani mara 22 na kujikusanyia pointi 50 kileleni.
Dravko Logarusic, Kocha wa Simba sc, ameshindwa kuipa mafanikio Simba kama ilivyotarajia na mashabiki wake.
Simba inashika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 36.