LAZIMA ukomae!.
Hukuna mchezaji mwenye namba ya kudumu katika kikosi cha mabingwa
watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara, Dar Young Africans msimu huu.
Kocha msaidizi wa klabu hiyo, Charles Boniface
Mkwasa `Master` ameuambia mtandao huu kuwa mabadiliko ya wachezaji yanayofanywa
katika kikosi chao yanatokana na ubora wa wachezaji katika mazoezi.
“Sisi hatujali wewe ni nani. Hutuwezi kumpanga mtu
kwasababu labda ana kitu fulani. Nidhamu ya mazoezi na kuonesha kiwango ndio sababu ya kupangwa
katika mechi. Mabadiliko kwetu ni kitu cha kawaida”. Alisema Mkwasa.
Mkwasa alisema ingizo la Jery Tegete na Hussein Javu
kwenye kikosi chao katika mechi mbili zilizopita kumetokana na kuonesha kiwango
kizuri wakati wa maandalizi na si vinginevyo.
Tegete na Hussein Javu wameonesha kurudi mchezoni na
kuwa mwiba mkali kwa wapinzani, huku Didier Kavumbagu aliyeonekana kuwa chaguo
la kwanza akishindwa kuanza.
Aidha, Mkwasa alisema kila mdau anayefuatilia michezo
ya ligi kuu, lazima anaelewa kuwa ushindani uliopo katika nafasi za juu ni
mkubwa zaidi ya misimu kadhaa nyuma.
“Kila timu imejidhatiti. Kupata ushindi ni lazima
ziwepo jitihada za wachezaji kitimu na binafsi. Nafasi tatu za juu zimekuwa
ngumu na lazima ujipange”. Alisema Mkwasa.
Mkwasa aliongeza kuwa timu zinazokwepa kushuka
daraja zimekuwa na changamoto kubwa katika ushindani, hivyo kama timu iliyopo nafasi nzuri ikashindwa
kujipanga, ni kazi ngumu kupata ushindi.
Mkwasa aliyekuwa kocha mkuu wa Ruvu Shooting
mzunguko wa kwanza, alisema kuwa kwasasa wanajiandaa na mchezo wa machi 30
(Jumapili) dhidi ya MgamboJKT, kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani, Jijini Tanga.
“Kila mechi ni ngumu kwetu. Ndio maana vijana wetu
tunawaambiwa wajiandae kwa kila kitu kitakachotokea uwanjani. Tunakutana na timu
inayotoka kufungwa mabao 2-0”.
“Tunajua
hawatakubali kufungwa kwa mara pili, watahangaika sana, lakini mwisho wa siku
wajue kuwa Yanga ni timu bora zaidi na kongwe, lazima wakubali kufungwa”.
Alisema Mkwasa.
Mkwasa aliwashukuru mashabiki wao kwa kuendelea
kujitokeza kwa wingi katika michezo yao
na aliwaomba kuendelea kuwaunga mkono zaidi ili kufanikisha malengo yao ya
kutwaa ubingwa.
“Mpira bila mashabiki si mpira tena. Nasema tena na
tena, shukurani sana mashabiki wetu kwa kuwa karibu na timu”. Alisema Mkwasa.
Mechi ya jumapili, itakuwa mechi ngumu zaidi kwa
Mgambo kwasababu kupoteza tena baada ya kipigo cha 2-0 kutoka kwa Azam fc,
itakuwa kujipalia mkaa.
Yanga wataingia katika mechi hiyo ya 22 msimu huu
wakiwa na pointi 46 katika nafasi ya pili, huku vinara Azam fc wenye pointi 50
kileleni watakuwa na kibarua dhidi ya Simba sc uwanja wa Taifa.
Baada ya kutoka Tanga, aprili 6 mwaka huu, Yanga
itacheza dhidi ya JKT Ruvu Uwanja wa Taifa.
Aprili 9, Yanga wataikaribisha Kagera Sugar katika
dimba la Taifa jijini Dar es saalam.
Aprili 13 katika dimba la Sh. Amri Kaluta Abeid
jijini Arusha, Yanga watakuwa wageni wa vibonde, JKT Oljoro.
Mechi ya mwisho kwa Yanga itakuwa aprili 19 mwaka
huu ambapo watakabiliana na mahasimu wao, Simba Sc.
No comments:
Post a Comment