*Awachezea kindava wachezaji wa Vital’O, washinda
*Yanga yatainga fainali, kazi ni dhidi ya wenyeji SC Villa
Na Saleh Ally
WIKI ILIYOPITA, Malima na wachezaji wenzake wa Yanga walipata faraja baada ya Francis Kifukwe akiongozana na mfadhiri Abbas Gulamali kutua mjini Kampala na kuwapa dola 200 kila mmoja. Mbele yao kuna mechi ya nusu fainali. Je, itakuwaje?
FURAHA ilikuwa ni kubwa kupita kiasi, tulivuka hadi kuingia nusu fainali bila ya kupata posho na maisha yalikuwa magumu sana. Dola 200 kwa kila mchezaji kwetu ni sawa na milioni mbili.
Tulikuwa na furaha sana na kila mtu niliyepishana naye alikuwa akiimba nyimbo kuonyesha ana furaha kubwa. Tuliishi angalau maisha mapya na mechi yetu ya nusu fainali ilikuwa ni dhidi ya Vital’O ya Burundi.
Wale Warundi walikuwa fiti sana, kila mmoja alikuwa akihofia kukutana nao. Lakini Yanga yetu, ilitaka kukutana na kila timu, hakuhakikishia kipindi kile hata wangekuja Man United wangesema kazi haikuwa ndogo, hata kama wangetufunga lakini wangelala na viatu.
Jamaa walikuwa fiti halafu walicheza kwa kasi sana, lakini nasi tulijibu mashambulizi. Tulianza kupata bao sisi katika dakika ya 19, Kally Ongala aliwatoka na kupachika bao safi sana.
Jamaa waliendelea kutushambulia mfululizo hadi walipopata bao katika dakika ya 31, nakumbuka alifunga jamaa anaitwa Olivier Nyangeko . Unajua nilikuwa naandika kila baada ya mechi, (Malima anatoa kitabu na kumhakikishia mwandishi kuwa kweli yeye ni mtu wa data). Baada ya bao hilo jamaa waliendelea kulisakama lango letu.
Vital’O walifanikiwa kupata bao la pili katika dakika ya 51, Saleh Omar akafunga bao la pili. Lakini ‘hatukulowa’ tulijua tuko vitani na tulitaka kwenda fainali. Tuliendelea kupambana na dakika ya 78, nikawazisha.
Ulikuwa ni mpira wa kona, kawaida nilikuwa nafunga mabao mengi ya vichwa lakini siku hiyo nilifunga kwa mguu. Baada ya kona kuchongwa, kipa alipangua na ule mpira ulinikuta mimi.
(Malima anavuta pumzi kwa nguvu halafu anatabasamu), aisee! Nilipiga shuti kali ambalo sijawahi kupiga maishani mwangu na sidhani kama nitapiga tena. Ngoma ikajaa wavuni na mimi nikakimbia kwenye kibendera.
Bao letu lilionekana kama kuwachanganya Vital’O, kila mmoja mchezaji alianza kumlaumu mwenzake. Sisi tuliona ulikuwa ni wakati wa kuwamaliza maana jamaa walikuwa kama wamekubali vile.
Tuliendelea kushambulia kwa kasi kubwa, Lunyamila na Kally walikuwa aakiwasumbua sana mabeki wa Vital’O ambao walitumia muda mwingi wakiwachezea faulo.
Mimi huku niliendelea kutandaza ubabe kwa mafowadi wao, niliwapa maneno ya kuwaudhi lakini nilicheza kindava ili kuwapoza. Mara nyingi niliwaita watoto ili kuwaudhi.
Ilionekana kama tutakwenda katika dakika 30 za nyongeza, kwani hadi dakika 87 kulikuwa hakuna bao tena. Kila upande ulitaka kwa kushinda lakini mimi niliona kama jamaa walikuwa tayari wameshachoka ingawa walisifiwa kwa kuwa na pumzi na stamina tokea kuanza kwa michuano hiyo.
Huku mashabiki wakionekana wanasubiri kwa hamu dakika ya 30 za nyongeza, Said Mhando alitufungia bao maridadi katika dakika za 90. Uhakika tulikuwa tumesonga hadi fainali.
Tulishajua tunacheza fainali dhidi ya wenyeji SC Villa ambao waliingia baada ya kuwafunga Rayon Sports kwa mabao 2-0. Nakumbuka waliotupia wavuni ni Hassan Mubiru na Charles Kayemba.
Jamaa nao walikuwa fiti sana, halafu ndiyo wenyeji wa michuano hiyo na walichotaka ni kulibakiza kombe nyumbani kwao. Hawakuwa na kitu kingine zaidi.
Lakini kiasi fulani nao waliingia hofu kwetu kutokana na namna tulivyokuwa tumeanza michuano hadi kufikia hapa tulipo. Waliona kama tulibadilika na kuwa hatari sana.
Pamoja na hivyo, walikuwa na hofu kubwa na washambuliaji wetu hasa Kally na Lunyamila aliyekuwa gumzo kubwa pale Kampala kutokana na kazi aliyokuwa anaifanya.
Pia walijua kwenye ulinzi, nilisimama mimi pamoja na watu kama Shabani Ramadhani, kiungo tuna mtu kama Salvatory Edward, haikuwa kazi lahisi.
Wangesema hao Villa wawalete hata baada ya kuwa tumemaliza mechi ngumu dhidi ya Vital’O, sisi hatukuwa na shida. Tungepambana nao na kuwachakaza.
KAZI ni kubwa, Yanga imetinga fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kombe la Kagame) dhidi ya wenyeji SC Villa ya Uganda. Malima na wachezaji wenzake wakawa tayari kupambana. Je, watawaweza wenyeji na nini kitatokea siku ya fainali. USIKOSE MWENDELEZO.