Kama nilivyotoa taarifa jana kuhusu mazungumzo yangu niliyoyafanya na mchezaji wa klabu bingwa ya bara la Asia, Al Sadd, Ally Hassan Afif, mtoto wa mchezaji wa zamani wa Simba, leo hii naanza kuwaletea baadhi ya mazungumzo tuliyoyafanya, mojawapo lilikuwa ni nafasi ya wachezaji wa kitanzania kucheza soka la kulipwa nchini Qatar ambapo sasa kumekuwa kimbilio la wachezaji wengi wakubwa wa umri waliotamba barani ulaya na Amerika.
Akiongelea kuhusu kiwango cha wachezaji wa kitanzania ambao kwa siku za hivi karibuni alipata bahati ya kuwashuhudia wakicheza soka, Ally anasema wachezaji wengi wa kibongo wanaujua sana mpira na wanaweza kucheza nchini Qatar na kujivunia fedha nyingi sana ambazo zitawajengea misingi imara ya maisha yao mbele baada ya soka.
"Kiukweli Tanzania imebarikiwa vipaji vya wachezaji wengi sana, wanacheza mpira vizuri tena kwa kutumia vipaji vyao bila kuwekewa msingi mzuri walipokuwa wadogo. Kwa kipindi ambacho nilichokuwa Tanzania nimepata bahati ya kuwaona wachezaji wengi wazuri hasa kwenye timu ya taifa lakini yule anayevaa jezi namba 15, anaitwa Mwinyi Kazimoto ni hatari sana yule. Jamaa anaujua sana mpira, nakuhakikishia yule kama anakuja Qatar hata mie simuwezi na kipindi kifupi tu atakachocheza kule atakuwa akipokea fedha nyingi huku timu zikigombea saini yake. Mwinyi mie tangu nimuone nimekuwa namfuatilia sana mechi anazocheza, ana kila kitu ambacho kiungo wa timu anapaswa kuwa nacho, anajua sana ndio maana nimempa jina la 'Failasufu" nikiwa na maana ya Mwanafalsafa wa soka. Kwa hakika Mwinyi Kazimoto anapoteza muda wake nchini Tanzania, namshauri aongee vizuri na timu yake ya Simba imruhusu aje ajiunge na timu kubwa huku Qatar ambazo zinaweza kumlipa sio chini dola 40,000 au zaidi kutokana na uwezo wake wa kisoka. Kiukweli amebarikiwa kipaji kikubwa ambacho ni haba kukipata kwa wachezaji wa kawaida."
"Pia nimewaona wachezaji wengine kama Kaseja na Ngassa kwa kweli wale nao wanatakiwa kucheza timu kubwa zaidi wanazozichezea sasa kwa kuwa ni wachezaji wa level ya juu, lakini ama kwa hakika mimi kama mimi Failasufu Mwinyi Kazimoto ni hatari zaidi na nitajaribu kwa njia zote kumleta Qatar."