Search This Blog

Saturday, October 20, 2012

LIVE MATCH CENTRE: YANGA 3 - 2 RUVU SHOOTING (FULL TIME)//// COASTAL 3 - 1(FULL TIME) MTIBWA


FULL TIME 

DK 85: Yanga 3 - 2 Ruvu Shooting

 Dakika ya 77, Young Africans inafanya mnabadiliko, anaingia Juma Seif Kijiko kuchukua nafasi ya Juma Abdul aliyeumia

 Dakika ya 72, Young Africans inafanya mabadiliko, anaingia Hamis Kiiza anatoka Jeryson Tegete

 DK 67: Didier Kavumbangu anaipatia Yanga goli la 3.

Dakika ya 60, Young Africans 2 - 2 Ruvu Shooting.
DK 50: Ruvu wanafanya mabadiliko anatoka Raphael Kyala anaingia Mangasini Mangasini, pia anatoka George Otei anaingia Ayoub Kitala.

 DK 48: Yanga inapata faulo nje kidogo ya eneo la hatari Niyonzima anapiga na inaokolewa.

 Kipindi cha pili cha mchezo,
Young Africans 2 - 2 Ruvu Shooting


 Half Time: Yanga 2 - 2 Ruvu Shoot

Dakika ya 35, Jeryson Tegete anaipatia Young Africans bao la pili - Young Africans 2 - 2 Ruvu Shooting

 Dakika ya 30, Young Africans 1 - 2 Ruvu Shooting
Dakika ya 20, Mbuyu Twite anaipatia Young Africans bao la kwanza

 Dakika ya 15, Young Africans 0 - 2 Ruvu Shooting


Dakika ya 9, Seif Abdallah anaipatia Ruvu Shooting bao la pili.
 
Dakika ya 2, Seif Abdallah anaipatia Ruvu Shooting bao la kwanza.
 
Mpira ndio umeanza hapa Uwanja wa Taifa kati ya
Young Africans Vs Ruvu Shooting


Hiki ndio kikosi cha Yanga kinachoanza leo dhidi ya Ruvu Shooting katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam


1. Yaw Berko
2. Juma Abdul
3. Oscar Joshua
4. Nadir Haroub 'Cannavaro'
5. Mbuyu Twite
6. Nurdin Bakari
7. Rashid Gumbo
8. Haruna Niyonzima
9. Didier Kavumbagu
10. Jeryson Tegete
11. David Luhende

Subs:
1. Ally Mustapha 'Barthez'
2. Ladislaus Mbogo
3. Athuman Idd 'Chuji'
4. Juma Seif 'Kijiko'
5. Shamte Ally
6. Nizar Khalfan
7.Hamis Kiiza

Kutoka Mkwakwani Tanga hiki ndio kikosi cha Coastal Union kinachoanza dhidi ya Mtibwa.


 Kutoka Mkwakwani Juma Jabu anapa uongozi Coastal Union katika dk ya 9.
 
DK 25: Coastal 1 - 0 Mtibwa.
DK 38: Danny Lyanga anaipatia Coastal goli la pili. 

DK 40: Salum Sued anafunga bao kwa upande wa Mtibwa.

 Coastal 2-1 mtibwa HALF TIME

 Mpira umeanza kipindi cha 2.

DK 60: Coastal union 2 Mtibwa 1

DK 70: Coastal union 2 Mtibwa 1

Lameck Dyaton anaipa Coastal bao la 3 kutokana na pasi ya Danny Lyanga. Coastal 3 - 1 Mtibwa. 

DK 90: Coastal Union 3 - 1 Mtibwa 
 

Friday, October 19, 2012

EL HADJI DIOUF: STEVEN GERRARD NI MBINAFSI KULIKO WACHEZAJI WOTE DUNIANI - MAGWIJI WA LIVERPOOL HAWAMPENDI KWA TABIA ZAKE

Baada juzi kuiomba serikali kuwaondoa viongozi wote wa shirikisho la soka la Senegal akiwalaumu kutokana vurugu zilijitokeza kwenye mechi dhidi ya Ivory Coast, leo hii mchezaji mtukutu El Hadji-Diouf  amezungumza tena, na muda huu ametoa tuhuma kali dhidi ya nahodha wake wa zamani wa Liverpool Steven Gerrard.
Katika mahojiano L’Equipe, mshambuliaji wa Leeds alizungumzia kazi yake ya soka na tabia yake yake isiyoridhisha, lakini zilikuwa kauli zake dhidi ya Gerrard ndizo zilizoleta utamu wa mahojiano yake. Maneno ambayo kiukweli yalikuwa yanalenga kujibu mapigo ya Gerrard aliyemuandika vibaya kwenye kitabu chake kwa kumuita msenegali huyo Panya.
“Maneno ya Steven Gerrard? Ni wivu tu. Nilikuwa ndio mchezaji muhimu zaidi kwa kipindi kile, na kila mtu alikuwa akiniangalia mimi. Nilikuwa naisadia sana timu yangu ya taifa na nilifanikiwa mpaka kuipeleka katika robo fainali kwenye World Cup 2002.
“Nilikuwa kwenye listi ya wachezaji bora 100 wa karn waliotajwa na Pele na Gerrard hakuwemo. Namheshimu kama mcheza soka, lakini hakuna mchezaji mbinafsi kama yeye. Alikuwa yupo radhi Liverpool ifungwe lakini yeye afunge bao.
 ”Hajali kuhusu kitu chochote wala mtu yoyote. Nimeongea na magwiji wa Liverpool na wote wanachukizwa na tabia zake."

ANGUKO LA UCHUMI UGIRIKI LASABABISHA KLABU KUDHAMINIWA NA DANGURO - WACHEZAJI WAAHIDIWA MADEMU WAKISHINDA MECHII

Kama ilivyo kwa vitu vingi vingine nchini Ugiriki, klabu za soka nazo zimekumbwa na tatizo la anguko la uchumi, lakini moja ya kampuni ya biashara ambayo yenyewe haijaathiriwa sana na na anguko la uchumi, imeamua kuchukua jukumu la kuisadia klabu moja ya soka ya nchi hiyo iliyopo mjini Larissa.
Kutoka AP:
Wachezaji wa klabu ya Voukefalas wamelazimika kuvaa jezi za pinki zenye logo za "Villa Erotica" na Soula's House of History, wakiwa ndio wadhamini wao wao wapya baada ya nchi hiyo kupigwa na tufani la anguko la uchumi hivyo kupelekea serikali kupunguza matumizi na kuiacha klabu hiyo ikiwa kwenye hali mbaya ya kifedha.
Timu nyingine pia zimekuwa kwenye hali tete ya kiuchumi, kuna klabu moja inadhaminiwa na kampuni inayojishughulisha na masuala ya mazishi huku nyingine ikidhaminiwa na maduka ya kuuza vitafunwa aina ya kebab.
Mmiliki wa kampuni ya Soula's House of History, Soula Alevridou, amelipa zaidi ya €1,000 kuweka jina lake kwenye jezi za pink za Voukefalas, lakini waandaji wa ligi wanajaribu kuizuia klabu hiyo kuvaa jezi hizo kwenye mechi kutokana wanahisi haitaleta picha nzuri kwa mashabiki wenye umri mdogo japokuwa biashara ya kuuza mwili ni halali nchini Ugiriki.
Kwa mujibu wa AP, Voukefalas inahitaji kiasi cha €10,000 kwa mwaka na mwanamama Alevridou, ambaye ni mmiliki wa kampuni inayosimamia danguro amesema ameamua kuidhamini timu hiyo kutokana na kuipenda klabu hiyo na sio kwamba anataka kuitangaza biashara yake ambayo kwa mujibu wake hahitaji matangazo.

Voukefalas mpaka sasa wamepoteza mechi nne mfululizo, lakini Ms.Alevridou amehaidi "muda maalum" kwa wachezaji katika danguro lake ikiwa watashinda.
Mmiliki wa Danguro Soula Alevridou akiwa amebeba jezi mpya ya timu anayoidhamini kupitia kampuni yake

ZENGWE: UWANJA WA KISASA CHAMAZI NA SOKOINE MBEYA UPI UNAFAA KUCHEZEWA MECHI KUBWA???

Kuna taarifa kwamba ombi la Azam FC kutaka mechi dhidi ya Yanga na Simba zichezwe kwenye dimba lao binafsi la Chamazi Complex limepigwa chini na TFF kwa madai ya usalama. Kutokana na hatua hiyo klabu ya Azam FC kupitia ukurasa wao wa mtandao wa Facebook wakatoa hoja kwamba iweje uwanja wenye hali mbaya ya kimazingira na usalama kama Sokoine-Mbeya uruhusiwe kuchezewa mechi kubwa zinazohusisha Simba na Yanga na uwanja wao wa kisasa ukataliwe ku-host mechi hizo??? Je mdau una maoni gani juu ya hili? 

UCHAMBUZI LIGI KUU RAUNDI YA 8: YANGA, KAGERA SUGAR COASTAL UNION, NA MTIBWA SUGAR AKA FC PORTO YA TANZANIA



YANGA SC
Msimu uliopita ilikumbwa na kirusi kikubwa cha migogoro ya kiuongozi ambayo ilichangia matokeo mabovu katika ligi na kuangukia nafasi ya tatu mwishoni mwa msimamo.


 Imejiimarisha kwa kuongeza wachezaji muhimu kwenye nafasi ambazo zilikuwa na mapungufu. Walishtuliwa mapema kwenye ligi baada ya suluhu-pacha siku ya ufunguzi wa msimu dhidi ya Tanzania Prisons na kukutana na kipigo kizito cha mabao 3-0 mbele ya Mtibwa Sugar.

 Wameimarisha na kupandisha kiasi kiwango chao cha uchezaji, huku urejeo wa majeruhi kama, Nurdin Bakary ukirejesha wingi wa machaguo bora kikosini. Imeweza kupanda haraka juu ya msimamo hadi nafasi ya tatu, pointi nane nyuma ya vinara na mahasimu wao Simba ambao wapo kileleni, lakini Yanga wana nafasi ya kufuta ‘gepu’ hilo wakati watakapocheza mchezo wao wa nane dhidi ya Ruvu Shooting hapo jumamosi, kama wakishinda watakuwa nyuma ya vinara kwa tofauti ya pointi tano tu.

UDHAIFU WAO
Yanga inafundishwa na kocha wa nne kwa kipindi cha miezi 12 tu. Alianza, Sam Timbe, akafuatia, Kostadin Papic, kisha Tom Saintfiet na sasa Ernest Brandts. Ni tatizo na udhaifu mkubwa wa timu hii kwa miaka ya karibuni, ingawa wamekuwa wakisajili kwa kiasi kikubwa cha pesa kwa miaka mitano iliyopita, Yanga imeshindwa kuwa timu imara kutokana na mabadiliko yasiyostahili ya makocha, wakati na muda wa kuingia na kutoka kwa makocha ndani ya timu hii huwa si mwafaka. 


UTABIRI. Wanaweza kurejea juu ya msimamo kama watani wao Simba hawatachanga vyema karata zao pale watakapokuwa ugenini dhidi ya Prisons, JKT Mgambo na Polisi Moro. Mategemeo watakuwepo kwenye Top 3.


MTIBWA SUGAR. FC PORTO YA TANZANIA INAYOOGOPA KIVULI CHAKE.
Wakati wanatwaa mataji mfululizo ya ligi kuu katika miaka ya 1999 na 2000, Mtibwa ilitambulisha vipaji kadhaa ambavyo vilitamba katika soka la Tanzania kwa miaka kadhaa, Mecky Mexime, Kassim Issa, Geofrey Magori, Abuubakary Mkangwa na wengine wengi ambao baadae walijiunga na vilabu maarufu vya Yanga na Simba, hata nyakati za kina Nico Nyagawa. Mussa Mgosi na sasa kina Hussen Javu, Babuu Ally na chipukizi kadhaa waliopo katika kikosi cha sasa ni mfano tosha kuwa timu hii kwa kipindi cha miaka 12 isiyo na taji la ligi kuu, imeweza kunufaika na uuzaji wa wachezaji. Wakati bingwa wa ligi kuu akitarajiwa kuingiza zaidi ,illion 70, Mtibwa inaingiza pesa hizo kwa kuuza wachezaji tu.

Mara kadhaa msemaji wa timu hiyo, Thobias Kifaru amekuwa akisisitiza hadi pale haki itakaporejea katika soka la Tanzania ndiyo wataweza kutwaa tena taji la ligi kuu, lakini kwa sasa si rahisi kufanikiwa katika hilo kutokana na aina ya ushindani uliopo katika ligi yetu, Kifaru amekuwa akisisitiza kuwa timu yao ni bora hata zaidi ya Simba na Yanga. Mwenendo wao bado si wa kuridhisha sana katika ligi, na mara baada ya kufungwa na Mgambo wikiendi iliyopita katika uwanja wao wa nyumbani, watakuwa Mkwakwani, Tanga kucheza na Coastal Union, jumamosi hii.


UDHAIFU WAO.
Wanawahi kukata tamaa mapema na imepoteza uwezo wake wa kushinda katika uwanja wao wa Manungu Complex.

COASTAL UNION.
Wana utajiri na wapo katika umbo zuri la ushindani hadi sasa. Mara ya mwisho klabu hii kutwaa taji ni mwaka 1988, pale walipotwaa taji la ligi daraja la kwanza ( sasa ligi kuu). Wamejiimarisha vizuri kiuchumi na kimaandalizi na wakati tayari wamecheza michezo saba, Coastal wamepoteza mara moja na kushinda michezo miwili, huku sare ikiwa imetoka mara nne. Wachezaji wa timu hiyo ni wale ambao walipata kuzichezea klabu za Simba, Yanga na Azam kwa vipindi tofauti. Tayari wamefanya mabadiliko katika benchi lao la ufundi kwa kumtoa, Juma Mgunda na kupewa kazi, Hemed Morocco. Ina wachezaji kama nahodha, Said Sued, Juma Jabu, Jerry Santo, Pius Kisambale, Nsa Job, Atupe Aggreen.
Ukizungumza na wachezaji wa timu hiyo wanadai wanataka kuwemo ndani ya nafasi mbili za juu, kitu ambacho kinamaanisha, Yanga, Simba, Azam au Mtibwa kugombea nafasi moja ya juu kati ya mbili. Ni ngumu na wakiwa tayari wameonesha kutokuwa imara katika uwanja wa nyumbani, Coastal inatakiwa kuonesha vitendo uwanjani na si maneno.
UTABIRI. Wana matarajio makubwa akilini mwao, lakini wanatakiwa kuangaza macho zaidi ili kuona kilichopo mbele yao, kama wataendelea kuangusha pointi nyumbani, watapata wakati mgumu wakienda, Morogoro kucheza na Mtibwa na Polisi, vipi kuhusu uwanja wa Kaitaba na sapoti wa wakazi wa Mwanza kwa Toto? Kisha watatakiwa kuja Dar es Salaam mara sita kwa msimu.


UTABIRI; Kama wasipokuwa makini watajikuta wakipigania kutoshuka daraja mwishoni mwa msimu, ni lazima wakusanye pointi za nyumbani ili kuwa salama.


KAGERA SUGAR;
Chini ya kocha Abdalah Kibadeni, Kagera inacheza soka safi lenye kuvutia, wachezaji wake hawakati tamaa, na wana hali kubwa ya ushindi, kuanzia kwa nahodha, Amandus Nesta, Maregesi Mwangwa, Salum Kanoni, Shija Mkina na utitiri wa vipaji chipukizi, timu hiyo iliweza kutoka nyuma ya mabao 2-0 dhidi ya Simba na kupata pointi moja muhimu katika uwanja wa Taifa. Wamejiimarisha vizuri kuanzia katika utawala hadi ndani ya uwanja. Kuwaondoa wachezaji kama Hussein Sued ilikuwa ni uamuzi mzuri ili kusajiliwa kwa Mnigeri, Enyina Darrington ambaye anaisaidia sana timu hiyo.


UTABIRI;  Timu kama hii unaweza kuifananisha na Everton kwa pale England, huwezi kujua watamalizia wapi mwishoni mwa msimu, imekuwa na udhaifu wa kushindwa kumaliza ligi vizuri na mara mbili walikosa ubingwa baada ya kushindwa kumaliza ligi. Wanawania nafasa ya kucheza michezo ya Super8 msimu ujao hivyo wanaweza kufanya lolote na kuwemo ndani ya ‘top 3’

TUHUMA: SIMBA NA YANGA ZATUHUMIWA KUTUMIA PESA KUIHARIBIA AZAM

KASHFA nyingine imezikumba klabu za Simba na Yanga zikidaiwa kuanzisha kampeni ya kutoa fedha kuhakikisha Azam haipati ubingwa msimu huu ambayo inaitwa 'kampeni didimiza Azam'.

Azam inaonekana kuwa tishio katika harakati za Simba na Yanga kuendelea kutawala soka ya Tanzania kwenye miaka ya karibuni.

Habari ambazo Mwananchi ilizipata zinadai kuwa viongozi wa Simba na Yanga walifanya kikao mwezi uliopita kwenye Hoteli ya Kempinski na kukubalina kwamba watahakikisha Azam haichukui ubingwa msimu huu.

Chanzo hicho kilidai kuwa viongozi hao walikubaliana kutumia mbinu zote kuhakikisha Azam haipati ubingwa, pia waliafikiana kutofanya michezo michafu katika michezo yao.

Mwananchi ilipomtafuta Katibu wa Simba, Evodius Mtawala kujibu tuhuma hizo alisema hana taarifa za kikao hicho cha pamoja na kwamba ndiyo kwanza anazisikia habari hizo.

"Sijawahi kusikia kikao kama hicho ndiyo kwanza nasikia kutoka kwako, sijui lolote," alisema Mtawala.

Naye Katibu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema, "Sielewi taarifa hizo kwani ni siasa ambazo nimekuwa nikizisikia kila wakati hivyo sishangazwi nazo zaidi ya kuangalia majukumu yangu ya kazi yanayonikabili."

"Hivi hizo habari mnazipata wapi? Kikao kama hicho ndiyo nakisikia kwako, hakuna taarifa hizo na wala sijasikia tuhuma kama hizo ambazo mimi naziita ni siasa za soka, acha timu zicheze, ni mapema sana kuanza kuzungumza mambo kama hayo ambayo mimi binafsi siyapi nafasi," alisema Mwalusako.

Hata hivyo chanzo chetu cha habari kilidai kuwa,"Kampeni hiyo imeingia dosari hivi karibuni baada ya viongozi wa Simba kudaiwa kutoa fedha kwa Kagera Sugar walipokuwa wanacheza na Yanga ili wawafunge."

"Tumebaini baada ya hapo viongozi wa Yanga nao wameapa kulipiza kisasa kwa Simba kwa kuhakikisha wanapitisha mikono yao kwa kila mechi watakayocheza ili wasiweze kutetea ubingwa wao," alisema kiongozi huyo aliyedai kuwa alishiriki katika kikao hicho ambaye ndiyo chanzo chetu cha habari hii.

Katika hatua nyingine chanzo hicho kilidai kuwa Azam katika kujihami imeingia katika mchezo mchafu wa kutoa fedha ili watwae ubingwa wa ligi baada ya msimu uliopita kuishia katika nafasi ya pili.

Yanga wanadaiwa walitoa ahadi ya Sh10 milioni kwa wachezaji wa Kagera Sugar kama wangeifunga Simba juzi, lakini kwa sare hiyo vijana wa Kagera walikabidhiwa Sh5 milioni huku Azam wakishutumiwa kutoa Sh7milioni kwa waamuzi wa mchezo huo ili kuwakandamiza Simba.

Akizungumzia tuhuma hizo, mratibu wa timu ya Azam, Patrick Kahemela alisema hawajawahi kutumia fedha ili kuharibu mechi ya Simba.

"Hatuna taarifa zozote juu ya kufanyiwa fitina hizo zaidi ya kuangalia malengo yetu ya kutwaa ubingwa kwa kucheza soka la uwanjani," alisema Kahemela.

Hivi karibuni Kocha wa Kagera Sugar, Abdallah Kibaden aliilamikia TFF kwa kushindwa kuchukua hatua ya kupambana na rushwa michezoni.

"Kutokana na baadhi ya waamuzi kuhongwa fedha na kupindisha sheria za soka, siku zote matokeo huwa mabaya na yasiyotarajiwa," alisema Kibaden.

(Source: www.mwananchi.co.tz)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI




ELECTIONS COMMITTEE

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

MAAMUZI KUHUSU  RUFAA DHIDI YA MAAMUZI YA KAMATI ZA UCHAGUZI VYAMA VYA MPIRA WA MIGUU MKOA WA MBEYA (MREFA), MKOA WA SHINYANGA (SHIREFA) NA MKOA WA DAR ES SALAAA (DRFA).

19 OKTOBA 2012


1.                   Kwa mujibu wa Katiba ya TFF Ibara ya 49(1), Kanuni za Uchaguzi  za wanachama wa TFF, Ibara  ya  10(6), 12(1) na 26(2) na (3), Kamati ya Uchaguzi ya TFF katika vikao vyake vilivyofanyika tarehe 12 na 18 Oktoba 2012 ilijadili michakato ya chaguzi za vyama vya mpira wa miguu vya Mikoa ya Mbeya (MREFA), Shinyanga (SHIREFA) na  Dar es Salaam (DRFA) na  kutoa maamuzi kama ifuatavyo:

(a)                 Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya (MREFA)

(i)                  Rufaa ya Ndg. Charles Makwaza: Kamati ilijadili rufaa iliyowasilishwa na Ndg. Charles Makwaza dhidi ya Kamati ya Uchaguzi ya MREFA, iliyoomba Kamati ya Uchaguzi ya TFF kubatilisha uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya MREFA kumpitisha Ndg. John Mwamwaja kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa MREFA, kwamba hakutekeleza wajibu wa kikatiba wa kuitisha Mkutano Mkuu wa MREFA kwa muda wa miaka 3.

Baada ya kupitia maelezo ya warufani na warufaniwa, Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilijiridhisha kuwa vielelezo na maelezo ya Ndg. Charles Makwaza yaliyowasilishwa mbele ya Kamati kwa kiwango kikubwa hayakuwa ya kweli. Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeitupa rufaa hiyo.

(ii)                Rufaa ya Ndg. Lusekelo E. Mwanjala: Kamati ilijadili rufaa iliyowasilishwa na Ndg. Lusekelo E. Mwanjala ikipinga  maamuzi ya  Kamati ya Uchaguzi ya MREFA kuliondoa jina lake kugombea  nafasi ya Mwenyekiti wa MREFA, kwa kigezo cha kutokuwa na uzoefu wa uongozi wa mpira wa Miguu.

Kamati ilipitia vielelezo kuhusu rufaa na kujadili maelezo ya Mrufani na Mrufaniwa na ilijiridhisha kuwa Ndg. Mwanjala anakidhi kigezo cha uzoefu. Kamati inakubaliana na rufaa ya mrufaa dhidi ya maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya MREFA na hivyo imemrejesha Ndg. Mwanjala kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa MREFA. 


(iii)              Rufaa ya Ndg. Thadeo T. Kalua: Kamati ilijadili rufaa iliyowasilishwa  mbele yake na Ndg. Kalua ikipinga  maamuzi ya  Kamati ya Uchaguzi ya MREFA kuliondoa jina lake kugombea  nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, kwa kigezo cha kutokuwa Mkazi wa Mkoa wa Mbeya. Kamati ilipitia vielelezo kuhusu rufaa hii na kubaini kuwa Katiba ya MREFA iliyosajiliwa haina sharti hilo kwa waombaji uongozi.  Kamati inakubaliana na maombi ya


(iv)               mrufaa na inamrejesha Ndg. Thadeo Kalua kugombea nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF. 

(v)                 Uchaguzi wa MREFA utafanyika Jumamosi, tarehe 27 Oktoba 2012 kama ulivyopangwa.


(b)                Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga (SHIREFA).

(i)                   Rufaa ya Ndg. Ibrahim Magoma: Kamati ilijadili rufaa iliyowasilishwa na Ndg. Magoma ikipinga maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya SHIREFA kuliondoa jina lake kugombea nafasi ya Katibu wa SHIREFA, kwa kigezo cha kuingilia Mchakato wa Uchaguzi kunyume na Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF na pia kutozingatia matakwa ya Kanuni hizo katika kujaza fomu za maombi ya uongozi wa SHIREFA.

Kamati ilipitia vielelezo kuhusu rufaa ya Ndg. Magoma na kujadili maelezo ya Mrufani na Mrufaniwa na ilijiridhisha kuwa Ndg. Magoma  aliingilia mchakato wa uchaguzi wa SHIREFA kunyume na Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF akiwa Katibu Mkuu wa SHIREFA kwa kushiriki kuivunja Kamati ya Uchaguzi ya SHIREFA iliyokuwa ikendelea na mchakato wa uchaguzi wa SHIREFA.  Kamati inakubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya SHIREFA wa kumwondoa Ndg. Magoma kugombea nafasi ya Katibu wa SHIREFA.  Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeitupa rufaa hiyo.

(ii)                 Uchaguzi wa SHIREFA umesogezwa Mbele kwa siku nne. Uchaguzi huo utafanyika Alhamisi, tarehe 25 Oktoba 2012, mjini Shinyanga.


(c)                 Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es salaam (DRFA).

Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilijadili Mchakato wa Uchaguzi wa DRFA na rufaa dhidi ya maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya DRFA  na kuamua kama ifuatavyo:

(i)                   Marekebisho na usajili wa Katiba ya DRFA: Hoja ya rufaa iliwasilishwa na Ndg. Michael R. Wambura ilikihoji uhalali wa marekebisho na usajili wa Katiba ya DRFA, kwamba usajili wa Katiba ya DRFA si halali. Kamati ilibaini kuwa marekebisho ya Katiba hiyo yalifanyika kwa kufuata maagizo ya TFF na kwamba DRFA ilizingatia maagizo hayo. Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliridhika kuwa Katiba ya DRFA imesajiliwa na Msajili wa vyama na vilabu vya michezo baada ya kuridhiwa na TFF, na hivyo, Kamati iliitupa hoja hiyo ya Mrufani kuhusu uhalali na usajili wa Katiba ya DRFA.

(ii)                 Kuundwa kwa Kamati ya Uchaguzi ya TFF : Hoja ya rufaa ya Ndg. Michael R. Wambura iliomba Kamati ya Uchaguzi ya TFF kutoa tamko kuwa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA imeundwa bila kufuata Kanuni za Uchaguzi Ibara ya 3(2). Kamati iliridhika kuwa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA iliteuliwa kabla ya marekebisho ya Kanuni za Uchaguzi  za wanachama wa TFF hususan, Ibara ya 3(2), hivyo uteuzi wa wajumbe wa Kamati hiyo haukukiuka Kanuni za Uchaguzi. Kamati iliitupa rufaa hiyo.

(iii)                Wapiga kura wa Mkutano Mkuu wa DRFA: Hoja za rufaa za Ndg. Michael R. Wambura na Ndg. Juma Jabir ziliomba kuyaondoa majina ya Ndg. Abeid Mziba, Ndg. Salehe Ndonga, Peter Muhinzi na Ndg. Daudi Kanuti katika orodha ya wapiga kura wa Mkutano Mkuu wa DRFA na uongozi wa wanachama wa DRFA, kwamba hawana sifa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi na Katiba za wanachama wa DRFA. Kamati ya Uchaguzi ya TFF haikupata vielelezo kuhusu hoja iliyowasisilishwa mbele ya Kamati na hivyo kuitupa hoja hiyo ya mrufani.

(iv)               Rufaa dhidi ya Ndg. Mohamed Salim (Bakhressa) kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa DRFA.  Rufaa dhidi ya uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA wa kumpitisha Ndg. Amin Mohamed Salim (Bakhressa) kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa DRFA iliyowasilishwa na Ndg. Michael R. Wambura na Ndg. Juma Jabir iliomba jina la Ndg. Amin Mohamed Salim (Bakhressa) liondolewe katika orodha ya wagombea uongozi wa DRFA kwa nafasi ya Mwenyekiti, kwa kuwa hana elimu ya kiwango cha kidato cha nne na hivyo kutokidhi matakwa ya Katiba ya DRFA Ibara ya 29(2) inayotamka kwamba ‘Mtu yeyote anayegombea nafasi yoyote ya DRFA hana budi awe na kiwango cha elimu kisichopungua kidato cha nne (Academic Certificate of Ordinary Secondary Education).

Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilipitia vielelezo kuhusu rufaa dhidi ya maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya DRFA na kujadili maelezo ya Warufani, Kamati ya Uchaguzi ya DRFA na Ndg. Amin Mohamed Salim na ilijiridhisha kuwa Ndg. Amin Mohamed Salim (Bakhressa) hana elimu ya kiwango cha kidato cha nne na hivyo hakidhi matakwa ya Katiba ya DRFA Ibara 29(2). Kwa kutokidhi matakwa hayo ya katiba ya DRFA, Ndg. Amin Mohamed Salim (Bakhressa) hastahili kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa DRFA. Kamati ya Uchaguzi ya TFF inakubaliana na maombi ya Warufaa.

(v)                 Rufaa kupinga kuenguliwa kugombea Uongozi DRFA:  Ndg. Evans Elieza na Ndg. Juma Jabir waliwasilisha rufaa  wakiomba Kamati ya Uchaguzi ya TFF kutengua uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA wa kuwaengua kugombea uongozi kwa madai ya kugushi sahihi ya Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondoni (KIFA). Katika vielelezo mbalimbali vilivyoletwa mbele ya Kamati na baada ya kuwahoji warufani, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA, Katibu wa KIFA, Ndg. Seif Ally Mailo aliyeshuhudia maelezo ya fomu za waombaji uongozi DRFA na baadhi ya waombaji uongozi ambao kupitishwa kwao na Kamati ya Uchaguzi ya DRFA kulilalamikiwa, Kamati ilibaini kuwa kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa Kanuni na taratibu za uchaguzi zilizofanywa na Kamati ya Uchaguzi ya DRFA na pia ama KIFA au wagombea wenyewe. Kutokana na mkanganyiko, maelezo yenye utata kutoka kwa warufani na warufaniwa na maamuzi ya utata ya Kamati ya Uchaguzi ya DRFA yameufanya mchakato wa uchaguzi wa DRFA kupoteza hadhi ya uchaguzi unaozingatia Kanuni za Uchaguzi na misingi ya demokrasia na uwazi kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni za Uchaguzi za TFF. Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilijiridhisha kwamba:

·         Kamati ya Uchaguzi ya DRFA iliwapitisha wagombea Ndg. Gungurugwa Tambaza, Ndg. Mohammed Bhinda, Ndg. Benny Kisaka na Ndg. Hamisi Ayoub Mpapai bila kuwa na vielelezo vinavyothibitisha kuwa wana kiwango cha elimu kisichopungua kidato cha nne (Academic Certificate of Ordinary Secondary Education).

·         Hoja ya kughushi saini ya Katibu wa KIFA katika kushuhudia maelezo ya  baadhi ya wombaji uongozi, ambayo  ilitumiwa na Kamati ya Uchaguzi ya DRFA kuwaondoa kugombea uongozi waombaji uongozi watano (5)  Ndg. Hamis Ambar, Ndg. Hamisi Kisiwa, Ndg. Andrew Tupa, Ndg. Evans Elieza na Ndg. Juma Jabir  haikutumika kuwaondoa baadhi wagombea ingawa fomu za waombaji uongozi saba zilisainiwa na Ndg.  Ndg. Seif Ally Mailo.

·         Ndg. Seif Ally Mailo ambaye si mwajiriwa na si kiongozi wa KIFA hakuwa na mamlaka ya kushuhudia maelezo ya wagombea kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi.

·         Kulikuwa na hali ya kumficha Ndg. Seif Ally Mailo aliyesaini fomu za wagombea walioenguliwa kwa kigezo cha kughushi saini asifike kwenye kamati ya Uchaguzi ya TFF kutoa maelezo kuhusu ushiriki wake katika mchakato wa uchaguzi wa DRFA.

·         Fomu za wagombea Ndg. Said H.Tully na Ndg. Shaffih Dauda zilizojadiliwa na Kamati ya Uchaguzi ya DRFA na hivyo kupitishwa na Kamati hiyo zilichezewa (tempered-with) kwa kunyofolewa baadhi ya kurasa na kuwekwa kurasa zenye maelezo na saini ambazo si za Ndg. Said H.Tully na Ndg. Shaffih Dauda. Wagombea hao ambao walikuwa wamepetishwa na Kamati ya Uchaguzi ya DRFA kwa maelezo kwamba fomu zao zilikuwa zimeshudiwa kwa sahihi halali ya Ndg. Ndg. Seif Ally Mailo



walikana kwa maandishi na kutoa vielelezo vilivyothibitisha kwamba fomu zao zilichezewa na maelezo yaliyo kwenye kurasa zilizobadilishwa siyo wao walioyandika na kusaini.

·         Kamati ya Uchaguzi ya DRFA iliwaondoa baadhi ya waombaji uongozi kwa maelezo kwamba maelezo kwenye fomu za wagombea hao hayakushuhudiwa na viongozi vyama wanachama wa DRFA wenye mamlaka ya kushuhudia maelezo ya waombaji uongozi lakini bila kuzingatia matakwa hayo ya kikanuni ikawapitisha kugombea Ndg. Muhsin S. Balhabou na Ndg. Benny Kisaka ambao maelezo ya kwenye fomu zao hayakushuhudiwa na kiongozi wa chama mwanachama yeyote wa DRFA.

·         Kamati ya Uchaguzi ya DRFA inahusika kwa kiwango kikubwa katika ukiukwaji wa Kanuni na taratibu za uchaguzi na kutozingatia matakwa ya Katiba ya DRFA katika mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa DRFA.

Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuzingatia Katiba ya TFF Ibara ya 49(1), Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara  ya  10(6), 12(1) na 26(2) na (3):

(i)                   Imeifuta Kamati ya Uchaguzi ya DRFA. DRFA inaagizwa kuteuwa Kamati mpya ya Uchaguzi itakayoandaa na kutekeleza majukumu yake ikizingatia Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF na Katiba ya DRFA. Uteuzi wa Kamati mpya ya Uchaguzi ya DRFA ufanyike kabla ya tarehe 25 Oktoba 2012

(ii)                 Imefuta mchakato wa Uchaguzi wa DRFA. Mchakato wa uchaguzi utaanza upya tarehe 29 Oktoba 2012 na uchaguzi utafanyika tarehe 08 Desemba 2012. Wagombea wote waliokuwa wamelipia Fomu za maombi ya uongozi (Fomu Na. 1) wanaokidhi sifa za kugombea uongozi kwa mujibu wa Katiba ya DRFA na Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF wajaze upya Fomu Na.1 bila kutozwa ada kwa nafasi zinazoendana na zile walizokuwa wameomba kugombea.




Deogratias Lyatto
MWENYEKITI
KAMATI YA UCHAGUZI TFF















BREAKING NEWS! AMINI BAKHRESSA APIGWA CHINI,KAMATI YA NDOLANGA YAVUNJWA

Hatimaye gwiji la chama cha soka mkoa wa Dar Es Salaam, Bwana Amini Bakhressa ameondolewa kuendelea kutetea nafasi yake ya uenyekiti wa DRFA baada ya kushindwa kukidhi vigezo.
pia kamati ya uchaguzi ya DRFA chini ya mwenyekiti Alhaj Muhidini Ndolanga imevunjwa kutokana na kushindwa kuusimamia mchakato wa uchaguzi wa DRFA.

Habari zaidi zitafuata!!!!

NEYMAR ATIMIZA MECHI YA 200 NA SANTOS NA GOLI LA HATARI DHIDI YA TIMU YA RONADINHO

Usiku wa juzi nchini Brazili mchezaji Neymar alitimiza mechi ya 200 akiwa na Santos, na kwa bahati nzuri mechi ya 200 ikawa dhidi ya timu anayoichezea Ronaldinho Gaucho Atletico Mineiro. 

Katika kuipa heshima mechi hiyo Neymar akavaa jezi  maalum yenye namba 200 mgongoni kwa usiku huo.  

Huku Santos wakiwa tayari mbele kwa 1-0 kutokana na goli la Miralles alilofunga sekunde kadhaa baada ya mchezo kuanza, Neymar akaja kushindilia msumari kwenye jeneza katika dakika ya 10 ya mchezo kwa goli safi na la uwezo binafsi akiwapita mabeki kadhaa wa Atletico na kwenda kufunga bao kali, na kuifanya siku yake kuwa nzuri zaidi.
Hapa akimsalimia mkubwa wake Ronaldinho

CHEMSHA BONGO YA WIKI: TAJA JINA NA KAZI ANAYOIFANYA MWANAMICHEZO HUYU

TIP: NI KOCHA WA MOJA YA TIMU KUBWA DUNIANI.

UCHAMBUZI: LIGI KUU RAUNDI YA 8 - SIMBA NA AZAM KAMA MAN CITY NA CHELSEA ENGLAND



Na Baraka Mbolembole
Ligi kuu ya Tanzania Bara umeingia katika raundi ya nane jana kwa timu kumi kucheza michezo .  Simba ndiyo inaongoza ligi hiyo hadi sasa. Ifuatayo ni tathimini na uchambuzi wa timu tano ambazo zinateka hisia za wengi katika ligi ya msimu huu.
 MATARAJIO
SIMBA SC. Miaka miwili iliyopita chini ya kocha, Patrick Phiri walimaliza msimu pasipo kupoteza mchezo wowote, na sasa baada ya kutwaa ubingwa msimu uliopita, kocha wa timu hii, Milovan Curkovic anaamini kuwa timu kadhaa ni nzuri lakini anabaki na imani yake aliyojiwekea ya kutwaa taji bila kufungwa msimu huu, Yanga, Azam, Mtibwa Sugar , Coastal Union na Kagera Sugar zinaonekana ni timu zinazotoa ushindani mkubwa katika ligi hiyo.
UDHAIFU WA SIMBA.
Bado timu imeweka imani kubwa kwa Emmanuel Okwi ambaye kimsingi ana mchango mkubwa ndani ya timu hiyo. Haruna Moshi amedai bado hajaridhishwa na mchango wa wacheji wapya wa kulipwa, Paschal Ochieng, Kommabil Keita na Danny Akkuffor. Simba wanacheza vizuri hadi sasa lakini bado timu haina safi imara na nzuri ya ulinzi, kwa mchezo wa juzi dhidi ya Kagera walionesha kutokuwa makini huku kipa namba moja Juma Kaseja akionesha kuchoka mwili. Wataenda kucheza na Mgambo JKT jumapili hii katika uwanja wa Mkwakwani ambap walitoka kuuulalamikia kuwa si mzuri wikiendi iliyopita. Wamepoteza kujiamini na tayari wamepata sare mbili mfululizo baada ya ushindi wa mechi tano za kwanza.


AZAM FC. NI KAMA CHELSEA

Kuna timu mbili ambazo hazijapoteza michezo katika raundi saba za ligi kuu ya Tz Bara na ligi kuu England, wakati Chelsea na Manchester City zikifanya hivyo, England, Simba na makamu bingwa mtetezi Azam FC hajizafungwa katika VPL. Azam ambayo imeruhusu mabao mawili tu ilishinda katika mikoa ya Kagera na Morogoro na ilipata sare jijini Mwanza iliweza kulinda rekodi yao ya kutofungwa jijini Mbeya dhidi ya Prisons kutokana na mchezo wao wa ushirikiano tena pasipo kuwa na mchezaji staa, wachezaji wote wapo katika levo inayofanana kimchezo na kiuwajibikaji. 

UDHAIFU Japo hawajapoteza mchezo wowote huku wakionekana kuimarika zaidi ya msimu uliopita, Azam bado hawaonekani ni wenye kujitolea asilimia ya uchezaji wao wakati wa mchezo, ni timu inayokata tamaa mapema. Imeshinda dhidi ya Kagera Sugar, Polisi Moro na kupata sare dhidi ya Toto Africa na Prisons, lakini wakati wanapokabiliwa na michezo migumu zaidi timu huonesha udhaifu wa 'team work' tatizo ambalo liliwanyima ubingwa msimu wa 2010/11 na kuwapatia, Yanga ambayo haikuwepo katika dalili za ubingwa hadi mechi ya tatu kabla ya ligi kumalizikana dhidi yao ( Azam FC) mechi ambayo, Jerry Tegete alifunga mara mbili huku aliyekuwa kipa namba moja Vladimir Niyonkuru akifukuzwa kwa madai ya hujuma. Baada ya sare ya jana dhidi ya Prisons Azam FC imebaki ni timu ‘isiyofungika’ pamoja na Simba hadi sasa.
UTABIRI.
Wanapigania kutwaa taji la kwanza la ligi katika msimu wake wa tano tangu kupanda daraja. Wamekuwa na bajeti nzuri ya msimu mzima na hata wachezaji si wa kulalamika matatizo kama wale wa timu nyingine, bado wana mtihani mkubwa wa kuwapiku KULWA na DOTTO katika mbinu mbalimbali za kutwaa taji. Kuwa na pesa pekee haitoshi ili kuwa juu ya Yanga na Simba na huu ndiyo mzigo uliowashinda, Moro United na hata Prisons katika miaka ya 2002 na 2008 miaka ambayo walitakiwa kuwa mabingwa wa haki kutokana na mchezo wao. Azam itamaliza ndani ya tatu bora na wakijipanga vizuri wanaweza safari hii wakatimiza ndoto yao ya kutwaa  taji.

SIMBA NA KAGERA SUGAR ZAINGIZA MILLIONI 58 - TIMU ZAGAWANA MILLIONI 22

Pambano la Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Kagera Sugar lililochezwa jana (Oktoba 17 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2 limeingiza sh. 58,505,000.
 
Watazamaji 9,842 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo iliyochezwa kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000, na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 11,013,785.54 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 8,924,491.53.
 
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni posho ya msimamizi wa kituo sh. 120,000, kamishna wa mechi sh. 250,000, waamuzi sh. 440,000, mtathimini wa waamuzi sh. 254,000, mwamuzi wa akiba sh. 70,000, usafi na ulinzi wa uwanja sh. 2,350,000 na Wachina (stadium technical support) sh. 2,000,000.
 
Umeme sh. 300,000, maandalizi ya uwanja (pitch preparation) sh. 400,000, ulinzi wa mechi sh. 3,500,000 wakati tiketi ni sh. 3,183,890. Gharama za mchezo sh. 3,671,261.85, uwanja sh. 3,671,261.85, Kamati ya Ligi sh. 3,671,261.85, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,202,757.11 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,468,504.74.

 
TFF, FKF ZAANZISHA USHIRIKIANO MPYA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya (FKF) wamefikia makubaliano ya kushirikiana katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuinua kiwango cha mpira wa miguu katika nchi hizo.
 
Akizungumza baada ya mkutano uliowakutanisha vinara wa mashirikisho hayo Dar es Salaam jana, Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema wameamua kurejesha uhusiano huo uliokuwepo zamani baada ya kuwepo utulivu katika uendeshaji mpira wa miguu nchini Kenya.
 
Amesema maeneo ya ushirikiano ambayo wameagiza yafanyiwe kazi na sekretarieti za pande zote (TFF na KFF) ili baadaye yaingizwe katika Hati ya Makubaliano (MoU) ni mafunzo, waamuzi, mechi za timu za Taifa za wakubwa, vijana na wanawake, na Ligi Kuu.
 
Rais Tenga pia amesema wameamua kuwepo ziara za mafunzo (study tours) katika maeneo mbalimbali ambapo kwa Kenya wao Ligi Kuu yao iliingia katika mfumo wa kampuni mapema, hivyo itakuwa fursa nzuri kwa Bodi ya Ligi Kuu ambayo iko kwenye mchakato wa kuanzishwa kupata uzoefu kwa wenzao wa Kenya.
 
Naye Rais wa FKF, Sam Nyamweya aliyefuatana na Makamu wake wa Rais, Robert Asembo amesema ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya ni wa kihistoria, hivyo wameamua kuuanzisha upya kwa faida ya nchi hizo.
 
Amesema hivi karibuni FKF ilichukua waamuzi kutoka Tanzania waliochezesha mechi ya kirafiki kati ya Kenya (Harambee Stars) na Afrika Kusini (Bafana Bafana), hivyo wameamua kubadilishana waamuzi kwa lengo la kuwaongezea uzoefu.
 
“Waamuzi wa Tanzania walichezesha vizuri mechi ile. Unajua kwetu kuna upinzani mkubwa katika klabu kama AFC Leopards na Gor Mahia, ukipanga refa utasikia wengine wanalalamika, mara huyo ni Mjaluo. Hata akichezesha vizuri bado watalalamika tu kutokana na upinzani uliopo katika klabu hizo,” amesema.
 
Rais Nyamweya ameongeza kuwa ili kuondoa malalamiko katika mechi za aina hiyo wanaweza kuchukua waamuzi kutoka Tanzania, na vilevile waamuzi kutoka Kenya wakachezesha mechi za aina hiyo nchini Tanzania.
 
Amesema vilevile wamepanga kuangalia uwezekano wa kuwa na mechi za kuandaa timu kabla ya kuanza Ligi Kuu za nchi hizo ambapo washindi watatu au wanne wa kwanza katika ligi hizo kushindana.
 
Kwa upande wa mafunzo, wamekubaliana kuwa kwa vile kila nchi ina wakufunzi wanaotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na la Afrika (CAF) watawatumia kuandaa mafunzo ya mara kwa mara kwa waamuzi, makocha, madaktari wa tiba ya michezo na viongozi badala ya kusubiri mafunzo ya aina hiyo kutoka kwa mashirikisho hayo ya kimataifa.