KASHFA nyingine imezikumba klabu za Simba na Yanga zikidaiwa kuanzisha
kampeni ya kutoa fedha kuhakikisha Azam haipati ubingwa msimu huu ambayo
inaitwa 'kampeni didimiza Azam'.
Azam inaonekana kuwa tishio katika harakati za Simba na Yanga kuendelea kutawala soka ya Tanzania kwenye miaka ya karibuni.
Habari
ambazo Mwananchi ilizipata zinadai kuwa viongozi wa Simba na Yanga
walifanya kikao mwezi uliopita kwenye Hoteli ya Kempinski na kukubalina
kwamba watahakikisha Azam haichukui ubingwa msimu huu.
Chanzo
hicho kilidai kuwa viongozi hao walikubaliana kutumia mbinu zote
kuhakikisha Azam haipati ubingwa, pia waliafikiana kutofanya michezo
michafu katika michezo yao.
Mwananchi ilipomtafuta Katibu wa
Simba, Evodius Mtawala kujibu tuhuma hizo alisema hana taarifa za kikao
hicho cha pamoja na kwamba ndiyo kwanza anazisikia habari hizo.
"Sijawahi kusikia kikao kama hicho ndiyo kwanza nasikia kutoka kwako, sijui lolote," alisema Mtawala.
Naye
Katibu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema, "Sielewi taarifa hizo
kwani ni siasa ambazo nimekuwa nikizisikia kila wakati hivyo sishangazwi
nazo zaidi ya kuangalia majukumu yangu ya kazi yanayonikabili."
"Hivi
hizo habari mnazipata wapi? Kikao kama hicho ndiyo nakisikia kwako,
hakuna taarifa hizo na wala sijasikia tuhuma kama hizo ambazo mimi
naziita ni siasa za soka, acha timu zicheze, ni mapema sana kuanza
kuzungumza mambo kama hayo ambayo mimi binafsi siyapi nafasi," alisema
Mwalusako.
Hata hivyo chanzo chetu cha habari kilidai
kuwa,"Kampeni hiyo imeingia dosari hivi karibuni baada ya viongozi wa
Simba kudaiwa kutoa fedha kwa Kagera Sugar walipokuwa wanacheza na Yanga
ili wawafunge."
"Tumebaini baada ya hapo viongozi wa Yanga nao
wameapa kulipiza kisasa kwa Simba kwa kuhakikisha wanapitisha mikono yao
kwa kila mechi watakayocheza ili wasiweze kutetea ubingwa wao," alisema
kiongozi huyo aliyedai kuwa alishiriki katika kikao hicho ambaye ndiyo
chanzo chetu cha habari hii.
Katika hatua nyingine chanzo hicho
kilidai kuwa Azam katika kujihami imeingia katika mchezo mchafu wa kutoa
fedha ili watwae ubingwa wa ligi baada ya msimu uliopita kuishia katika
nafasi ya pili.
Yanga wanadaiwa walitoa ahadi ya Sh10 milioni
kwa wachezaji wa Kagera Sugar kama wangeifunga Simba juzi, lakini kwa
sare hiyo vijana wa Kagera walikabidhiwa Sh5 milioni huku Azam
wakishutumiwa kutoa Sh7milioni kwa waamuzi wa mchezo huo ili
kuwakandamiza Simba.
Akizungumzia tuhuma hizo, mratibu wa timu ya
Azam, Patrick Kahemela alisema hawajawahi kutumia fedha ili kuharibu
mechi ya Simba.
"Hatuna taarifa zozote juu ya kufanyiwa fitina
hizo zaidi ya kuangalia malengo yetu ya kutwaa ubingwa kwa kucheza soka
la uwanjani," alisema Kahemela.
Hivi karibuni Kocha wa Kagera
Sugar, Abdallah Kibaden aliilamikia TFF kwa kushindwa kuchukua hatua ya
kupambana na rushwa michezoni.
"Kutokana na baadhi ya waamuzi
kuhongwa fedha na kupindisha sheria za soka, siku zote matokeo huwa
mabaya na yasiyotarajiwa," alisema Kibaden.
(Source: www.mwananchi.co.tz)
No comments:
Post a Comment