Makocha
wa Tanzania (Taifa Stars), Kim Poulsen na Zambia (Chipolopolo) watakuwa
na mkutano na waandishi wa habari utakaofanyika kesho (Desemba 21 mwaka
huu) kuzungumzia pambano lao litakalochezwa Jumamosi (Desemba 22 mwaka
huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mkutano
huo utafanyika saa 5 asubuhi kwenye ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Makocha hao watazungumzia maandalizi yao
ya mwisho kabla ya pambano hilo litakalochezeshwa na mwamuzi Sylvester
Kirwa kuanzia saa 10 kamili jioni.
Pia
makocha hao watajibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari kuhusu
pambano hilo litakalokutanisha timu hizo ambazo zimefanya vizuri kwenye
orodha ya viwango vya ubora vya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa
Miguu (FIFA) vilivyotolewa jana (Desemba 19 mwaka huu).
Wakati
Zambia ambao ni mabingwa wa Afrika wamepanda juu kwa viwango vya ubora
kwa nafasi nne, Taifa Stars ambayo katika mchezo uliopita iliifunga
Kenya (Harambee Stars) bao 1-0 imepanda kwa nafasi nne.
Taifa
Stars ambayo inadhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager iko kambini
tangu Desemba 12 mwaka huu kujiandaa kwa mechi hiyo kubwa ya kirafiki
inayotarajiwa kuwa ya kuvutia.
TENGA ATOA NOTISI YA MKUTANO MKUU TFF
Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ambaye
ndiye Mwenyekiti wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho hilo tayari ametoa notisi
ya mkutano huo utakaofanyika Februari 23 na 24 mwakani jijini Dar es
Salaam.
Mkutano
huo utafanyika Februari 23 mwakani na kufuatiwa na ajenda ya uchaguzi
siku inayofuata. Ajenda ya uchaguzi iko chini ya Kamati ya Uchaguzi ya
TFF.
Notisi
hiyo imetumwa kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu ambao ni kutoka vyama vya
mpira wa miguu vya mikoa, vyama shiriki, klabu za Ligi Kuu ya Vodacom na
wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF.
Ajenda za Mkutano Mkuu zitatumwa kwa wajumbe siku 15 kabla ya mkutano huo wenye wajumbe zaidi ya 100.
NUSU FAINALI UHAI CUP KUPIGWA KARUME
Mechi
za nusu fainali ya michuano ya Kombe la Uhai 2012 inayoshirikisha timu
za vijana wenye umri chini ya miaka 20 za klabu za Ligi Kuu ya Vodacom
zitachezwa kesho (Desemba 21 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya
Karume, Dar es Salaam.
Nusu
fainali ya kwanza ya michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Said
Salim Bakhresa kupitia maji Uhai itazikutanisha timu za Mtibwa Sugar ya
Morogoro na Azam na itafanyika kuanzia saa 2 kamili asubuhi.
Simba
na Coastal Union zitacheza nusu fainali ya pili kuanzia saa 10 kamili
jioni kwenye uwanja huo huo. Mtibwa Sugar imepata tiketi ya nusu fainali
baada ya kuichapa African Lyon mabao 3-1 wakati Simba iliilaza Oljoro
JKT mabao 2-0.
Nayo
Azam iliindoa JKT Ruvu kwenye robo fainali kwa bao 1-0 huku Coastal
Union ikipata ushindi wa penalti 4-3 dhidi ya Ruvu Shooting kwenye mechi
ya mwisho ya robo fainali.
Mechi
ya fainali na ile ya kutafuta mshindi wa tatu zitachezwa Jumapili
(Desemba 23 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es
Salaam. Mechi ya mshindi wa tatu itaanza saa 2 kamili asubuhi wakati ya
fainali itakuwa saa 10 kamili jioni.