Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesema ipo haja kwa Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kufikiria
upya uamuzi wake wa kutengua usajili wa Katiba ya TFF ya mwaka 2012 na
kutaka itumike ya mwaka 2006, kwani hautekelezeki.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo mchana, mara baada ya kikao cha Kamati ya
Utendaji, Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema ni muhimu jambo hilo
likaangaliwa upya kwa sababu athari zake ni mbaya, na pengine Dk.
Mukangara hakushauriwa vizuri kabla ya kufanya uamuzi huo.
“Kamati
ya Utendaji ya TFF haitaki kubishana na Mheshimiwa Waziri hata kidogo,
ila tunaamini wakati anatamka haya hakufahamu madhara yake, athari zake
na ugumu wa utekelezaji wake. Kwa waliomshauri hili, wamemshauri
vibaya,” amesema Rais Tenga.
Amesema
rai ya TFF kwa Waziri ni kuwaita ili wamweleze ni kitu gani wafanye
kunusuru mpira wa miguu wa Tanzania, kwani wanaamini jambo hili
litakwisha baada ya kumwelimisha hasa kutokana na ukweli kuwa kabla ya
kufanya uamuzi huo hakuwasikiliza.
Katika
mkutano huo, Rais Tenga alianza kwa kusema kuwa TFF inaiheshimu sana
Serikali, hivyo inaheshimu maagizo yaliyotolewa na Waziri, lakini
akaongeza kuwa TFF ina wajibu wa kutoa ufafanuzi juu ya maagizo hayo.
Amesema
lengo la kuelezea historia ya TFF ilikotoka ni kubaini migongano ya
maagizo hayo na taratibu za TFF ambazo kwa bahati mbaya zinasigana na
maagizo hayo.
Rais
Tenga amesema TFF ni chombo cha wanachama, ambapo wanachama wake ni
vyama vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu, na ina taratibu za
kufanya uamuzi kwa mujibu wa Katiba yake na za wanachama wake ambazo
zimeidhinishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema
si TFF pekee, bali vyama vya nchi zote ambavyo vimeunganishwa na
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), zinaheshimu na kufuata
maagizo na miongozi ya shirikisho hilo la kimataifa la mpira wa miguu.
Rais
Tenga amesema TFF haitakiwi kuingiliwa katika uongozi na uendeshaji
wake, kwani jambo hilo likitokea rungu la FIFA litaiangukia TFF, na
madhara yake ni makubwa. Miongozo ya FIFA inasisitiza uhuru wa wanachama
wake katika uendeshaji shughuli za mpira wa miguu, na iko kwenye Katiba
ya TFF.
“Sheria
za nchi ndizo zilizozaa Katiba ya TFF. TFF ni chama kamili kinatakiwa
kufanya uamuzi wake ili mradi uzingatie madhumuni ya kuanzishwa kwake.
Leo TFF ikiacha mpira wa miguu na kuanza kujishughulisha na gofu, hapo
Msajili ana haki ya kuingilia,” amesema Rais Tenga.
Kuhusu
maagizo ya Waziri, Rais Tenga amesema kifungu cha 11 cha Sheria ya
Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kinazungumzia usajili wa chama, na si
marekebisho ya katiba, ingawa kanuni zinahusu marekebisho ambapo
ameongeza kuwa uamuzi wa marekebisho ni wa Mkutano Mkuu na si Msajili.
“Ukienda
kuomba viza, fomu unapewa na yule anayekupa viza. TFF tulipowasilisha
marekebisho ya Katiba hatukupewa fomu. Msajili akasema sawa. Jambo la
kujaza fomu si la TFF, ndiyo maana tunasema ipo haja ya jambo hili
kufikiriwa upya.
“Usajili
tayari umepita, kwamba Msajili hakutoa fomu, mwathirika anakuwaje TFF?
Tunaona ni muhimu jambo hili likaangaliwa upya,” amesema Rais Tenga na
kuongeza kuwa utaratibu wa kusajili Katiba ya 2006 ambayo ndiyo Waziri
ameagiza itumike ulikuwa huo huo uliosajili Katiba ya 2012.
Akizungumzia
historia ya TFF kutoka mikononi mwa BMT, Rais Tenga amesema ni zao za
Katiba ya 2004 ambayo ilifanyiwa marekebisho ukumbini na kugongwa mhuri
na Msajili hapo hapo na kuingia kwenye uchaguzi. Katiba hiyo ndiyo
iliyoiondoa BMT kuisimamia TFF.
“Huko
ndiko tulikotoka, si kwa kulazimishwa, bali kwa kupewa Katiba ya 2004.
Katiba ina utaratibu mzima wa kufanya uamuzi. Maelekezo ya Waziri
yamesahau huko tulikotoka siku nyingi. Uhalali wa marekebisho unatokana
na ridhaa ya Mkutano Mkuu. Hiyo ni kwa mujibu wa Katiba yenyewe, hakuna
nafasi ya BMT,” amesema.
Amesema
katika maagizo ya Waziri, ameitaka TFF kufuata Katiba ya 2006 na kanuni
za BMT, lakini Katiba hiyo hiyo ya 2006 haina nafasi ya BMT, na hata
kama TFF ingetaka kutekeleza hilo haliwezekani.
“Kwa
maagizo haya inaonekana Waziri kashauriwa vibaya. Tunajua hakuwepo
katika nafasi hiyo (2004) wakati wa makubaliano kati ya Serikali na FIFA
kuacha mpira wa miguu ujiendeshe wenyewe,” amesema Rais Tenga.
Pia
amezungumzia umuhimu wa Katiba toleo la 2012, kwani kuna marekebisho
mengi yalifanyika mwaka 2007, 2008, 2009 na 2011 ambapo ukiyafuta maana
yake unakiweka pembeni Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), Bodi ya
Wadhamini, wanachama wapya (mikoa), Bodi ya Ligi, Kamati ya Rufani ya
Uchaguzi, Leseni za Klabu na Kanuni za Fedha.
“Kwa
uamuzi huu yote yaliyofanyika hayana maana. Waziri sidhani kama alikuwa
anafahamu athari za maagizo yake. Kama angelijua asingefanya uamuzi
huo. Si rahisi kurudi katika Katiba ya 2006. Hao wajumbe wa Katiba ya
2006 unawapata wapi? Maana yake hata vyama wanachama ni batili kwa vile
vimerekebisha Katiba zao 2009 na 2010,” amesema Rais Tenga.
Amesema
kwa Serikali kufuta, maana yake ni kutengua uamuzi wa TFF ambapo
madhara yake ni nchi kufungiwa, ambapo timu za Taifa hazitacheza mpira,
klabu hazitashiriki michuano ya kimataifa na wadhamini nao watakaa
pembeni kwa vile hawawezi kudhamini timu ambazo hazishindani kimataifa.
“Dhana
kwamba tukae tu tusicheze nje, ni dhana ya watu walio nje ya mpira wa
miguu. Dhamira yetu ni kuhakikisha hatufungiwi. Waziri ametuagiza
tupeleke barua FIFA kuwa ametengua marekebisho ya katiba. Hatupeleki
hivyo, kwani hiyo ni Government interference, watatufungia.
“Nia
yetu bado ni Waziri kutupa nafasi ya kutusikiliza,” amesema Rais Tenga
na kuongeza kuwa kuhusu uchaguzi kwa vile FIFA wanakuja ombi la TFF kwa
Waziri ni kuacha kwanza mchakato uendelee hadi ufike mwisho.
“FIFA
wanakuja, tuwasubiri. Nilidhani utaratibu huo utaheshimika. Kama mtu wa
mpira haitaki FIFA anataka nini? Ahadi yetu ni kuhakikisha watu
wanapewa haki. Hiyo ndiyo ahadi yetu na tumeisimamia, na ndiyo maana
FIFA wanakuja,” amesema.
Akijibu
swali kuhusu waraka, Rais Tenga amesema marekebisho ya Katiba
hayakufanywa kwa siri, ridhaa ya wajumbe wa Mkutano Mkuu kufanya
marekebisho hayo kwa njia ya waraka ilipatikana ambapo 70 waliunga mkono
na 33 walikataa.