AZAM FC imenunua chakula chake binafsi kwa hofu
ya hujuma wakati ikitarajiwa kuwasili leo Jumamosi kujiandaa na mechi
dhidi ya Al Nasri kesho Jumapili.
Uongozi umenunua mchele mjini Nairobi, Kenya wakati mchele mwingine
unatarajiwa kuletwa leo Jumamosi mjini Juba na viongozi wengine wa Azam.
Hata hivyo jumla ya kilo 30 za mchele zilinunuliwa Juba kwa ajili ya
chakula cha wachezaji. Kwa mujibu wa Watanzania wanaoishi mjini Juba
walisema, tatizo la kuwekeana sumu katika chakula mjini Juba ni suala la
kawaida hivyo inabidi kuwa makini muda wote.
Watu wa hapa Juba bado wana tatizo la kumalizana kwa kuwekeana sumu
katika chakula, hata sisi wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa hatupikiwi
chakula cha pamoja, sisi hununua chakula chetu na kila mtu
hujipikia, alisema Kassim Matokeo ambaye ni Mtanzania anayefanya kazi
katika ofisi za Umoja wa Mataifa hapa Sudan ya Kusini.
Tayari viongozi wa Azam waliotangulia kwa ajili ya kuandaa mazingira
hapa Juba wameshaandaa utaratibu kwa ajili ya kupika wenyewe chakula
hicho cha wachezaji ili kuepuka kuhujumiwa.
Azam itakabiliana na Al Nasri katika mechi ya marudiano ya Kombe la
Shirikisho la Soka Afrika. Katika mechi ya kwanza Azam ilishinda 3-1 Dar
es Salaam.
Msafara wa Azam utakaokuwa na viongozi na wachezaji 20 utawasili saa 8:20 mchana ikitokea Dar es Salaam kupitia Nairobi.
Hali ya hewa hapa Jua ni jua na joto kali linalofikia nyuzi 40
ingawa wenyeji wanadai huongezeka zaidi ya hapo. Mji wa Juba unatumia
umeme wa majenereta.
Uongozi wa Azam umeikataa Hoteli ya South Sudan ambayo ilikuwa imeandaliwa na wenyeji wao.
Mratibu wa Azam, Florian Kaijage akiwa na kocha msaidizi wa Azam,
Kally Ongala waliikataa hoteli hiyo na kuchukua Hoteli ya Rainbow.
Gharama za hoteli hapa Juba zipo juu kwani hoteli zipo chache. Chumba kinaanzia dola 100(sh.160,000) kwenda juu.
SOURCE: GAZETI LA MWANASPOTI
No comments:
Post a Comment